MAKATIBU WAKUU WAKAGUA AICC MAANDALIZI YA MWISHO MKUTANO WA IPU, ARUSHA

Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali pamoja na Kamati ya Wataalamu ya Maandalizi ya Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), wamefanya ukaguzi wa mwisho wa maandalizi ya mkutano huo leo Oktoba 02, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Ukaguzi huo uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Bi. Christine Mwakatobe ambapo

walikagua miundombinu muhimu ikiwemo ukumbi mkuu wa mikutano, kumbi za vikao vya pembeni, Ofisi za Viongozi, mifumo ya sauti na tafsiri, eneo la waandishi wa habari, pamoja na maeneo ya mapokezi ya wageni.

Baada ya ukaguzi huo, Makatibu Wakuu waliiagiza Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya mkutano huo kumalizia maandalizi ya baadhi ya sehemu ambazo zinafanyiwa marekebisho na maboresho ya mwisho kabla ya kuanza kwa mkutano huo Oktoba 04 hadi 09, 2026.

Mkutano huu unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki 2,000 kutoka Mabunge 183 wanachama wa IPU ambao ni Maspika, Wabunge, Makatibu na Maafisa mbalimbali.

Dunia inakuja Tanzania, Tuipe sababu ya kurudi tena.

 

Rais Mwinyi Kuzungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Zanzibar Kesho

Global Publishers
October 2, 2026
0 views
0 Comments

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari kesho, Oktoba 3, 2026, kuanzia saa 5:00 asubuhi katika Ikulu Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu Zanzibar leo, Oktoba 2, 2026, mkutano huo utarushwa mubashara kupitia vyombo mbalimbali vya habari, ikiwemo televisheni na mitandao ya kijamii, ili kuwawezesha wananchi kufuatilia moja kwa moja.

Taarifa hiyo imetolewa na Raqey Mohamed, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu.

VETA, BGC kushirikiana kukuza ujuzi – HabariLeo

GEITA; Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ipo katika mazungumzo na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Buckreef (BGC) ya Katoro, Geita, kwa lengo la kukuza ushirikiano utakaoandaa nguvu kazi mahiri kwa ajili ya sekta ya madini.
‎
‎Akizungumza katika kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa kampuni hiyo Oktoba 1, 2026, Meneja wa VETA Kanda ya Kaskazini, Monica Mbelle, amesema ushirikiano huo unatarajiwa kutoa fursa za mafunzo kwa vitendo kwa wakufunzi na wanafunzi wa VETA pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa kampuni hiyo.
‎
‎”Tumezungumza na uongozi wa Buckreef kuona namna tunavyoweza kushirikiana, ikiwemo kuleta wanafunzi wetu wanaosoma fani mbalimbali ili wapate mafunzo kazini, mafunzo haya yatasaidia kukomaza ujuzi wao katika stadi wanazojifunza,” amesema Mbelle.
‎
‎Ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia, VETA imeomba nafasi za mafunzo kwa wakufunzi wake ili waweze kupata ujuzi mpya na kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira.
‎
‎Aidha, Mbelle amesema VETA itashirikiana na Buckreef kuhakikisha wananchi wanaozunguka mgodi huo wanapata mafunzo ya ufundi stadi yatakayofadhiliwa na kampuni hiyo.


‎
‎”Buckreef wameona kuwa sisi VETA tunaweza kutoa ujuzi kwa vijana wa maeneo haya, na sisi tumeona jinsi tutakavyoandaa programu za kuwawezesha vijana wanaozunguka eneo la mgodi kupata ujuzi katika stadi mbalimbali,” amefafanua.
‎
‎Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa mgodi huo, Isaac Bisansaba, amewataka wananchi wanaozunguka mgodi huo kujiandaa kunufaika na fursa zitakazotokana na ushirikiano huo.

 


‎
‎”Tayari tumeanza mchakato wa kuwatambua vijana waliomaliza kidato cha sita, kidato cha nne au hata wale ambao hawakufaulu kwa viwango vya juu, ili tuwasaidie kujiunga na vyuo vya VETA kwa kulipia sehemu ya gharama za mafunzo yao na baadaye kuwapa nafasi za mafunzo kwa vitendo mgodini kwetu,” amesema Bisansaba.

MAWAKALA WA UTALII KUTOKA INDIA WAVUTIWA NA HIFADHI ZA NGORONGORO NA SERENGETI

Mawakala wa utalii kutoka Jamhuri ya India wameelezea kuridhishwa na kuvutiwa na uzuri  wa Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kufuatia ziara ya mafunzo (Fam Trip) iliyoandaliwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa kushirikina na Ubalozi wa Tanzania Nchini India

Ziara hiyo yenye lengo la kuitangaza Tanzania katika soko la kimataifa la utalii, imewajumuisha mawakala 13  kutoka majiji mbalimbali ya India.

Wakizungumza mara baada ya ziara katika hifadhi ya  Kreta ya Ngorongoro iliyotangazwa kama Ajabu ya Nane ya Dunia, walisema Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vya utalii vya kipekee duniani.

“Tumetembea nchi nyingi duniani, lakini kile tulichokiona hapa Ngorongoro ni cha tofauti sana. Muunganiko wa mandhari ya kuvutia, wingi wa wanyamapori katika eneo moja na uhifadhi uliotukuka ni jambo linaoonesha upekee wake, Hakika hii ni sehemu ambayo kila Mhindi anatakiwa kuja kuiona angalau mara moja maishani mwake,”

Kwa upande wa Serengeti, mawakala hao walipata fursa ya kushuhudia moja ya maajabu makubwa ya wanyamapori duniani, yakiwemo maelfu ya nyumbu na pundamilia katika harakati za uhamaji, pamoja na wanyama wakubwa watano (Big Five).

Mmoja wa mawakala hao  alisema Serengeti imezidi matarajio yao.

“Tulikuwa tumesikia mengi kuhusu Serengeti kwenye filamu, lakini kuiona kwa macho yetu wenyewe ni hisia tofauti kabisa. Ni mbuga kubwa, ya asili na iliyohifadhiwa vizuri. Tuliona simba, chui na tembo kwa ukaribu. Huduma za malazi na ukarimu wa Watanzania ni wa hali ya juu,” alieleza.

Naye Afisa Masoko wa TTB Bwana  Michael Ndaisaba alisema soko la India ni muhimu na linaendelea kukua kwa kasi, ambapo Ujio wa mawakala hao utachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya watalii kutoka Bara la Asia.

Ziara ya mawakala hao inatarajiwa kuhitimishwa jijini Zanzibar kwa kutembelea vivutio vya utalii wa fukwe na utamaduni.

 

Kituo kipya kuongeza huduma za meno – HabariLeo

DAR ES SALAAM: Huduma za afya ya kinywa nchini zinatarajiwa kuimarika baada ya Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam kuzindua kituo maalumu cha huduma za meno na vipandikizi vya meno, katika hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa.

Kituo hicho kimejengwa kwa uwekezaji wa Sh bilioni 1.3 na kina vyumba sita vya kisasa vyenye vifaa kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali za meno, ikiwemo huduma za vipandikizi.

Akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Emmanuel Tayari, amesema uwekezaji huo unaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya nchini.

Amesema sekta binafsi ina mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za afya, ambapo takribani asilimia 85 ya huduma za afya katika Mkoa wa Dar es Salaam hutolewa na sekta hiyo, huku katika huduma za afya ya kinywa ikifikia asilimia 70.

Tayari amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika huduma za afya ya kinywa kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kisasa, radiolojia ya meno kwa njia ya kidijitali pamoja na kuboresha miundombinu ya huduma hizo.

Amesema mkazo pia umewekwa katika kinga, utambuzi wa mapema na matibabu kwa wakati ili kupunguza hali ya wagonjwa kusubiri hadi kung’oa jino kuwa suluhisho pekee.

Aidha, amesema ushirikiano kati ya mifumo ya bima ya afya na hospitali binafsi unaendelea kuimarika, akitolea mfano Hospitali ya Aga Khan ambayo hivi karibuni ilisaini mkataba na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wa kuendelea kutoa huduma kwa wanachama wa mfuko huo.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan, Profesa Muzdalifat Abeid, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza huduma maalumu za afya zenye viwango vya juu, kwa lengo la kupunguza idadi ya Watanzania wanaosafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Utafiti wa Kitaifa wa Afya ya Kinywa wa mwaka 2020 ulionesha kuwa asilimia 76 ya Watanzania watu wazima waliathiriwa na tatizo la kuoza kwa meno, huku asilimia 52 wakiwa na ugonjwa wa fizi.

Aidha, hadi Julai 2025, ni asilimia 42 pekee ya vituo vya afya vya umma vilivyokuwa vikitoa huduma za afya ya kinywa, hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza uwekezaji na upatikanaji wa huduma hizo.

Uhakiki wabaini deni la Sh Bil 1.78 KNCU – HabariLeo

KILIMANJARO; Serikali ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuimarisha na kuinua vyama vya ushirika nchini, kwa lengo la kuhakikisha vinaendeshwa kwa uwazi, uadilifu na uwajibikaji na vinawanufaisha wananchi, hususan wakulima.

Kupitia usimamizi wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Taifa, Serikali imeendelea kutafuta suluhisho la changamoto zinazovikabili vyama vya ushirika, ikiwemo migogoro, madeni ya muda mrefu, uwajibikaji na uadilifu katika uendeshaji.

Hatua hiyo imeonekana katika Mkutano Mkuu Maalumu wa KNCU ulioitishwa kwa ajili ya kujadili matokeo ya uhakiki wa madeni kati ya KNCU na vyama wanachama, ambapo uhakiki huo uliofanywa na COASCO umebaini kuwa KNCU inadaiwa jumla ya Sh1,782,919,016.

Uhakiki huo umehusisha kipindi cha miaka 14 ya fedha hadi mwaka 2024/25, huku vyama 92 vya msingi vikiwa wanachama wa KNCU.

Kati ya hivyo, vyama 84 vilishiriki katika zoezi hilo, ambapo 64 vilibainika kuwa na madai dhidi ya KNCU, huku vyama vinne vikiwa na madeni kwa KNCU. Vyama vinane havikushiriki uhakiki huo.

Akizungumza kwenye mkutano huo jana, Mrajis wa Vyama vya Ushirika Taifa, Dk Benson Ndiege, amesema uhakiki huo umeweka wazi kiwango cha deni kinachoweza kuthibitishwa kwa nyaraka, lakini bado kuna haja ya kufanya uchunguzi wa kina, ili kubaini chanzo cha madeni na hasara zilizojitokeza katika kipindi cha nyuma.

Amesema Mkutano Mkuu Maalumu umeafiki kufanyika kwa uchunguzi wa kiforensiki (forensic investigation), ili kubaini chanzo cha madeni hayo, pamoja na iwapo kuna watendaji au viongozi waliowahi kuhusika.

“Tumekubaliana kufanya uchunguzi maalumu wa kina, ili kuangalia uhalisia wa jambo hili. Ingawa miaka mingi imepita, tutafikia kiini cha tatizo na wahusika watawajibishwa kwa mujibu wa nyaraka na sheria,” amesema Ndiege.

Amesema uchunguzi huo unalenga pia kubaini iwapo madeni hayo yalisababishwa na mdororo wa kiuchumi, hasara za biashara, au hatua na maamuzi ya watendaji na viongozi waliowahi kusimamia KNCU huko nyuma.

Kwa mujibu wa taarifa ya uhakiki, kati ya vyama 84 vilivyoshiriki, vyama 64 vilibainika kuwa na madai dhidi ya KNCU, huku vyama vinne vikibainika kuwa na madeni kwa KNCU. Pia, chama kimoja kilikuwa na madai ya takribani Sh 8 milioni.

Uhakiki huo ulifanyika kwa hatua mbalimbali, ikiwemo kufanya vikao na KNCU, kuchambua nyaraka, kulinganisha kumbukumbu za KNCU na zile za vyama wanachama, kupitia madai ya pande zote mbili na kufanya mahojiano na vyama husika.

Katika madai yaliyohusisha miradi ya pamoja, ripoti imebainisha kiasi cha takribani Sh24 milioni, sawa na takribani Sh 6 milioni kwa kila mradi wa pamoja.

Ndiege amesema changamoto kubwa katika kazi hiyo ilikuwa upatikanaji wa nyaraka za zamani. Baadhi ya nyaraka hazikuweza kupatikana, huku mabadiliko ya mara kwa mara ya watendaji yakisababisha baadhi ya kumbukumbu kupotea au kukosekana kwa watu wenye uelewa wa historia ya miamala hiyo.

Pia, baadhi ya nyaraka zilichelewa kuwasilishwa au hazikuwasilishwa kabisa na vyama husika.

Amesema tofauti zilizokuwepo kati ya kumbukumbu za KNCU na madai ya vyama wanachama ndizo zilizofanya zoezi la reconciliation kuwa muhimu katika kubaini deni linaloweza kuthibitishwa kwa nyaraka.

Kuhusu hatua zinazofuata, Ndiege amesema KNCU itaunda timu maalumu itakayopendekeza namna ya kulipa madeni yaliyothibitishwa, kisha mapendekezo hayo yatawasilishwa mbele ya wanachama kwa ajili ya kujadiliwa na kuafikiwa.

“Deni lipo na ni lazima lilipwe. Kinachotakiwa sasa ni kuweka utaratibu wa malipo na kuhakikisha unatekelezwa,” amesema.

Amesema serikali inaendelea kutumia ushirika kama nyenzo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, hivyo vyama vya ushirika vinapaswa kuendeshwa kwa misingi ya uadilifu, uwazi na uwajibikaji.

Aidha, amesema serikali inaendelea na taratibu za kuboresha vyama vya ushirika kupitia kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu”, inayolenga kutafuta majawabu ya changamoto zinazofanya vyama hivyo visifanye vizuri.

Kuhusu migogoro ya mali na mashamba, Ndiege amesema kati ya migogoro 19 iliyokuwepo, 16 imeshughulikiwa na mitatu imebaki ikiendelea kufanyiwa kazi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Moshi Vijijini, Enock Koola, amesema uhakiki huo ni hatua muhimu katika kuweka wazi ukweli kuhusu madeni yaliyodumu kwa muda mrefu kati ya KNCU na vyama vya msingi.

Amesema yeye pamoja na Mbunge Morris Makoi waliwasilisha hoja na kufanya mahojiano kuhusu madai ya wakulima na wanachama wa vyama vya ushirika ambao wamekuwa wakisubiri malipo yao kwa muda mrefu.

Koola amesema baada ya mahojiano hayo, Mrajis aliahidi kuunda kamati mbalimbali na kufanya uchunguzi wa kina ili kuhakikisha wakulima na wanachama wa vyama vya ushirika kutoka Moshi Vijijini na Vunjo wanapata haki yao.

Amesema uhakiki huo umewezesha kupata uelewa mpana kuhusu kiwango cha deni kinachoweza kuthibitishwa, huku akisisitiza kuwa mchakato huo haupaswi kuishia kwenye ripoti pekee.

Koola amesema anaunga mkono uamuzi wa kufanya uchunguzi wa kiforensiki, ili kubaini chanzo cha madeni na hasara zilizojitokeza, na iwapo uchunguzi utabaini ukiukwaji wa taratibu, hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

“Kwa upande wangu, nimejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba wakulima hawa wanapata haki yao. Tutaunga mkono mchakato huo na tutafuatilia hatua kwa hatua ili kuhakikisha haki inatendeka,” amesema.

Amesema iwapo uchunguzi utabaini kuwa kuna viongozi au watendaji wa KNCU ambao hawakutenda kwa uadilifu na kusababisha hasara, vyombo husika vinapaswa kuwabaini na kuwawajibisha kwa mujibu wa sheria.

“Fedha zilizopotea zinapaswa kurejeshwa na waliohusika wawajibishwe. Hata hivyo, jambo la msingi zaidi kwa sasa ni kuhakikisha wakulima wa Vunjo na Moshi Vijijini wanapata haki yao,” amesema.

Koola amesema wabunge wataendelea kufuatilia suala hilo bungeni na kwa waziri mwenye dhamana, ili kuhakikisha hatua zilizokubaliwa zinatekelezwa na madeni yaliyothibitishwa yanafanyiwa utaratibu wa malipo.

Naye Mbunge wa Moshi Vijijini, Morris Makoi, amesema mkutano huo ulikuwa muhimu kwa sababu umeweka wazi madai ya vyama vya msingi na kutoa msingi wa kuendelea kutafuta suluhisho la changamoto hiyo.

Amesema wakulima wamekuwa wakisubiri malipo yao kwa muda mrefu na kwamba kuchelewa kwa malipo hayo kunaathiri maisha yao pamoja na uzalishaji wa kahawa.

Ameiomba serikali na uongozi wa KNCU kuhakikisha mpango wa kulipa madeni yaliyothibitishwa unaandaliwa na kutekelezwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Amesema hatua iliyofuata inapaswa kuwa kuhakikisha matokeo ya uhakiki na uchunguzi yanafanyiwa kazi, huku wakulima wakiendelea kupewa taarifa kuhusu hatua zinazochukuliwa.

 

Mloganzila yalaza wagonjwa watano wa kiharusi kila siku – HabariLeo

DAR ES SALAAM: Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila hulaza wagonjwa kati ya watano na saba wenye kiharusi kila siku, hali inayodhihirisha ukubwa wa tatizo hilo na umuhimu wa jamii kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo.

Daktari Bingwa Bobezi wa Magonjwa ya Ubongo na Mishipa ya Fahamu kutoka hospitalini hapo, Dk Brighton Mushengezi, amesema kiharusi kinaendelea kuwa changamoto kubwa ya kiafya duniani na hutokea pale mzunguko wa damu kwenda kwenye ubongo unapozuiwa au mshipa wa damu katika ubongo unapopasuka.

Amesema hali hiyo husababisha sehemu ya ubongo kukosa oksijeni na virutubisho vinavyohitajika, jambo linaloweza kusababisha madhara makubwa kwa mgonjwa endapo hatapatiwa huduma kwa wakati.

Kwa mujibu wa Dk Mushengezi, dalili za kiharusi zinaweza kujitokeza ghafla na ni pamoja na uso kupinda upande mmoja, mkono au mguu kuwa dhaifu au kufa ganzi, kushindwa kuzungumza au kuelewa mazungumzo, kupoteza uwezo wa kuona pamoja na kushindwa kutembea vizuri.

Amesema takwimu za Shirika la Kiharusi Duniani (World Stroke Organization) za mwaka 2025 zinaonesha kuwa takribani watu milioni 12 hupata kiharusi kila mwaka duniani.

Ameongeza kuwa shirika hilo linaeleza pia kuwa mtu mmoja kati ya watu wanne wenye umri wa miaka 25 na kuendelea yuko katika hatari ya kupata kiharusi katika maisha yake, hali inayosisitiza umuhimu wa jamii kuwa na uelewa wa ugonjwa huo na kuchukua hatua za kinga.

Dk Mushengezi ametaja shinikizo la damu kuwa miongoni mwa vihatarishi vikubwa vya kiharusi, huku kisukari, matumizi ya tumbaku, kutofanya mazoezi, ulaji usiofaa na matumizi hatarishi ya pombe pia vikiongeza uwezekano wa kupata ugonjwa huo.

Amesema baadhi ya vihatarishi hivyo vinaweza kudhibitiwa kwa kubadili mtindo wa maisha, ikiwamo kufanya mazoezi, kula mlo unaofaa, kudhibiti shinikizo la damu na kisukari pamoja na kuepuka matumizi ya tumbaku na pombe kwa kiwango hatarishi.

Aidha, amewataka wananchi kutopuuza dalili za kiharusi zinapojitokeza, bali kuwahi kumfikisha mgonjwa hospitalini kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.

Amesema utambuzi na matibabu ya mapema ni muhimu katika kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na kiharusi, huku elimu kwa jamii kuhusu dalili, vihatarishi na hatua za kuchukua ikiwa muhimu katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Putin Aonya NATO Kuhusu Kaliningrad, Kutumia Silaha Zote Ikishambuliwa

Moscow, Urusi — Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema nchi yake iko tayari kutumia silaha zote ilizonazo, ikiwemo silaha za nyuklia, endapo eneo la Urusi litashambuliwa na nchi wanachama wa NATO.

Putin alitoa kauli hiyo Alhamisi katika mkutano wa Valdai Club, akisisitiza kwamba Moscow haina mpango wa kushambulia nchi za Ulaya, lakini itajibu mashambulizi dhidi ya eneo lake.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Urusi kuonya NATO kuhusu uwezekano wa kutumia silaha za nyuklia iwapo nchi za muungano huo zingejaribu kuzuia au kuitenga Kaliningrad, eneo la Urusi lililopo kati ya Poland na Lithuania.

“Hakupaswi kuwa na makosa — Urusi iko tayari kutumia silaha zake zote, ikiwemo za nyuklia, kulinda eneo lake,” ubalozi wa Urusi nchini Ireland ulisema katika taarifa yake Jumanne.

Putin alisema iwapo kutatokea shambulio la moja kwa moja dhidi ya Shirikisho la Urusi, suala la kutumia silaha zote zilizo katika himaya ya nchi hiyo litakuwa mezani.

Hata hivyo, Putin hakutaja moja kwa moja kwamba Urusi itatumia silaha za nyuklia, akisema Moscow ina aina za silaha ambazo, kwa mujibu wake, hakuna nchi nyingine yenye uwezo kama huo.

NATO Yakataa Tishio Hilo

NATO imejibu kwa kukataa madai kwamba muungano huo unapanga kuishambulia au kuitenga Kaliningrad.

Msemaji wa NATO Allison Hart alisema Jumatano kwamba muungano huo umepokea ujumbe wa maandishi kutoka Urusi na kwamba NATO “inapinga vikali vitisho vya kutumia nguvu, ikiwemo kauli zisizowajibika kuhusu silaha za nyuklia.”

NATO imesisitiza kuwa ni muungano wa kujilinda na kwamba mazoezi yake ya kijeshi hayalengi kuweka tishio kwa eneo lolote la Urusi.

Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte pia amesema majibu ya muungano huo kwa ujumbe wa Urusi yalikuwa mafupi, huku akitoa wito kwa Moscow kuacha vitisho vya nyuklia.

Kaliningrad Yawa Kiini cha Mvutano

Kaliningrad ni eneo muhimu kimkakati kwa Urusi kutokana na nafasi yake kati ya Poland na Lithuania, ambazo zote ni wanachama wa NATO.

Eneo hilo lina kambi kuu ya wanamaji wa Urusi katika Bahari ya Baltic pamoja na mifumo mbalimbali ya kijeshi, ikiwemo makombora ya Iskander yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia.

Wakati huohuo, wanachama wa NATO wameongeza shughuli za kijeshi katika eneo la Bahari ya Baltic, huku mazoezi mengine yakitarajiwa kufanyika mwezi Oktoba.

Mvutano huo unakuja wakati vita kati ya Urusi na Ukraine vikiingia mwaka wake wa tano, huku viongozi wa Ulaya na mashirika ya ujasusi wakionya kuhusu uwezekano wa Urusi kuwa na uwezo wa kutishia nchi nyingine za Ulaya katika miaka ijayo.

Putin na viongozi wa Urusi wameendelea kuyapinga madai hayo, wakiyataja kuwa ni sehemu ya kampeni ya kuongeza hofu kuhusu Moscow.

Kwa sasa, kauli za pande zote zinaonyesha kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi na kidiplomasia katika eneo la Baltic, lakini hazimaanishi kwamba NATO na Urusi tayari zimeingia katika vita vya moja kwa moja.

WANAFUNZI WAFURIKA BANDA LA WAKALA WA VIPIMO MAONESHO YA MADINI GEITA

GEITA_ 

Banda la Wakala wa Vipimo (WMA) limekuwa kivutio kikubwa kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Mkoani Geita, baada ya mamia ya wanafunzi kuendeleq kufurika kujifunza elimu ya matumizi sahihi ya vipimo.

Wanafunzi hao kutoka shule mbalimbali za Geita wameonesha shauku kubwa ya kutaka kufahamu jinsi vipimo vinavyolinda haki zao kama walaji, hususan katika ununuzi wa bidhaa za kila siku kama vile gesi ya kupikia, mafuta na hata mizani inayotumika masokoni na madukani.

Akizungumza na wanafunzi hao, Meneja wa WMA Mkoa wa Mara Bw. Balisco Kapesa, ambaye ni mmoja wa Watumishi wa WMA walioko katika maonesho hayo,  aliwasisitiza wanafunzi kuwa na utamaduni wa kuhoji na kujiridhisha kama kifaa cha kupimia kimehakikiwa na WMA kabla ya kununua bidhaa yoyote, huku akiwaonesha kwa vitendo jinsi ya kutambua stika halali ya WMA kwenye mizani.

Kwa upande wake, Mwalimu wa wanafunzi kutoka Shule ya Msingi Zanzui ambayo ni moja ya shule zilizotembelea banda la WMA hao, Mwl. Sofia Kayongo alisema elimu hiyo ya vipimo ni ya vitendo na inapaswa kuingizwa kwenye mitaala ya shule, kwani inamjengea mwanafunzi uwezo wa kuwa mjasiriamali mwadilifu na mlaji makini, badala ya kusoma nadharia tu darasani.

Mmoja wa wanafunzi, Blasius Enosy, alisema elimu aliyoipata ni muhimu sana kwake na kwa familia yake, kwani sasa amejua kuwa kama mtungi wa gesi haujapimwa kwenye mzani uliohakikiwa na WMA, basi haupaswi kununuliwa, kwa kaulimbiu isemayo “Kama Gesi Haijapimwa kwenye mzani uliohakikiwa na WMA, Siitaki!”

Kwa ujumla, Maonesho ya Madini Geita 2026 yamekuwa fursa muhimu kwa WMA kutoa elimu kwa makundi mbalimbali, huku kaulimbiu ya Wakala isemayo “Kipimo Sahihi ni Haki Yako” ikiendelea kusikika kwa wananchi wengi wanaotembelea banda hilo.

WMA inaendelea na utaratibu wa kufikisha elimu ya vipimo kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi ambapo inatekeleza Mpango wa kuanzisha na kuendesha Klabu za Vipimo mashuleni.

WMA YATOA ELIMU YA VIPIMO KWA MAAFISA NA ASKARI WA JKT

 Dodoma_ 

Wakala wa Vipimo (WMA) jana Oktoba 1, 2026 ilifanya ziara ya kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliyopo eneo la Buigiri, Chamwino jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoa elimu hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka WMA, Bw. Francis Olwero, alisema amefurahishwa na mwitikio mkubwa na shauku waliyoionesha askari na maafisa wa JKT.

“Askari ni sehemu ya jamii, maisha yao kama yalivyo ya wananchi wengine yamezungukwa na vipimo kuanzia asubuhi hadi jioni. Ndio maana WMA iliona ni busara kuwaelimisha,” alisema Olwero.

Alisema katika elimu hiyo, WMA imewasisitiza askari kuhoji na kujiridhisha kama vipimo vinavyotumika katika biashara mbalimbali wanazonunua vimehakikiwa na WMA, ikiwemo gesi ya kupikia, maji, umeme, mizani za madukani na sokoni na hata pampu za mafuta.

Kwa upande wake, Private Fatma Mohamed alisema elimu hiyo imemfungua macho kama mwananchi kujua haki yake.

“Mimi  binafsi nimevutiwa na elimu hii, kama mwananchi nina haki ya kuhoji na kujiridhisha kama mizani ya buchani na hata pampu ya mafuta ya Sheli imehakikiwa na WMA kabla sijanunua bidhaa. Watanzania wenzangu hakikisheni mnafuatilia elimu inayotolewa na WMA ili kujua haki zenu kuhusu vipimo ili msipunjwe,” alisema Private Fatma.

Naye Luteni Isaka Zacharia alisema ujio wa WMA umekuwa fursa muhimu kwa JKT.

“Tumejua kuwa tunapaswa kujiridhisha kuhusu matumizi ya vipimo sahihi kwenye huduma zinazogusa maisha yetu ya kila siku ikiwemo dira za maji na hata mita za umeme. Natoa rai kwa WMA kuendelea kutoa elimu ya vipimo kwa makundi mbalimbali katika jamii hususan wananchi wa kawaida na walioko vijijini,” alisema Luteni Zacharia.

Private Michael Mdegela alisema elimu aliyoipata itamsaidia kuachana na mazoea ya kununua bidhaa bila kupima.

“Tumejifunza na tunaenda kuthibitisha hilo, maana kuanzia sasa tutaanza kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo na tutahoji kujiridhisha kama bidhaa tunazonunua zimepimwa kwa usahihi, hususan gesi ya kupikia. Kama gesi haijapimwa kwenye mzani uliohakikiwa na WMA, Siitaki!” alisisitiza.

Akifafanua kuhusu mkakati wa WMA, Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma kutoka WMA, Bi. Veronica Simba, amesema WMA inaendelea na zoezi la utoaji elimu ya vipimo kwa makundi mbalimbali katika jamii kwa kutumia mbinu mbalimbali za mawasiliano.

“Lengo letu ni kuhakikisha elimu ya matumizi sahihi ya vipimo inafika kwa kila mtu nchini, kwa kaulimbiu yetu isemayo, _Kipimo Sahihi ni Haki Yako_ alisema Bi. Simba.