Marekani Yawafukuza Wajumbe Wawili wa Iran Baada ya UNGA

WASHINGTON: Marekani imewafukuza nchini humo wajumbe wawili wa ujumbe wa Iran waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA), baada ya kudaiwa kukaidi amri ya kuondoka nchini humo baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

Idara ya Nchi ya Marekani imesema wajumbe hao walibainika kuwa bado wapo New York siku kadhaa baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

“Wajumbe wengine wawili wa ujumbe wa Iran walikutwa bado New York muda mrefu baada ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kumalizika. Sasa wameondolewa nchini Marekani,” afisa wa Marekani aliliambia Shirika la Habari la AFP.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesisitiza utekelezaji wa amri hiyo.

Vyombo vya habari vya Marekani viliripoti kuwa Idara ya Nchi iliwaelekeza Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, pamoja na ujumbe wake kuondoka nchini humo siku ya Jumatatu.

Hatua ya kuwafukuza wajumbe hao ilichukuliwa baada ya Marekani kupata taarifa kutoka kwa Ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa kwamba bado walikuwa nchini humo hadi Ijumaa.

Kwa mujibu wa Axios, mmoja wa wajumbe hao aliondoka nchini Marekani Ijumaa usiku, huku mwingine akiondoka Jumamosi asubuhi.

Hatua hiyo imekuja wakati uhusiano kati ya Washington na Tehran ukiendelea kuwa na mvutano, huku pande hizo zikiwa zimekuwa zikifanya mawasiliano kuhusu masuala mbalimbali.

Maafisa wa Marekani na Iran walikutana wiki iliyotangulia mjini New York pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Rais wa Marekani, Donald Trump, awali alikataa pendekezo kutoka Tehran kuhusu kufunguliwa upya kwa mazungumzo yanayohusiana na Mlango wa Hormuz.

Hata hivyo, Trump aliwaambia waandishi wa habari nchini Marekani kuwa anatarajia mazungumzo kati ya pande hizo kuanza tena katika siku zijazo.

Kwa upande mwingine, Shirika la Habari la Serikali ya Iran, IRNA, limeripoti kuwa Tehran haikuwa na mazungumzo yoyote ya moja kwa moja yaliyopangwa na Washington.

Mvutano huo unaendelea kufuatiliwa huku hatua ya Marekani dhidi ya wajumbe hao ikiongeza hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu uwezekano wa mazungumzo mapya kati ya nchi hizo mbili.

Fursa za Ajira Saudi Arabia na UAE Zatangazwa kwa Watanzania, Maombi Mwisho Oktoba 4, 2026

Global Publishers
October 4, 2026
1,740 views
0 Comments

BRAVO JOB CENTER AGENCY LIMITED inatangaza fursa za ajira kwa waombaji wenye sifa mbalimbali za kufanya kazi Saudi Arabia na Falme za Kiarabu (UAE).

NAFASI ZA MADEREVA WA MAGARI MAKUBWA – SAUDI ARABIA

Waombaji wanahitajika kuwa na:

✅ Uzoefu wa kuendesha magari makubwa wa angalau miaka 2
✅ Leseni halali ya udereva
✅ Rekodi nzuri ya udereva
✅ Umri wa miaka 35 au zaidi
✅ Uwezo wa kufanya kazi kwa muda mrefu/shift ndefu

💰 MASLAHI YA MADEREVA

✅ Mshahara unaoshindana na viwango vya soko
Usafiri wa kwenda kazini kila siku
✅ Posho za safari
✅ Bima ya afya inayotolewa na kampuni
✅ Tiketi ya ndege

🇦🇪 FURSA ZA AJIRA – UAE

BRAVO JOB CENTER AGENCY LIMITED, kwa kushirikiana na SAEY BUSINESS – Misri, inatangaza fursa za ajira nchini UAE.

🎁 MASLAHI YA MFANYAKAZI

✅ Mshahara na posho kulingana na mkataba wa mwajiri
✅ Malazi hutolewa
✅ Huduma za matibabu bure
✅ Usafiri hutolewa kila siku kwenda kazini
✅ Chakula/kitchen facility hutolewa
✅ Saa 8 za kazi kwa siku, siku 6 kwa wiki
✅ Siku 1 ya mapumziko kwa wiki
✅ Overtime hulipwa
✅ Likizo ya siku 30 zenye malipo baada ya kutimiza miezi 12
✅ Tiketi ya kurudi UAE–Tanzania baada ya kukamilika kwa mkataba
✅ Mkataba wa awali wa miaka 2, unaoweza kuongezwa kwa makubaliano
✅ Bima na fidia kwa mujibu wa sheria za nchi ya ajira

📋 UTARATIBU WA AJIRA

Waombaji watachaguliwa kulingana na mahitaji ya mwajiri na nafasi husika. Waombaji watakaokidhi vigezo watawasilishwa kwa mwajiri kwa ajili ya hatua zinazofuata za mchakato wa ajira.

Mwisho wa kufanya usaili ni Oktoba 4, 2026

📞 MAWASILIANO NA MAOMBI

BRAVO JOB CENTER AGENCY LIMITED

📞 0714 326005
📞 0781 634642
📞 0678 805452

📍 OFISI:
Rissa Tower, Lumumba na Amani, Dar es Salaam.

📢 WOTE MNKARIBISHWA!
🤝 Mwambie na mwenzako kuhusu fursa hii

Mume Adaiwa Kumuua Mkewe kwa Risasi Bunju B, jijini Dar – Video

DAR ES SALAAM: Tukio la kushtua limetokea Mtaa wa Senzele, Kata ya Bunju B, jijini Dar es Salaam, baada ya Laurent Kweka kudaiwa kumuua mkewe, Jeni Urassa, kwa kumpiga risasi kichwani na kisha kujisalimisha kwa Polisi.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Alhamisi, Oktoba 1, 2026, majira ya saa 11:30 alfajiri, ndani ya nyumba walimokuwa wakiishi wanandoa hao.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi kwa ajili ya upelelezi.

Kwa mujibu wa Mafwele, Laurent na marehemu Jeni walikuwa wanandoa na wote walitoka mkoani Kilimanjaro.

Amesema baada ya uchunguzi kukamilika pamoja na taratibu nyingine za kisheria, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Mgogoro wa nyumba wadaiwa kuchangia

Mfanyakazi wa ndani wa familia hiyo, Rebecca Mbasha, ambaye amesema amefanya kazi katika nyumba hiyo kwa takribani miaka minane, amedai kuwa mauaji hayo yalitokana na mgogoro wa muda mrefu wa kifamilia kuhusu umiliki wa nyumba.

Rebecca amesema Jeni alikuwa akitaka kubadilisha majina yaliyokuwa kwenye hati ya nyumba ili kubakiza jina lake pamoja na majina ya watoto wao.

Kwa mujibu wa Rebecca, Jeni alieleza kuwa yeye ndiye aliyenunua kiwanja na kujenga nyumba hiyo.

Akisimulia kinachodaiwa kutokea siku ya tukio, Rebecca amesema Laurent aliingia nyumbani na muda mfupi baadaye alimsikia Jeni, kisha akasikia kishindo.

Amesema aliporejea ndani ya nyumba, alimkuta Laurent akitoka chumbani akiwa ameshika bastola na kumwambia, “nimeshamaliza kazi.”

Rebecca amesema alipoingia chumbani alimkuta Jeni akiwa ameanguka chini akiwa na jeraha kichwani.

Aliwahi kutishiwa kwa bastola

Jacqueline Nkaya, ambaye ni mama mdogo wa marehemu, amesema wanandoa hao walikuwa na mgogoro wa muda mrefu.

Amedai kuwa wakati mmoja Jeni aliwahi kutishiwa kuuawa kwa kutumia bastola na mumewe na kwamba tukio hilo liliripotiwa Polisi.

Jacqueline amesema Laurent aliondoka Dar es Salaam na kwenda mkoani Kilimanjaro, ambako alikaa kwa takribani miezi miwili kabla ya kurejea jijini siku ya tukio.

Hata hivyo, majirani wa familia hiyo wamesema hawakuwa na taarifa kuhusu kuwepo kwa migogoro hiyo, wakieleza kuwa kwa nje familia hiyo ilionekana kuishi kwa amani tangu ilipohamia katika nyumba hiyo Desemba 2025.

Marehemu Jeni ameacha watoto wanne, watatu wakiwa wanafunzi na mmoja ambaye bado hajaanza shule.

Polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku Laurent akiendelea kushikiliwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria.

Chivayo na Mkewe Kuzikwa Bila Kuonyeshwa Miili, Familia Yafunguka

Global Publishers
October 4, 2026
930 views
0 Comments

Familia ya mfanyabiashara wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, imesema hakutakuwa na utaratibu wa kuonyeshwa miili ya marehemu Chivayo na mke wake, Lulu, kabla ya mazishi kutokana na hali ya miili yao baada ya ajali ya helikopta iliyowaua.

Msemaji wa familia, Hebert Chivayo, amesema miili ya wanandoa hao ilipata madhara makubwa katika ajali hiyo, huku sehemu za miili yao zikitawanyika katika eneo la tukio.

Akizungumza na waombolezaji waliokusanyika katika makazi ya marehemu Ijumaa jioni, Hebert amesema hali hiyo imefanya familia kuamua kutokuwa na utaratibu wa kuonyeshwa miili wakati wa mazishi.

Amesema wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi bado wanaendelea na vipimo vya DNA kwa ajili ya kutambua na kutenganisha mabaki ya waathirika, kabla ya familia kuendelea na maandalizi ya mazishi.

Hadi sasa, familia haijatangaza tarehe rasmi ya mazishi.

Chivayo, ambaye baada ya kifo chake alitangazwa kuwa shujaa wa mkoa na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, alifariki Jumatano pamoja na mke wake na abiria wengine baada ya helikopta waliyokuwa wakisafiria kuanguka katika eneo la vijijini la Marondera.

Familia inaendelea kusubiri kukamilika kwa mchakato wa utambuzi wa mabaki kabla ya kutangaza mipango zaidi kuhusu mazishi.

Makonda ataka michezo itumike elimu utunzaji misitu – HabariLeo

MOROGORO; WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema michezo inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi misitu na mazingira, kwani wanapoweza kuona na kunufaika na rasilimali hizo.

Makonda, amesema hayo  Oktoba 3, 2026 wakati wa ziara yake eneo la mashindano ya Serengeti Rally of Tanzania 2026 katika  Shamba la Miti Morogoro, ambapo pia alitembelea banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na kupata maelezo kuhusu shughuli za uhifadhi zinazotekelezwa na wakala huo  .

Waziri Makonda amesema mashindano yanayofanyika katika mazingira ya misitu yanatoa fursa kwa wananchi kujifunza kwa vitendo kuhusu thamani ya misitu na umuhimu wa kuilinda.

“Ni jambo la kujifunza kwa kuona, ukijifunza kwa vitendo unapata fursa kubwa zaidi ya kuelewa,” amesema Makonda.

Makonda amesema kuwa misitu ina mchango muhimu katika maisha ya wananchi, ikiwemo kusaidia upatikanaji wa mvua na mazingira bora ya kuishi, hivyo jamii inapaswa kuendelea kunufaika nayo na kuzilinda rasilimali hizo.

Kwa kutambua umuhimu huo , amewahimiza  Watanzania kuwa walinzi wa misitu kwa kutambua thamani yake na kushiriki kikamilifu katika kuilinda dhidi ya uharibifu.

“ Manufaa yanayotokana na misitu yanaweza kuendelea kupatikana iwapo rasilimali hizo zitatunzwa kwa kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Makonda.

Kwa upande wake, Ofisa Utalii wa TFS, Salome Kivuyo amesema Wakala huo unaendelea kuwashirikisha wadau na wafadhili katika kuendeleza michezo ndani ya maeneo ya misitu kwa kuzingatia taratibu za uhifadhi.

Kivuyo amesema kuwa michezo hiyo ni pamoja na  mbio za baiskeli, pikipiki na marathon, kwa lengo la kuunganisha michezo na uhifadhi wa mazingira.

“Tunawakaribisha wadau mbalimbali waje tushirikiane katika kuleta michezo ndani ya misitu yetu, ili kuwapa Watanzania fursa ya kufurahia michezo hiyo, huku wakijifunza, kutambua na kuthamini thamani ya misitu na umuhimu wa kuilinda,” amesema Kivuyo.

Akielezea mashindano hayo amesema yameandaliwa vema na kufanyika katika mazingira ya Shamba la Miti Morogoro, na kwa kuunganishwa michezo na uhifadhi kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira ikiwa na kukuza michezo na utalii.

Kivuyo amesema kuwa Mashindano ya Serengeti Rally of Tanzania 2026 yanayofanyika  Shamba la Miti Morogoro, linalosimamiwa na TFS, yamekuwa fursa ya kuunganisha michezo, uhifadhi, utalii na elimu ya mazingira.

 

Viongozi wa dini Kimara wapewa msaada wa vyakula – HabariLeo

DAR ES SALAAM: Masheikh, walimu wa madrasa na viongozi wa dini katika Kata ya Kimara, Dar es Salaam, wamepatiwa tani moja na kilo 400 za mchele na kiasi kama hicho cha unga kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Nino.

Msaada huo umetolewa na mfanyabiashara, mkulima na mchimbaji wa madini, Dennis Mguye maarufu King Papa, wakati alipokutana na viongozi hao wa dini, akisema ameamua kuwafariji kutokana na mchango wao katika kuelimisha jamii bila kutegemea malipo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mguye amesema ametoa chakula hicho pia kutokana na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuhusu mvua za El Niño, hivyo kuona umuhimu wa jamii kuwa na maandalizi ya chakula endapo kutatokea changamoto zinazoweza kuathiri maisha ya wananchi.

Amesema ni muhimu kwa watu wenye uwezo kujenga utamaduni wa kuwajali na kuwasaidia wengine katika maisha ya kila siku, akitoa wito kwa wafanyabiashara, wabunge, madiwani na viongozi wengine kutumia nafasi walizonazo kusaidia jamii badala ya kuwafikia wakati wa kampeni pekee.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya BAKWATA Kata ya Kimara, Khamis Rashid, amesema kitendo hicho ni mfano kwa watu wengine ambao Mwenyezi Mungu amewajaalia uwezo wa kutoa kwa ajili ya jamii, huku akimshukuru mfanyabiashara huyo kwa kuwajali viongozi wa dini.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mavurunza, Batista Chang’a, amesema msaada huo si mara ya kwanza kutolewa na Mguye, akieleza kuwa amekuwa akisaidia jamii hiyo zaidi ya mara tatu au nne na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia moyo wa kusaidia watu.

Maria Nyerere awabariki washiriki wa Vodacom Nyerere Cycling Tour – HabariLeo

Meneja Mauzo na mkakati wa biashara wa kanda ya Dar es Salaam na Pwani wa Vodacom Tanzania Plc, Caleb Majo akizungumza na waendesha baiskeli wa Nyerere Cycling Tour wakati wa hafla ya kuwaaga na kupata baraka kutoka kwa Mama Maria Nyerere kabla ya kuanza mashindano ya Vodacom Coastal Classic pamoja na safari ya Nyerere Cycling Tour kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, mkoani Mara. Safari hiyo inalenga kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kupitia mchezo wa baiskeli na shughuli za maendeleo ya jamii.

Mtoto wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Madaraka Nyerere akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga waendesha baiskeli wa Nyerere Cycling Tour na kutoa salamu za familia ya Mwalimu Nyerere. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam kabla ya kuanza safari ya Nyerere Cycling Tour kuelekea Butiama, mkoani Mara, ikiwa na lengo la kumuenzi Mwalimu Nyerere na kuunganisha mchezo wa baiskeli na jitihada za kuleta matokeo chanya katika jamii.

Waendesha baiskeli wa msafara wa Nyerere Cycling Tour wakimsikiliza Mama Maria Nyerere akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga na kupata baraka zake kabla ya kuanza mashindano ya Vodacom Coastal Classic pamoja na safari ya Nyerere Cycling Tour kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, mkoani Mara. Safari hiyo inalenga kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, huku ikiunganisha mchezo wa baiskeli na jitihada za kuleta matokeo chanya katika jamii.

Waendesha baiskeli wa msafara wa Nyerere Cycling Tour wakisikiliza wazungumzaji wakati wa kikao cha kuwaaga na kupata baraka kutoka kwa Mama Maria Nyerere kabla ya kuanza mashindano ya Vodacom Coastal Classic pamoja na safari ya Nyerere Cycling Tour kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, mkoani Mara. Safari hiyo inalenga kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, huku ikiunganisha mchezo wa baiskeli na jitihada za kuleta matokeo chanya katika jamii.

Wafanyakazi wa Vodacom Tanzania Plc wakiwa katika picha ya pamoja na Mama Maria Nyerere, Madaraka Nyerere, Meneja Mauzo na Mkakati wa Biashara wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani wa Vodacom Tanzania Plc Caleb Majo na Mkuu wa kitengo cha tahadhari wa Stanbic Bank, Wilmot Ishengoma, baada ya hafla ya kuwaaga na kupata baraka kwa waendesha baiskeli wa Nyerere Cycling Tour jijini Dar es Salaam. Safari hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, mkoani Mara, inalenga kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kupitia mchezo wa baiskeli na shughuli za maendeleo ya jamii.

Mama Maria Nyerere (katikati) akizungumza wakati alipokutana na waendesha baiskeli wa msafara wa Nyerere Cycling Tour ambapo Vodacom Tanzania Plc waliokwenda kumuaga na kupata baraka zake kabla ya kufanya mashindano ya Vodacom Coastal Classic pamoja na Nyerere Cycling Tour.

Safari ya Nyerere Cycling Tour kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, mkoani Mara, inalenga kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kuunganisha mchezo wa baiskeli na jitihada za kuleta matokeo chanya katika jamii. Kupitia safari hiyo, waandaaji na washirika wanatarajia kutekeleza shughuli mbalimbali zinazogusa elimu, afya, uhifadhi wa mazingira, elimu ya fedha na maendeleo ya jamii zikiwemo utoaji wa madawati 1,000, ujenzi wa madarasa 10, ukarabati wa madarasa 40 na upandaji miti, huku shughuli hizo zikitarajiwa kuwafikia zaidi ya watu 25,000.

Tukio hilo lilishuhudiwa na Meneja mauzo na mkakati wa biashara wa kanda ya Dar es salaam na Pwani Vodacom Tanzania PLC Caleb Majo(kulia), mtoto wa Mwalimu Nyerere – Madaraka Nyerere (wa pili kushoto) na Wilmot Ishengoma, Mkuu wa Kitengo cha Tahadhari wa Stanbic Bank Tanzania (kushoto) pamoja na wadau wengine wa mchezo wa baiskeli. Tukio hilo lilifanyika wikendi hii, jijini Dar es salaam.