SUA yawajengea uwezo wananchi wanaoshiriki biashara ya kaboni – HabariLeo

MOROGORO: Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kupitia Mradi wa Tathmini ya Mapato ya Kaboni kama Njia Endelevu ya Uwezeshaji Kifedha katika Uhifadhi na Usimamizi wa Misitu ya Jamii Tanzania kimewajengea uwezo maafisa na wananchi kutoka maeneo yenye hifadhi za misitu ya vijiji pamoja na baadhi ya vijiji vyenye misitu ya hifadhi za vijiji ambao wanashiriki biashara ya kaboni na wemeshapata mapato yanayotokana na biashara hiyo.

Wakizungumza wakati wa mafunzo hayo, wananchi wa vijiji ambavyo havijaanza kunufaika na mapato ya kaboni akiwemo Mwanangao Msanya kutoka wilayani Mvomero mkoani Morogoro amesema wamekuwa wakihifadhi misitu ya Kijiji kwa muda sasa lakini mafunzo hayo yamewapa uelewa mpya wa vigezo na taratibu za kuingia na kunufaika na biashara ya kaboni.

Ofisa Misitu Mwandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Siima Bakengesa, akifungua warsha hiyo iliyohusisha wadau kutoka asasi za kiserikali na asasi zisizo za kiserikali na baadhi ya wananchi wa Wilaya za Tanganyika, Mbulu, Mvomero, Mwanga na Korogwe, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuimarisha uhifadhi wa bioanuwai na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia usimamizi shirikishi wa misitu ya vijiji.

Mtafiti Kiongozi wa Mradi, Dk. Kajenje Nkukurah amesema SUA inaamini mafunzo hayo yatawezesha vijiji ambavyo bado havijaingia katika biashara ya kaboni kufanya maamuzi sahihi kuhusu ushiriki wao pamoja na kuimarisha utawala na usimamizi wa mapato katika ngazi ya vijiji.

Aidha amesema mradi unalenga kuwajengea uwezo wananchi wa vijiji vyenye misitu iliyo katika biashara ya kaboni ili waweze kuendelea kunufaika kiuchumi kupitia biashara ya kaboni, huku mapato yakitumika katika usimamizi endelevu wa misitu ya hifadhi ya vijiji na kuchochea maendeleo endelevu.

Akitoa ushuhuda wakati wa kuwasilisha sauti za jamii, Ofisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Bruno Mwaisaka amesema wilaya hiyo imepokea zaidi ya shilingi bilioni 34 kutokana na biashara ya kaboni ambapo fedha hizo zimechangia kuboresha ustawi wa jamii kupitia ujenzi wa shule, vituo vya afya na kutoa ajira za muda kwa wananchi huku pia zikiongeza ari ya jamii kushiriki katika uhifadhi na usimamizi wa misitu.

Mradi wa Tathmini ya Mapato ya Kaboni kama Njia Endelevu ya Uwezeshaji Kifedha katika Uhifadhi na Usimamizi wa Misitu ya Jamii Tanzania ni wa miaka mitatu unaotekelezwa na SUA kama taasisi inayoongoza, kwa kushirikiana na NCMC na Chuo Kikuu cha Bangor cha Uingereza ukifadhiliwa na Defra kupitia GCBC, DAI, ISPF pamoja na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza.

Serikali yasisitiza usahihi wa taarifa – HabariLeo

DAR ES SALAAM: Serikali imesisitiza umuhimu wa kusimamia uadilifu, usahihi na ukweli katika mnyororo wa taarifa, hasa katika kipindi hiki ambacho teknolojia ya kidijitali imeongeza kasi ya upatikanaji na usambazaji wa habari.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa (IDUAI), kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari MAELEZO, Evordy Kyando, Mkurugenzi Msaidizi wa Usajili wa Idara hiyo, amesema Serikali inatambua umuhimu wa majukwaa ya wadau wa habari katika kujitathmini na kusikiliza maoni kuhusu utekelezaji wa wajibu wake wa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, kwa wakati na zinazoweza kuthibitishwa.

Kyando amesema mazingira ya sasa ya kidijitali yameleta changamoto kutokana na taarifa kusambazwa kwa urahisi na kwa kasi kupitia intaneti, mitandao ya kijamii, simu janja na teknolojia mpya, ikiwemo akili bandia (AI), hali inayoweza kuchangia kuenea kwa taarifa potofu na kuathiri maamuzi ya wananchi.

Ameongeza kuwa upatikanaji wa taarifa ni haki ya msingi kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku Serikali ikiendelea kuweka mifumo na kuboresha sheria zinazoratibu upatikanaji wa taarifa.

Aidha, amesema mapambano dhidi ya taarifa potofu (misinformation) na taarifa zinazotumiwa kwa nia ya kupotosha au kudhuru (malinformation) hayawezi kuachiwa Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa waandishi wa habari na wadau wote wa uhuru wa habari.

Amesisitiza umuhimu wa kila mdau kuhakikisha taarifa zinahakikiwa kabla ya kutumiwa au kusambazwa, huku akieleza kuwa Serikali iko tayari kusikiliza tathmini na kushiriki katika mijadala kuhusu utekelezaji wa sheria za upatikanaji wa taarifa, huduma za vyombo vya habari na sheria nyingine zinazohusiana na sekta hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Mwenyekiti wa Muungano wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI), Ernest Sungura, amesema upatikanaji wa taarifa pekee hautoshi katika zama za kidijitali, bali wananchi wanahitaji taarifa zinazopatikana kwa wakati, zilizo sahihi na zinazoweza kuaminika.

Sungura amesema mazingira ya sasa yamejaa taarifa potofu, taarifa zilizopotoshwa, picha na video zilizohaririwa pamoja na maudhui yanayotengenezwa kwa kutumia akili bandia, hali inayoweza kufanya iwe vigumu kwa wananchi kutofautisha taarifa halisi na bandia.

Amesema kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya upatikanaji wa taarifa na uadilifu wa taarifa, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha taarifa zinazotolewa na kusambazwa zinazingatia ukweli na usahihi.

Serikali yatambua mchango wa Saccos ustawi wa watu – HabariLeo

MOROGORO: SERIKALI imesema inatambua kuwa vyama vya ushirika na saccos nchini vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi kwa wananchi na kwa kupitia Saccos  wanaweza kuweka akiba, kupata mikopo kwa masharti nafuu , kukuza biashara na kuimarisha ustawi wa familia.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu  Munde, amesema hayo akifungua mkutano mkuu wa 13 wa mwaka wa wawakilishi wa Hazina Saccos Ltd mjini Morogoro .

Mkutano mkuu huo ulilenga kujadili taarifa mbalimbali na kupitia hali ya kifedha , kutathimini utekelezaji wa maamuzi ya mkutano mkuu uliopita, kuweka vipaumbele kwa kipindi kijacho na kufanyika uchaguzi wa viongozi wapya.

Naibu Waziri amesema Serikali kupitia Wizara hiyo inaziagiza  Saccos ikiwemo ya  Hazina iendelee kuwa mfano wa chama kinachotoa huduma  bora , kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni , miongozo ya serikali na kutuza  fedha za wanachama.

Amesema kupitia Saccos zao wananchi wanaweza kukusanya nguvu zao za kiuchumi na kupata huduma ambazo wakati mwingine ni vigumu kuzipata wakiwa mmoja mmoja .

“ Kuna umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa Saccos ili ziongeze weledi , uwazi na uwajibikaji,” amesisitiza Mhandisi  Munde.

Mhandisi Munde amesema mikopo inatotolewa na Hazina Saccos  imewawezesha wanachama wake kuendesha biashara , kujenga nyumba , kugharamia elimu , kukabiliana na dhoruba na kutekeleza shughuli za maendeleo.

Ameipongeza Hazina Saccos kwa utoaji wa mikopo kwa wanachama ambapo  wanawake  wameendelea kuwa kundi kubwa la wakopaji wakiwa ni asilimia 55.4 .

“ Jambo hili ni kubwa na  kama inavyofahamika  hata iliyokuwa kwenye asilimia 10  na sasa asilimia 15 ya mapato ya ndani ya Halmashauri , wakopaji na walipaji wazuri ni wanawake” amesema Mhandisi Munde.

Amesema kuwa inaonesha Hazina Saccos ina nachangia kuwezesha wanawake kiuchumi na kutekeleza azma ya serikali ya kuongeza ujumuishi kwa kifedha.

Mhandisi Munde  ameitaka Menejimenti ya Hazina Saccos kuhakikisha kuwa fedha za wanachama zinalindwa kwa kiwango cha juu ambalo ni matumaini makubwa ya wanachama.

Amewataka wanachama kutumiza wajibu wao kwa kuweka akiba kwa utaratibu na kurejesha mikopo kwa wakati kwani Saccos haiwezi kukua ikiwa hawataweka akiba na kutimiza masharti ya mikopo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Hazina SACCOS Limited,Dk  Festo Mwaipaja  amesema katika  kipindi cha Januari hadi Agosti 2016  wanachama imeongezeka  kwa kasi kwa kufikia 12,000  kutoka 10, 326 waliokuwepo mwishoni mwa mwaka 2025.

Amesema Hazina Saccos imefanikiwa kuongeza mali  zake kutoka takribani bilioni 49.4 mwaka 2025  kufikia  takribani Sh bilioni 63.75  mwezi Agosti mwaka huu (2026), na amana za wanachama zimeongezekakufikia bilioni 50 wakati bakaa ya mikopo imefikia  takribani sh bilioni 48.5 .

Dk Mwaipaja amesema kwa kipindi cha miezi minane cha mwaka huu mikopo  2,318 yenye thamani takribani Sh bilioni 22.8 ilitolewa na  wanawake waliongoza kuchukua mikopo ikiwa ni asilimia 55.4.

Urusi Yashambulia Ukraine kwa Drones, Watu Wawili Wauawa Sokoni

KYIV, Ukraine – Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drones) yanayodaiwa kufanywa na Urusi yamesababisha vifo vya watu wawili katika soko lililopo nje kidogo ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, huku watu wengine watatu wakiripotiwa kuuawa katika mashambulizi tofauti katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine, shambulio hilo lilitokea Jumapili, Septemba 27, 2026, katika eneo la Sofiiska Borshchahivka, upande wa magharibi wa Kyiv. Waendesha mashtaka walisema watu wawili waliuawa na takribani wengine 10 kujeruhiwa.

Picha zilizosambazwa baada ya tukio zilionyesha magari na maeneo mbalimbali ya soko yakiwa yamewaka moto, huku mabaki ya vitu vilivyoharibiwa yakionekana kutapakaa eneo la tukio.

Kyiv Yashambuliwa

Katika mji wa Kyiv wenyewe, Meya Vitali Klitschko alisema watu tisa walijeruhiwa, akiwemo mtoto mmoja. Watu sita kati ya waliojeruhiwa walikuwa wakipatiwa matibabu hospitalini.

Klitschko pia alisema drone iligonga jengo refu la makazi katika eneo la mashariki mwa jiji na kusababisha moto, huku mtu mmoja akijeruhiwa.

Baadaye, aliripoti kuwa drone nyingine iligonga jengo lingine refu katika eneo la katikati ya jiji, ambapo huduma za dharura zilifika kufanya tathmini ya hali na kubaini iwapo kulikuwa na majeruhi zaidi.

Maeneo yaliyo karibu na shule ya chekechea na uwanja wa michezo pia yaliripotiwa kushambuliwa.

Vifo Vyaripotiwa Sumy na Kharkiv

Katika mji wa Sumy, kaskazini mwa Ukraine, mabomu matatu ya aina ya glide bombs yaliripotiwa kulipuka karibu na kituo cha kusaidia familia, na kusababisha vifo vya watu wawili, kwa mujibu wa Gavana wa Mkoa wa Sumy, Oleh Hryhorov.

Nchini Kharkiv, mji mkubwa wa pili wa Ukraine uliopo kaskazini-mashariki, waendesha mashtaka walisema drone iligonga gari na kumuua dereva.

Mashambulizi hayo yamekuja katika kipindi ambacho Urusi imeongeza matumizi ya mashambulizi ya anga dhidi ya miji mbalimbali ya Ukraine. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, alisema Urusi ilirusha drones 277 za aina mbalimbali tangu Jumamosi, zikiwemo 155 za injini za ndege (jet-powered drones).

Zelenskiy amelaani mashambulizi hayo, akisema kulengwa kwa maeneo ya kiraia ni “ugaidi” na kwamba, kwa mtazamo wake, mashambulizi hayo hayana malengo ya kijeshi.

Miundombinu ya Mawasiliano Yalengwa

Mbali na maeneo ya makazi, miundombinu ya mawasiliano na vituo vya kuhifadhi data pia iliripotiwa kuathiriwa.

Kampuni kubwa zaidi ya huduma za simu nchini Ukraine iliiambia Interfax Ukraine kuwa makao yake makuu yaligongwa katika mashambulizi yanayoendelea dhidi ya vituo vya data na miundombinu ya mawasiliano. Hakuna vifo vilivyoripotiwa katika tukio hilo.

Kwa upande mwingine, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema vikosi vyake vilishambulia vituo viwili vya data jijini Kyiv, kituo cha usafirishaji bidhaa mjini Odesa pamoja na meli mbili za mizigo zilizokuwa zikielekea Odesa.

Mashambulizi hayo yanaendelea huku vita kati ya Urusi na Ukraine vikiingia katika kipindi kingine cha mapigano makali, huku miji na miundombinu ya kiraia ikiendelea kuwa miongoni mwa maeneo yanayoripotiwa kuathiriwa.

Abri achangia mabati Usolanga – HabariLeo

IRINGA: Ujenzi wa nyumba ya muhudumu wa afya katika Zahanati ya Usolanga, wilayani Iringa unatarajiwa kupiga hatua baada ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Arif Abri, kuchangia mabati 30.

Pamoja na msaada huo utakaosaidia kuimarisha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani, kada huyo wa CCM ametoa msaada wa kompyuta moja kwa matumizi ya Zahanati hiyo.

Diwani wa Kata ya Malengamakali, Stephano Mkisi, amesema nyumba hiyo ni sehemu muhimu ya jitihada za wananchi kuhakikisha wahudumu wa afya wanakuwa na mazingira bora ya kuishi karibu na kituo chao cha kazi.

“Mpango huu unalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma wakati wowote, hususan kwa wagonjwa wanaohitaji msaada wa haraka nje ya muda wa kawaida wa kazi,” amesema.

Amesema msaada huo wa Abri umeongeza nguvu katika ujenzi wa nyumba hiyo ambayo tayari ilikuwa imefikia hatua ya kuezekwa wakati wananchi walipowasilisha mahitaji yao kwa viongozi na wadau wa maendeleo.

Mkisi, amesema ujenzi wa nyumba hiyo ni miongoni mwa mahitaji muhimu yaliyotambuliwa na wananchi kwa lengo la kuboresha huduma katika zahanati hiyo.

Mabati hnpamoja na kompyuta hiyo yamekabidhiwa kwa niaba ya Abri na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Arnold Mvamba, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho.

Akizungumza katika mkutano huo, Mvamba amesema serikali ndiyo mdau mkuu wa maendeleo, lakini ushiriki wa wananchi, viongozi na wadau wengine ni muhimu katika kuharakisha utekelezaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi.

Mvamba amesema msaada huo unatokana na ahadi iliyotolewa na Abri wakati wa ziara yake Usolanga, ambapo wananchi walieleza changamoto zinazowakabili katika huduma za afya na uhitaji wa vifaa vya teknolojia.

Amesema msaada huo unaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, wananchi na wadau mbalimbali katika kutatua changamoto za huduma za kijamii.

Licha ya msaada huo kuwa hatua muhimu ya ujenzi huo amesema, bado ushirikiano wa wananchi unahitajika ili kukamilisha nyumba hiyo na kuhakikisha inatumika kwa lengo lililokusudiwa.

Aidha Mvamba amewataka wananchi kuendelea kuzingatia tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu mwenendo wa mvua na kuchukua hatua stahiki kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

BRELA yatoa wito usajili nembo za biashara – HabariLeo

GEITA: WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewaomba wafanyabiashara, wajasiriamali na wachimbaji wadogo kuzingatia usajili wa nembo ya biashara badala ya kuishia kusajili jina la biashara pekee.

Ofisa Usajili BRELA, Athumani Makuka ametoa wito huo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika badala la BRELA kwenye viwanja vya Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita.

Makuka amesema watanzania wanapaswa kutambua kuwa BRELA inatoa huduma nyingi na siyo usajili wa majina ya makampuni pekee ambapo huduma zote zinaambatana na usajili ili kutoa haki miliki.

Amesema usajili wa nembo ya biashara ni muhimu kwa kila mfanyabiashara ama mchimbaji mdogo mwenye taasisi ama kampuni ili kumsaidia kutumia nembo hiyo kama mbadala wa jina la kampuni.

Amesema hatua zote za usajili zinamsaidia mhusika kuwa na uhalali wa matumizi ya nembo ya biashara pasipo kikwazo na kuzuia nembo hiyo kutumika vibaya na watu wengine bila taarifa ya mwaasisi.

“Usajili una umuhimu katika kusaidia maendeleo ya mfanyabiashara kwani ukitaka Kwenda benki kuomba mkopo utalizwa kama tayari umesajili BRELA na hata ukiomba zabuni inahitaji usajili wa BRELA.

“Pia kuanzisha biashara bila usajili kuna hatari kubwa ya kuziwa kwa maana mtu anaweza akaja akasajili baadaye wewe ambaye ulianzisha kwa kutumia nguvu nyingi mwisho wa siku ukapokonywa jina la biashara”, amesema Makuka.

Amesema usajili wa makampuni katika mfumo wa BRELA inarahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi kitaifa juu ya kampuni au taasisi zinazojihusisha na sekta fulani ikiwemo sekta ya madini.

Wema Aandika Ujumbe wa Umama, Mashabiki Wamiminika Instagram

Global Publishers
September 28, 2026
0 views
0 Comments

Mwigizaji na mwanamitindo maarufu nchini Tanzania, Wema Sepetu, ameendelea kuwavutia mashabiki wake baada ya kushiriki ujumbe mfupi unaoonekana kuonyesha furaha yake katika hatua ya maisha ya kuwa mama.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Wema ameandika “I am Mother…❤️”, ujumbe ambao umeibua maelfu ya hisia kutoka kwa mashabiki na wafuasi wake.

Sehemu kubwa ya maoni ya mashabiki imeelekezwa katika kumpongeza Wema, huku baadhi yao wakimuita “Mama Ollie” na kumtakia maisha marefu pamoja na furaha katika hatua hiyo ya maisha.

Baadhi ya mashabiki pia wametumia fursa hiyo kumtakia heri katika siku yake ya kuzaliwa, huku wengine wakieleza namna wanavyofurahia kumuona akiwa katika nafasi ya umama.

Miongoni mwa maoni yaliyotolewa, shabiki mmoja ameandika, “Beautiful mother and son,” huku mwingine akisema, “Motherhood looks better on you.”

Wengine walimpongeza kwa malezi na kumtakia afya njema yeye pamoja na mtoto wake, huku wakitumia emoji za upendo, pongezi na furaha.

Kauli hiyo ya Wema imekuja wakati ambapo maisha yake binafsi, hususan hatua yake ya kuwa mama, yamekuwa yakifuatiliwa kwa karibu na mashabiki wake kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa ujumbe wake mfupi wa “I am Mother”, Wema ameonyesha namna anavyothamini nafasi hiyo, huku mashabiki wake wakimiminia pongezi na salamu za upendo.

Gofu yafungua milango ya ushirikiano wa biashara – HabariLeo

Mashindano hayo yalifanyika Septemba 26, 2026, katika viwanja vya Sea Cliff Golf Course, Zanzibar, yakishirikisha zaidi ya wachezaji 80 kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali ya Afrika, yakiwemo Kenya, Uganda, Zambia, Malawi, Afrika Kusini na Nigeria.

Wachezaji kutoka Kenya, Thomas Mwangi na Caroline Muigai, walitwaa ubingwa wa jumla kwa wanaume na wanawake mtawalia katika mashindano hayo yaliyochezwa kwa mfumo wa Stableford kwenye mashimo 18.

Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando akishiriki katika mashindano ya CEO Golf Tournament, iliyofanyika Septemba 26, 2026 katika viwanja vya Sea Cliff Golf Course visiwani Zanzibar.

Mashindano hayo yaliwakutanisha viongozi wa biashara, Maafisa Watendaji wakuu (CEOs), wanadiplomasia na wadau mbalimbali kutoka Tanzania na mataifa mengine ya Afrika, huku Vodacom Tanzania Plc ikiwa mdhamini mkuu wa shindano hilo lililolenga kuimarisha uhusiano, kujenga mitandao ya kibiashara na kukuza ushirikiano miongoni mwa viongozi wa sekta mbalimbali.

Mwangi alitwaa ubingwa wa jumla kwa wanaume baada ya kukusanya pointi 40, huku Muigai akiibuka mshindi kwa wanawake kwa kupata pointi 41.

Katika Division A, Patrick O’Rourke alishinda nafasi ya kwanza, huku Ernest Sengeu akimaliza nafasi ya pili kwa pointi 31.

Kwa upande wa Division B, Thagaran Govender alitwaa ushindi kwa pointi 39, akifuatiwa na Gregory Eayrs aliyepata pointi 38.

Mkuu wa Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Business wa kampuni ya Vodacom Tanzania PLC Joseph Sayi (kulia) akikabidhiwa zawadi na afisa masoko wa kampuni hiyo Chelsea Njau, baada ya kuibuka mshindi wa Pili wa Mashindano ya CEO Golf Tournament 2026.

Katika Division C, Abbas Simkoko aliibuka mshindi kwa pointi 40, huku Joseph Sayi akimaliza nafasi ya pili kwa pointi 37.

Kwa upande wa wanawake, Salome Gakere alishinda kwa pointi 36, huku Vicky Elias akimaliza nafasi ya pili kwa pointi 35, sawa na Maryanne Mugo, lakini akashinda kwa kutumia mfumo wa countback.

Akizungumza wakati wa mashindano hayo, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema kampuni hiyo inajivunia kuunga mkono mashindano yanayounganisha michezo na jumuiya ya wafanyabiashara.

“Tunafurahi kudhamini na kushiriki mashindano ya CEO Golf Tournament kwa sababu gofu si mchezo pekee, bali ni jukwaa linalowakutanisha watu, mawazo na fursa,” alisema Kamando.

Mkuu wa idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Business katika kampuni ya Vodacom Tanzania PLC Joseph Sayi (kulia) akimkabidhi zawadi mshindi wa pili wa divisheni A katika Mashindano ya CEO Golf Tournament 2026, Ernest Sengeu (kushoto). Mashindano hayo yaliwakutanisha viongozi wa biashara, Maafisa Watendaji wakuu (CEOs), wanadiplomasia na wadau mbalimbali kutoka Tanzania na mataifa mengine ya Afrika, huku Vodacom Tanzania Plc ikiwa mdhamini mkuu wa shindano hilo lililolenga kuimarisha uhusiano, kujenga mitandao ya kibiashara na kukuza ushirikiano miongoni mwa viongozi wa sekta mbalimbali.

Alisema mashindano hayo yanatoa mazingira rafiki kwa viongozi wa biashara kutoka sekta mbalimbali kukutana, kubadilishana mawazo na kujenga mahusiano ya kikazi yanayoweza kufungua fursa za ushirikiano.

Wafanyakazi wa Vodacom Tanzania PLC wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kuibuka na ushindi katika mashindano ya CEO Golf Tournament 2026, iliyofanyika Septemba 26, 2026 katika viwanja vya Sea Cliff Golf Course visiwani Zanzibar.

Kamando alisema pia mashindano hayo yana mchango katika kukuza utalii Zanzibar, akibainisha kuwa matukio ya kimataifa ya michezo yanaifanya Zanzibar kufahamika zaidi kwa wageni ambao wanaweza kurejea kwa shughuli za utalii na biashara.

“Tunajivunia kushiriki katika kuitangaza Zanzibar kama kituo cha biashara, utalii na michezo. Matukio kama haya yanaongeza thamani si kwa washiriki pekee, bali pia kwa uchumi kiujumla,” alisema.

Mkuu wa Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Business katika kampuni ya Vodacom Tanzania PLC Joseph Sayi akishiriki katika mashindano ya CEO Golf Tournament. Mashindano hayo yaliwakutanisha viongozi wa biashara, Maafisa Watendaji wakuu (CEOs), wanadiplomasia na wadau mbalimbali kutoka Tanzania na mataifa mengine ya Afrika, huku Vodacom Tanzania Plc ikiwa mdhamini mkuu wa shindano hilo lililolenga kuimarisha uhusiano, kujenga mitandao ya kibiashara na kukuza ushirikiano miongoni mwa viongozi wa sekta mbalimbali.

Alisema ushiriki wa Vodacom Tanzania katika majukwaa kama CEO Golf Tournament unaipa kampuni hiyo fursa ya kukutana na viongozi wanaofanya maamuzi katika sekta ya biashara, kusikiliza mahitaji yao na kujadili namna teknolojia inavyoweza kusaidia biashara kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Kupitia ushiriki huo, Vodacom Tanzania inaendelea kutumia majukwaa ya michezo kujenga mahusiano na viongozi wa makampuni, kuendeleza mazungumzo ya kibiashara na kuchochea fursa za ushirikiano katika mazingira ya biashara yanayozidi kutegemea teknolojia na huduma za kidijitali.

Serikali kuongeza wigo wa utafiti wa madini – HabariLeo

GEITA: SERIKALI imejizatiti kuimarisha utafiti wa kina wa jiofizikia kutoka takribani asilimia 16 ya sasa hadi angalau kufikia asilimia 50 ya eneo lote la nchi ifikapo mwaka 2030.

Mpango huo unalenga kuongeza mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa ambapo hadi mwaka 2025/26 mchango wa sekta ya madini umefikia asilimia 10 huku ikichangia asilimia 56 ya fedha za kigeni.

Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa, ametoa taarifa hiyo katika hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Dk Samia Suluhu mjini Geita.

Dk Kiruswa amesema utafiti wa kina wa jiofizikia utaongeza upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu miamba yenye viashiria vya madini na hivo wizara kuweza kupata maeneo mapya kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

“Hii itapunguza kwa kiasi kikubwa gharama ya utafutaji madini inayosababisha wachimbaji wadogo kupoteza mitaji yao”, amesema Dk Kiruswa.

Amesema mpango huo pia ni sehemu ya kutokomeza mila na desturi potofu kwa baadhi ya wachimbaji wadogo ambao awali walikuwa wanafungamanisha uchimbaji wa madini na imani za kishirikina.

“Madini ni sayansi, na sisi kama wizara tumekuja na visiona 2030, kuwaonyesha watanzania ni wapi madini yapo, ya namna gani, yenye ubora gani, kwa kiwango gani ili tukafanye uwekezaji wenye tija”, amesema Dk Kiruswa.

Amesema katika kufangamanisha sekta ya madini na sekta zingine wizara inaendelea kutekeleza Mining for a Better Tommorrow (MBT) ili kuhakikisha madini yananufaisha makundi yote katika kijamii.

Amesema programu hiyo inahusisha utoaji wa nyenzo, msaada wa kitaalamu, utoaji wa taarifa za utafiti, utoaji wa leseni, na fursa zingine za biashara na uwekezaji pamoja na uwendeshaji wa vifaa na mitambo.

Aidha amewahakikishia watanzania wizara inaendelea kufuatilia na kufanyia marekebisho sera na sheria za madini ikiwemo sheria ya hakimiliki aridhi dhidi ya hakimiliki madini ili kupunguza mgongano wa kimaslahi.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, amesema ili kuhakikisha madini yanakuwa si chanzo cha migogoro ipo haja kwa wizara ya madini kufanyia mapitio ya sheria ya hakimiliki aridhi na hakimiliki madini.

Mnyeti amesema mpaka sasa kumekuwa na migogoro mingi inayosababishwa na mgongano wa maslahi wa sheria hiyo ambapo hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kulinda maslahi ya watanzania.

Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Fredy Liundi amesema kwa mjibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mwaka 2025 mauzo ya madini yalikuwa sh Trillioni 11.7.

Liundi amesema mauzo hayo yanaonyesha usimamizi thabiti wa sekta ya madini chini ya serikali ya awamu ya sita ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo mauzo ya madini yalikuwa takribani Sh Trillioni 7.2.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amesema kuwa Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini mwaka 2026 yamehusisha washiriki 765 ikiwemo kampuni 15 za uchimbaji wa madini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), Ashraf Suryaningrat amepongeza serikali kwa maonyesho hayo na kuyataja kama jukwaa huru na ujuzi, biashara na mahusiano katika sekta ya madini.

Ajali ya Ndege DR Congo Yaua Watu 17, Serikali Yatangaza Maombolezo

KINSHASA, DR Congo – Watu 17 wamefariki dunia baada ya ndege aina ya LET 410 UVP kuanguka na kushika moto karibu na mji wa Kenge, makao makuu ya jimbo la Kwango nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ajali hiyo ilitokea Ijumaa mchana wakati ndege hiyo, iliyokuwa ikiendeshwa na kampuni ya TRACEP Congo Aviation, ikiwa katika safari kutoka Kikwit kuelekea Kinshasa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Uchukuzi, ndege hiyo ilipata hitilafu ya kiufundi na ndipo ikaelekezwa Kenge katika jaribio la kutua kwa dharura. Hata hivyo, mamlaka za eneo hilo zilisema hakukuwa na uwanja wa ndege unaofanya kazi ambao ungeweza kupokea ndege hiyo.

Ndege hiyo ilianguka katika eneo la makazi kabla ya kulipuka na kushika moto. Watu wote 17 waliokuwa ndani yake, wakiwemo abiria 13 na wahudumu wanne, walifariki dunia.

Miongoni mwa waliopoteza maisha ni maafisa wawili waandamizi wa mahakama ya kijeshi ya DRC, Luteni Jenerali Joseph Mutombo Katalayi Tiende, aliyekuwa Rais wa Mahakama Kuu ya Kijeshi, na Luteni Jenerali Lucien-René Likulia Bakumi, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Kijeshi wa FARDC.

Awali, taarifa za mamlaka zilitaja vifo vya watu 13, kabla ya idadi hiyo kufikia 17 baada ya shughuli za uokoaji kukamilika.

Serikali Yasitisha Shughuli za TRACEP

Baada ya ajali hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchukuzi, Jean-Pierre Bemba, aliamuru kusimamishwa mara moja kwa Cheti cha Uendeshaji wa Ndege (Air Operator Certificate) cha TRACEP Congo Aviation.

Hatua hiyo imesababisha kusitishwa kwa shughuli za shirika hilo nchini hadi uchunguzi wa ajali hiyo utakapokamilika.

Wachunguzi kutoka mamlaka ya uchunguzi wa ajali za anga nchini humo wamepelekwa katika eneo la tukio ili kubaini chanzo cha ajali na mazingira yaliyopelekea ndege hiyo kuanguka.

Wizara ya Mawasiliano pia imesema Waziri wa Sheria ameagiza uchunguzi wa kina kuhusu ajali hiyo ufanyike kwa mujibu wa sheria za nchi.

Tshisekedi Atuma Rambirambi

Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliofariki, huku Serikali ikieleza mshikamano wake na familia hizo, mfumo wa mahakama na wanajeshi walioathiriwa na msiba huo.

Kutokana na ukubwa wa janga hilo, Serikali ya DRC imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.

Rais Tshisekedi pia ameagiza bendera ya taifa kupeperushwa nusu mlingoti kuanzia Jumatatu, Septemba 28, hadi siku ya mazishi ya waathiriwa.

Serikali imewataka wananchi kuwa na utulivu, heshima na mshikamano na familia zilizopoteza wapendwa wao.

Aidha, mamlaka zimewaomba wananchi kuepuka kusambaza picha za waathiriwa au taarifa zinazoweza kudhalilisha heshima yao na kuongeza maumivu kwa familia zao.

DR Congo itaendelea na kipindi hicho cha maombolezo ya kitaifa huku uchunguzi wa chanzo cha ajali ukiendelea.