Wizara ya Elimu Yabadili Tarehe ya Kufunga Shule, Sasa ni Novemba 13

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeagiza shule zote za msingi na sekondari Tanzania Bara kufungwa Novemba 13,  2026, badala ya Desemba 4, 2026 kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Uamuzi huo umetangazwa kupitia Waraka wa Elimu Na. 3 wa Mwaka 2026 kuhusu mabadiliko ya tarehe ya kufunga shule za awali, msingi na sekondari Tanzania Bara, uliotolewa na Wizara hiyo tarehe 30 Septemba 2026.

Kwa mujibu wa waraka huo, hatua hiyo imechukuliwa kufuatia taarifa za hali ya hewa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mvua kubwa zinazohusishwa na El Niño katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026.

Wizara imeeleza kuwa mvua hizo zinaweza kusababisha mafuriko na athari nyingine katika baadhi ya maeneo, hivyo hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama na ustawi wa wanafunzi, walimu pamoja na watumishi wengine wa shule.

Awali, kupitia Waraka wa Elimu Na. 6 wa Mwaka 2025 kuhusu kalenda ya mihula ya masomo kwa mwaka 2026 na Waraka wa Elimu Na. 1 wa Mwaka 2026 kuhusu kalenda ya mihula kwa Kidato cha Tano na Sita kwa mwaka wa masomo 2026/2027, shule zilipangwa kufungwa tarehe 4 Desemba 2026.

Hata hivyo, Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene M. Mtahabwa, ametangaza kuwa shule zote zifungwe tarehe 13 Novemba 2026, ikiwa ni hatua ya tahadhari kutokana na utabiri wa hali ya hewa.

Waraka huo umeelekeza kuwa uamuzi huo unaanza kutumika rasmi kuanzia Oktoba 1, 2026.

Wizara imetoa waraka huo kwa wadau mbalimbali wa elimu, wakiwemo TAMONGSCO, Christian Social Services Commission (CSSC), BAKWATA, Tanzania Association of Private Investors in Education (TAPIE), Baraza la Sunnar Tanzania (BASUTA), TEN/MET, TAWOSCO pamoja na Umoja wa Wazazi wa CCM.

PROF. EZEKIEL: TEKNOLOJIA YA HABARI NI NYENZO MUHIMU KUKUZA UCHUMI WA VIJANA , 32 WAHITIMU MAFUNZO YA KIDIGITALI AWAMU YA PILI DIT

  Na Mwandishi Wetu.

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imehitimisha awamu ya pili ya mafunzo ya mradi wa majaribio unaolenga kuwawezesha vijana kutumia teknolojia ya kidigitali katika kujitangaza, kujiajiri na kuongeza fursa za ajira, huku vijana 32 waliokuwa wakishiriki mafunzo hayo wakihitimu.

Hafla ya kufunga mafunzo hayo imefanyika leo, Oktoba 02, 2026, katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia za kuwawezesha vijana kutumia ujuzi wa kidigitali katika kujiletea maendeleo na kuchangamkia fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa kidigitali.

Mafunzo hayo ya majaribio yamewalenga vijana kuwawezesha kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha ufanisi wa shughuli wanazofanya, ikiwemo shughuli za kibiashara, utengenezaji wa maudhui mtandaoni pamoja na kujitangaza kitaalamu kupitia majukwaa ya kidigitali.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Prof. Ezekiel Amri, amesema teknolojia ya habari ni moja ya nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa mtu binafsi, hususan vijana, pamoja na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Prof. Amri amewapongeza vijana hao kwa kukamilisha mafunzo hayo, akibainisha kuwa wote 32 walioanza mafunzo wameweza kuyamaliza, bila mshiriki hata mmoja kuacha njiani.

“Katika Dunia ya leo, suala la Teknolojia ya Habari ni mojawapo ya mambo yanayosaidia sana kukuza uchumi, kwa mtu binafsi hasa vijana kupitia shughuli mnazozifanya na pia uchumi wa Taifa. Napenda kuwapongeza sana, mmeanza mafunzo haya mkiwa 32 na mmeyamaliza mkiwa hao hao 32, hakuna aliyeishia njiani,” amesema Prof. Amri.

Aidha, Prof. Amri amewakaribisha vijana hao kuendelea kutumia fursa zinazopatikana DIT kwa ajili ya kuendeleza ujuzi walioupata, akieleza kuwa taasisi hiyo imejipambanua kwa kuwa na wataalamu waliobobea katika masuala ya teknolojia.

Amesema DIT ina wataalamu pamoja na vifaa vinavyoweza kuwawezesha vijana kupata mafunzo mbalimbali ya kiteknolojia, hivyo kuwataka wahitimu hao kutumia mafunzo waliyopata kama hatua ya kuendelea kujifunza kupitia kozi fupi zitakazotolewa na Kitengo cha ITCOEICT.

“Mafunzo haya yawafanye mfikirie kupata mafunzo zaidi ya kozi fupi mbalimbali zitakazotangazwa hapa na Kitengo chetu cha ITCOEICT. Hongereni sana na karibu sana DIT,” amesema Prof. Amri.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mafunzo, Kituo cha Umahiri wa TEHAMA – DIT, Bw. Othman Mfinanga, amesema mafunzo hayo yamekuja kutoa majibu kwa changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili vijana katika kutumia teknolojia ya kidigitali kwenye shughuli zao.

Bw. Mfinanga amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa majaribio ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeuanzisha kwa kutambua umuhimu wa kuwawezesha vijana kutumia ujuzi wa kidigitali katika kuboresha shughuli zao.

Amesema kupitia mafunzo hayo, vijana wamepata nafasi ya kujifunza namna teknolojia inavyoweza kutumika katika kuongeza ufanisi wa shughuli mbalimbali, ikiwemo biashara na utengenezaji wa maudhui mtandaoni.

“Haya mafunzo ni mafunzo ya majaribio ambayo Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeona kwamba kuna haja ya kuwawezesha vijana katika shughuli zao ili waweze kutumia ujuzi wa kidigitali katika kuboresha ufanisi wa shughuli wanazozifanya, kama ni shughuli za kibiashara, utengenezaji wa maudhui mtandaoni na kadhalika,” amesema Bw. Mfinanga.

Naye mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Fredy Mwita, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Bahari, ameishukuru Serikali kwa kutoa fursa hiyo kwa vijana na kusema mafunzo hayo yatamsaidia kutumia maarifa aliyoyapata kwa namna yenye manufaa.

Fredy amesema anatarajia kutumia ujuzi huo katika shughuli zake na kuhakikisha maarifa aliyoyapata yanakuwa sehemu ya mchango wake chanya kwa maendeleo ya nchi.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa fursa muhimu kwa vijana kupata ujuzi unaoweza kuwasaidia katika mazingira ya sasa ambayo teknolojia ya kidigitali imekuwa sehemu muhimu ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa majaribio unaolenga kuwajengea vijana uwezo wa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano katika kuboresha shughuli zao, kujitangaza, kuongeza ufanisi, kukuza biashara na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia uchumi wa kidigitali.

IKUMBUKWE,  hii ni awamu ya pili ya mafunzo hayo kwa upande wa DIT. Awamu ya kwanza ilihitimishwa wiki iliyopita, ambapo vijana 48 walihitimu mafunzo hayo na kukabidhiwa vyeti vya utambuzi wa ushiriki wao. Leo, Oktoba 02, 2026, vijana wengine 32 wamehitimisha awamu ya pili, hivyo kuendelea kwa DIT katika kuwajengea vijana uwezo wa kutumia teknolojia ya kidigitali kama nyenzo ya kujiajiri, kujitangaza na kuongeza fursa za ajira.


TANZANIA YATANGAZA UTALII WA MADINI QATAR

*Dkt. Kiruswa asisitiza ushirikiano wa Tanzania na Qatar katika kukuza utalii wa madini*

**Doha, Qatar*

Tanzania imetangaza fursa na vivutio vya utalii wa madini nchini Qatar, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza sekta hiyo, kuongeza idadi ya watalii na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ameongoza ujumbe wa Tanzania nchini Qatar, ambapo amefanya mazungumzo na viongozi na wadau wa sekta ya utalii nchini humo kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar katika kukuza utalii, hususan utalii unaohusisha vivutio vya madini.

Akizungumza baada ya kutembelea na kufanya mazungumzo na uongozi wa utalii nchini Qatar, Dkt. Kiruswa amesema Tanzania ina fursa kubwa katika sekta ya utalii kutokana na kuwa na vivutio mbalimbali, ikiwemo utalii wa madini, mbuga za wanyama, bahari na fukwe pamoja na vivutio vilivyopo Zanzibar.

Amesema Serikali ya Tanzania ipo tayari kushirikiana na Qatar katika kuendeleza, kutangaza na kuvutia watalii katika vivutio vilivyopo nchini, hatua ambayo itasaidia kuongeza mapato, ajira na manufaa ya kiuchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, ikiwemo utalii wa madini, wanyamapori, bahari na Zanzibar. Tunataka kutumia fursa hii kuimarisha ushirikiano na Qatar ili kutangaza vivutio vyetu na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania,” amesema Dkt. Kiruswa.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Habibu Mohamed, ameupongeza uongozi wa utalii wa Qatar kwa kukubali kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika nchi hizo.

Amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza uelewa kuhusu fursa za utalii zilizopo Tanzania na Qatar, sambamba na kuongeza idadi ya watalii na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi baina ya nchi hizo.

Naye, Mwenyekiti wa Utalii nchini Qatar, Saad Bin Ali AlKharji  ameipongeza Tanzania kwa kuonesha nia ya kushirikiana na Qatar katika kukuza utalii wa madini na sekta nyingine za utalii.

Ameahidi kutoa ushirikiano kwa Tanzania katika kuhakikisha vivutio vya utalii, ikiwemo utalii wa madini, vinatangazwa kwa kiwango kikubwa nchini Qatar ili kuvutia watalii zaidi kutembelea Tanzania.

Ushirikiano huo unatarajiwa kufungua fursa zaidi za kutangaza utalii wa madini wa Tanzania katika masoko ya kimataifa, pamoja na kuchochea uwekezaji na shughuli nyingine za kiuchumi zinazohusiana na sekta ya utalii.

Kadogosa ataka ushirikiano kuimarisha ujenzi – HabariLeo

DODOMA: WAZIRI wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, amesema atashirikiana kwa karibu na viongozi na watumishi wa wizara hiyo kuhakikisha miradi inayotekelezwa katika Sekta ya Ujenzi inatekelezwa kwa weledi na ufanisi, kwa lengo la kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali katika kuendeleza miundombinu nchini.

Kadogosa ameyasema hayo leo, Oktoba 2, 2026, katika Ofisi za Wizara ya Ujenzi, Mtumba jijini Dodoma, mara baada ya kuwasili na kukabidhiwa rasmi Ofisi na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kufuatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Septemba 27, 2026.

Amesema yupo tayari kujifunza, kupokea maoni na ushauri kutoka kwa viongozi, watumishi na wadau mbalimbali kuhusu namna bora ya kuendeleza na kukuza Sekta ya Ujenzi nchini, akisisitiza kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya taifa.

“Niwaeleze kuwa Ofisi yangu ipo wazi kwa yeyote mwenye maoni na ushauri wa kuboresha Sekta yetu. Mlango upo wazi, tushirikiane kwa pamoja kuinua Sekta hii,” amesema Kadogosa.

Aidha, Kadogosa amepongeza namna wizara, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ilivyojipanga kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua zinazotarajiwa kunyesha nchini.

Amesisitiza umuhimu wa wakala huo kuendelea kuchukua tahadhari na hatua stahiki za kuimarisha usalama na uendelevu wa miundombinu ya barabara na madaraja, hususan katika kipindi cha mvua.

Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na sasa Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Ulega, amewataka watumishi wa Wizara ya Ujenzi kumpa ushirikiano wa kutosha Waziri mpya ili wizara hiyo iendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kusonga mbele katika ujenzi wa taifa.

Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, Katibu Mkuu, Balozi, Mhandisi Aisha Amour, Naibu Katibu Mkuu, Dk. Charles Msonde, Menejimenti ya Wizara, Wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara pamoja na baadhi ya watumishi wa Wizara.

WAZIRI MKUU: SERIKALI YAENDELEA KUWEKA MAZINGIRA BORA KWA WATANZANIA KUJILETEA MAENDELEO

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuwawezesha Watanzania kujiletea maendeleo, ikiwemo kurekebisha sheria mbalimbali zinazowakwaza katika kutekeleza shughuli zao.

Ameyasema hayo leo, Ijumaa, Oktoba 2, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mwibara, eneo la Kibara, mkoani Mara.

Amesema baadhi ya mambo yamefanyika ndani ya siku 100 kama alivyoahidi Rais, huku mengine yakiendelea kuchukuliwa hatua.

“Leo tunavyoongea, tumerekebisha sheria mbalimbali ili tuweze kuhakikisha kuwa Watanzania hawakwazwi na baadhi ya sheria katika kutekeleza wajibu wao,” amesema.

Amesema miongoni mwa hatua hizo ni kuwapa wafanyabiashara wapya muda wa kuimarisha biashara zao, ambapo kodi ya mapato kwa biashara mpya inaanza baada ya mwaka mmoja tangu kupata TIN kwa ajili ya kuanza biashara.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekemea tabia ya baadhi ya watumishi kuwachangisha wananchi fedha kwa ajili ya mafuta ya magari ya wagonjwa (ambulance), akisema vitendo hivyo havikubaliki.

“Hatuwezi tukawa na magari ya Serikali yana mafuta, halafu ambulance ya kunusuru maisha ya wagonjwa tuchangishane mafuta. Haya ni mazoea mabaya ambayo hatutaki kuwa utaratibu wa Serikali. Wa aina hiyo akipatikana, tunachukua hatua kali,” amesema.

Aidha, amekemea tabia ya kuficha dawa zilizotolewa na Serikali huku wagonjwa wakielekezwa kununua dawa nje ya vituo vya afya, na kuwaagiza viongozi wa afya kufuatilia hali hiyo hatua kwa hatua ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazostahili.

Katika sekta ya nishati, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kusogeza huduma ya umeme kwenye vitongoji, mitaa na maeneo mapya ya makazi, akisisitiza kuwa wananchi katika maeneo hayo wanapaswa kunufaika na huduma hiyo.

Kuhusu mvua, amewataka viongozi na mamlaka zinazohusika kujiandaa kukabiliana na uwezekano wa mvua kubwa, ikiwemo kusafisha mifereji na maeneo ya kupitisha maji ili kupunguza athari za mafuriko.

Aidha, amewataka wananchi kutotumia nguvu au kuchukua sheria mkononi katika kushughulikia migogoro ya ardhi na mifugo, akisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kutatua changamoto za maeneo ya malisho na upatikanaji wa maji kwa mifugo.

Waziri Mkuu pia amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani ya nchi na mali za umma, akisisitiza kuwa shule, barabara na vituo vya afya ni mali za wananchi na uharibifu wake unawaathiri wao wenyewe.

𝙈𝘼𝙆𝘼𝙈𝙐 𝙒𝘼 𝙍𝘼𝙄𝙎 𝘼𝙎𝙃𝙐𝙃𝙐𝘿𝙄𝘼 𝙐𝙏𝙄𝘼𝙅𝙄 𝙎𝘼𝙄𝙉𝙄, 𝙈𝙋𝘼𝙉𝙂𝙊 𝙒𝘼 𝙐𝙎𝙃𝙄𝙍𝙄𝙆𝙄𝘼𝙉𝙊 𝙒𝘼 𝙏𝘼𝙉𝙀𝙎𝘾𝙊 𝙉𝘼 𝘾𝙍𝘿𝘽 𝙆𝙐𝙒𝘼𝙒𝙀𝙕𝙀𝙎𝙃𝘼 𝙒𝘼𝙉𝘼𝙉𝘾𝙃𝙄 𝙆𝙐𝙋𝘼𝙏𝘼 𝙐𝙈𝙀𝙈𝙀.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa wito kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na wadau husika wa sekta binafsi kuandaa mpango utakaowawezesha wananchi kununua umeme kwa mkopo kama ilivyo mikopo katika mitandao ya simu ili kuwasaidia wananchi wanapokuwa na uhitaji wa umeme lakini hawana fedha.
 
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa hafla ya utiaji Saini Mkataba wa Uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Amesema hatua hiyo itaweza kusaidia wananchi kuendelea kutumia huduma ya umeme na kufanya uzalishaji mali au mahitaji ya nyumbani hata pale wanapokuwa na changamoto ya fedha ya kununua umeme huo.
 
Aidha, Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendeleza mradi ulioanzishwa chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha wananchi wanaoishi mazingira yanayofanana na kijijini lakini mipaka ya kiutawala inawatambua wapo mjini wanaunganishiwa huduma ya umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 kama ya wananchi wa vijijini. Amesema yapo maeneo ambayo ni mipaka ya kiutawala inawatenganisha wananchi kati ya mijini na vijijini lakini wananchi hao maisha yao yanafanana.
Makamu wa Rais, amesema azma hiyo, inalenga kufikia lengo la kitaifa, malengo ya “mission 300” pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, kuhakikisha huduma ya umeme inamfikia mtanzania kwa gharama nafuu.
 
Makamu wa Rais ameipongeza TANESCO na Benki ya CRDB kwa hatua hiyo muhimu inayolenga kuimarisha na kuboresha maisha ya wananchi kwa kupata huduma ya umeme.  Amesema ushirikiano huo ni mfano bora wa namna ya Taasisi za Umma na Sekta Binafsi zinavyoweza kuwaunganisha watanzania na kuwekeza nguvu na rasilimali ili kutatua changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Abdulmajid Nsekela amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono na uwepo wa Dira ya Maendeleo 2050. Amesema Serikali na Sekta binafsi kupitia ubunifu itawezesha kutekelezwa na kufanikiwa kwa Dira 2050 inayolenga kujenga uchumi mkubwa, yenye kuzalisha ajira, wenye ushindaji, unaotumia teknolojia na kuboresha maendeleo ya wananchi.
 
Amesema Benki ya CRDB imedhamiria kuwa mshirika wa maendeleo yan chi kwa kutumia uwezo wa kifedha, teknolojia iliyopo, rasilimali ya wataalamu waliopo, mtandao uliopo na ubunifu katika kusaidia kutatua changamoto ya maendeleo ya Taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Razaro Twange amesema upatikaji wa umeme umeendelea kuongezeka nchini na ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme na kusambaza umeme ikiendelea kujengwa. Amesema Tanzania inafikia megawati 4500-4600 hivi sasa huku kukiwa na mtandao wa kiliometa 9000 za kusafirisha umeme, na mtandao wa zaidi ya kilometa 220,000 wa njia za kusambaza umeme.
 
Utiaji wa Saini wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), utawezesha wananchi wa maeneo ya vijiji kuunganishwa bure huduma ya umeme kutokana na ruzuku kutoka Benki ya CRDB, na kwa wananchi maeneo ya mijini watapewa huduma hiyo kwa mkopo wa riba nafuu ambao wataweza kuunganishwa umeme na kufanya shughuli za uzalishaji mali.

DC SHAKA: MIILI YENU ISIWE KITEGA UCHUMI

Na Matukio Daima Media, Kilosa.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amewataka wakulima na wananchi wa Kata ya Magole kuacha kutumia madhara wanayopata katika migogoro ya wakulima na wafugaji kama njia ya kujipatia fedha.
Shaka amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakipokea malipo kutoka kwa watuhumiwa na baadaye kuacha kutoa ushahidi mahakamani dhidi ya vitendo hivyo.
Amesema hali hiyo inaweza kudhoofisha kesi na kuacha mazingira ya matukio ya ukatili kujirudia, hivyo amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola hadi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa.
Lakini wakati Shaka akitoa tahadhari hiyo, wakazi wa Magole wameibua changamoto nyingine inayohusiana na maisha yao ya kila siku ikiwemo upatikanaji wa ardhi ya kilimo na zahanati isiyo na huduma Rafiki.
Wananchi hao wameiomba Serikali kuwawezesha kupata maeneo ya kulima, hususan mashamba yaliyofutwa, wakisema ongezeko la watu limeongeza mahitaji ya ardhi kwa shughuli za kilimo.
Omary Saidi na Elia Chisongela ni miongoni mwa wakazi walioeleza hitaji hilo huku pia wakibainisha changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya kuwa ni changamoto katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Shaka amesema Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote anayechangia migogoro hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia vyombo vya dola katika kushughulikia vitendo vya ukatili.
Mwisho

 

DC SHAKA: MIILI YENU ISIWE KITEGA UCHUMI

Na Matukio Daima Media, Kilosa.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amewataka wakulima na wananchi wa Kata ya Magole kuacha kutumia madhara wanayopata katika migogoro ya wakulima na wafugaji kama njia ya kujipatia fedha.

Shaka amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakipokea malipo kutoka kwa watuhumiwa na baadaye kuacha kutoa ushahidi mahakamani dhidi ya vitendo hivyo.

Amesema hali hiyo inaweza kudhoofisha kesi na kuacha mazingira ya matukio ya ukatili kujirudia, hivyo amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola hadi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa.

Lakini wakati Shaka akitoa tahadhari hiyo, wakazi wa Magole wameibua changamoto nyingine inayohusiana na maisha yao ya kila siku ikiwemo upatikanaji wa ardhi ya kilimo na zahanati isiyo na huduma Rafiki.

Wananchi hao wameiomba Serikali kuwawezesha kupata maeneo ya kulima, hususan mashamba yaliyofutwa, wakisema ongezeko la watu limeongeza mahitaji ya ardhi kwa shughuli za kilimo.

Omary Saidi na Elia Chisongela ni miongoni mwa wakazi walioeleza hitaji hilo huku pia wakibainisha changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya kuwa ni changamoto katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Shaka amesema Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote anayechangia migogoro hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia vyombo vya dola katika kushughulikia vitendo vya ukatili.

Mwisho