Wadau wataka mipango ya tabianchi izingatie jinsia

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiendelea kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, wadau wameonya kuwa vita hiyo haitakuwa na tija iwapo haitazingatia masuala ya kijinsia, hususan haki za afya ya uzazi na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Onyo hilo linakuja wakati tathmini ya mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika wilaya ya Kinondoni kuanzia mwaka 2013/14 hadi 2024/25 ikionyesha kuwa juhudi nyingi zimejikita zaidi kwenye miundombinu kama usafishaji wa mifereji na utunzaji wa mazingira, huku mahitaji maalumu ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu yakiachwa pembezoni.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Shirika la My Legacy, Fortunata Temu, amesema makundi hayo yameendelea kubeba mzigo mkubwa wa athari za tabianchi, ikiwemo ukosefu wa maji safi, ongezeko la magonjwa na vitendo vya ukatili vinavyochochewa na mazingira magumu ya kiuchumi na kijamii.

Amesema kupitia mradi wa “Kesho Njema”, shirika hilo lilifanya tathmini katika kata za wilaya ya Kinondoni na kubaini kuwa mipango mingi ya tabianchi haijajumuisha mtazamo wa kijinsia ipasavyo.

“Wengi huwa wanaangalia athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye upande wa mazingira tu. Ukweli ni kwamba zipo athari nyingine ambazo zinawakumba moja kwa moja wanawake, watoto hata watu wenye ulemavu, lakini mipango iliyopo haingalii kwa jicho hilo.

“Tulibaini kuwa ushirikiano kati ya idara za mazingira, afya na jinsia bado ni mdogo. Pia, takwimu zilizogawanywa kijinsia hazitoshelezi, na ushiriki wa wanawake, vijana na makundi yaliyotengwa katika uamuzi wa tabianchi ni hafifu,” amesema Fortunata.

Ameongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi ni ajenda mtambuka inayohitaji kuangaliwa kwa upana wake, akisisitiza umuhimu wa kuingiza viashiria vya haki za afya ya uzazi na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia katika mikakati ya tabianchi kuanzia ngazi za mitaa.

Fortunata amesema ni muhimu pia kuimarisha uratibu wa kisekta na kutenga bajeti zinazozingatia jinsia ili kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma katika harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Programu wa shirika hilo, Amina Ally, amesema mbali na tathmini, mradi huo uliotekelezwa kwa mwaka mmoja kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, umewezesha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kukabiliana na athari za tabianchi kwa vitendo.

Mkurugenzi wa shirika la My Legacy Fortunata Temu (kushoto) akizungumza kuhusu athari za mabadiliko ya tabia nchini. Kulia ni mratibu wa programu Amina Ally.

Amesema miti 2,000 ya kivuli na matunda imepandwa katika shule 24 za Wilaya ya Kinondoni ili kupunguza joto na kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Wanafunzi pia wamepatiwa mafunzo ya upandaji na utunzaji wa miti, pamoja na matumizi ya mifumo rahisi ya umwagiliaji kwa kutumia chupa za plastiki zilizotumika, hatua inayosaidia kupunguza taka ngumu.

“Jumla ya wanafunzi 775 kutoka shule 25 wamefikiwa kupitia vilabu vya WASH kwa vipindi maalumu vya elimu ya tabianchi. Tumetumia mbinu shirikishi kama maigizo, hadithi na sanaa kuwajengea uelewa kuhusu matumizi sahihi ya nishati, uhifadhi wa mazingira na uhusiano wa tabianchi na masuala ya kijinsia,” amesema Amina.

Aidha, shirika hilo liliandaa mdahalo wa kijamii uliopewa jina la ‘Mgahawa wa Maarifa’ uliowakutanisha viongozi wa mitaa, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujadili changamoto na suluhisho za tabianchi katika maeneo yao.

Akichangia katika mdahalo huo, mkazi wa Kawe, Richard Mtanga, amesema kuwa haitawezekana kuwa na mkakati madhubuti wa tabianchi bila kushughulikia kwa uzito masuala ya kijinsia.

“Hakuna mkakati madhubuti wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi iwapo hautashughulikia ukatili wa kijinsia na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi na haki zake. Ulinzi na utu lazima viwe sehemu ya hatua za kukabiliana na tabianchi,” amesema.

Afrika kugeukia teknolojia ya AI kuimarisha usalama wa mitihani

Arusha. Mabaraza ya mitihani barani Afrika yameshauriwa kutumia mifumo ya kidijitali, uchanganuzi wa data na akili unde (AI) kubaini na kudhibiti udanganyifu wa mitihani unaozidi kuwa wa kisasa, ili kuboresha ubora wa elimu na kuzalisha wanafunzi wenye ushindani katika soko la ajira.

Wito huo umetolewa leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, katika mkutano wa 42 wa mwaka wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu Afrika (AEAA), unaofanyika Arusha kwa siku nne na kuwakutanisha zaidi ya wajumbe 350 kutoka nchi 28 za Afrika na mabara mengine.

Mkutano huo ulioandaliwa chini ya uenyeji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), umewakutanisha maofisa wa wizara za elimu, mabaraza ya mitihani, wataalamu wa tathmini na wadau wa elimu kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha mifumo ya tathmini barani Afrika kutokana na kasi ya maendeleo ya teknolojia, hususan matumizi ya AI.

Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo amesema njia za jadi za kulinda usalama wa mitihani hazitoshi tena kukabiliana na changamoto zinazotokana na matumizi ya simu janja, mitandao ya kijamii na AI.

Amesema udanganyifu wa mitihani umebadilika kutoka mbinu za kawaida na sasa unaweza kufanyika kupitia vifaa na majukwaa ya kidijitali yanayowezesha taarifa kusambazwa kwa haraka.

“Usalama wa mitihani haupaswi kuishia katika kuzuia mwanafunzi kuingia na nyenzo zisizoruhusiwa kwenye chumba cha mtihani, bali unapaswa kuanzia hatua ya uandaaji wa maswali hadi utoaji wa matokeo,” amesema.

Amesema hatua hizo zinapaswa kujumuisha uandaaji na uchapishaji wa maswali, usafirishaji na uhifadhi wake, uendeshaji wa mitihani, usahihishaji, uchakataji wa taarifa na utoaji wa matokeo.

“Kadiri teknolojia inavyoendelea, udanganyifu katika mitihani nao unazidi kuwa wa kisasa, huku simu janja, mitandao ya kijamii na AI zikitajwa miongoni mwa changamoto zinazohitaji mifumo mipya ya usalama,” amesema.

Hata hivyo, Profesa Nombo amesema teknolojia hizo hazipaswi kuonekana kama tishio pekee, bali zitumike pia kutafuta suluhisho la changamoto hizo.

“Niwahimize mabaraza ya mitihani barani Afrika kuwekeza katika mifumo imara ya usalama wa kidijitali, uchanganuzi wa data na zana zinazotumia AI ambazo zinaweza kusaidia kubaini viashiria vya udanganyifu na dosari katika mchakato wa mitihani,” amesema.

Kwa upande wake, Rais wa AEAA, Dk Eshetu Kebede Gichoro, amesema pamoja na uwekezaji katika mifumo ya kiteknolojia, nchi za Afrika zinapaswa kuweka sera na miongozo ya wazi ya matumizi ya AI katika tathmini ya elimu.

Amesema miongozo hiyo inapaswa kuzingatia maadili, uwazi, usalama wa data, usawa na haki kwa wanafunzi.

Kwa mujibu wa Dk Gichoro, AI inatoa fursa kubwa za kuboresha mifumo ya tathmini, ikiwamo mitihani inayoweza kubadilika kulingana na uwezo wa mwanafunzi, uchanganuzi wa utabiri na uundaji wa njia binafsi za ujifunzaji.

Hata hivyo, amesema teknolojia hiyo pia inazua maswali kuhusu usawa, maadili na umiliki wa data, hasa kwa nchi zinazotumia mifumo ya kiteknolojia inayotengenezwa nje ya Afrika.

Amesema bara hilo linapaswa kujenga mifumo yake ya tathmini inayounganisha teknolojia na mahitaji yake, badala ya kutegemea mifumo ya nje ambayo huenda isiakisi uhalisia wa Afrika.

“Endapo Afrika haitajenga mifumo yake huru ya tathmini inayounganisha teknolojia, tunahatarisha kuwa watumiaji wa mifumo iliyoagizwa kutoka nje ambayo huenda isiakisi uhalisia wala kutumikia matarajio yetu,” amesema.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Ally Mohamed amesema mkutano huo unalenga kutafakari namna mifumo ya tathmini inavyoweza kubadilishwa ili kukabiliana na kuongezeka kwa matumizi ya AI na teknolojia duniani.

Amesema pia mkutano huo unatoa fursa kwa wataalamu kutoka nchi mbalimbali kubadilishana tafiti, uzoefu na ubunifu kuhusu matumizi ya teknolojia katika kuboresha tathmini ya elimu.

“Pamoja na usalama wa mitihani, pia utaangazia namna data inayozalishwa kupitia tathmini inavyoweza kutumika katika kuboresha elimu,” amesema.

Ameongeza kuwa mkutano huo utaangazia pia umuhimu wa kuhakikisha matumizi ya teknolojia hayawaachi nyuma wanafunzi kutoka maeneo yenye changamoto za kiuchumi, vijijini na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu.

CookFund yachochea mapinduzi ya nishati safi, wanafunzi 62,000 wanufaika

Dar es Salaam. Zaidi ya wanafunzi 62,000 nchini wamenufaika na matumizi ya nishati safi ya kupikia kutokana na usakinishaji wa majiko ya kisasa katika shule na taasisi za umma zaidi ya 45, huku idadi ya majiko ikizidi 170.

Hatua hiyo imechukuliwa kupitia programu ya CookFund, inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF).

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Machi 26, 2026, katika hafla ya makabidhiano ya msaada huo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Bunge, jijini Dar es Salaam, ikionesha hatua muhimu katika kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, pamoja na kukabiliana na changamoto ya ukataji miti.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kipaumbele cha kimkakati cha Taifa katika kulinda mazingira, kuboresha afya ya jamii, na kuongeza ufanisi wa kiuchumi.

Amesema kwa kuzipatia shule na taasisi za umma teknolojia za kisasa za kupikia, Serikali inalenga kupunguza hewa chafuzi, kulinda rasilimali za misitu, na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

“Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kupanua upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 hadi 2034,” amesema Naibu Waziri Makamba.

Jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini zinaongozwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali, zikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi, Wizara ya Maliasili na Utalii, na Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira.

Mpango huo unalenga taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa wakati mmoja, hususan shule, ili kuondokana na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira, kama kuni na mkaa.

Akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Ulaya, Mkuu wa Ushirikiano nchini Tanzania, Marc Stalmans, amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kusaidia mpito kuelekea matumizi ya nishati safi.

“Tunasaidia watu kuhamia kwenye mbinu endelevu zinazolinda mazingira huku zikichochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira, na kuboresha upatikanaji wa nishati katika sekta mbalimbali,” amesema.

Kwa upande wake, Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kiufundi wa UNCDF, Peter Malika, amesema programu hiyo imewekeza Dola milioni 10.1 za Marekani katika biashara ndogo na za kati 102, pamoja na kusaidia taasisi 45 katika wilaya 14 za mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, na Mwanza.

Amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yana mchango mkubwa katika kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, huku yakiboresha usalama, afya, na ufanisi katika shughuli za upishi shuleni.

Kwa mujibu wa wataalamu, matumizi ya kuni na mkaa huchangia uzalishaji wa chembechembe hatarishi zinazosababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji, ikiwemo pumu na saratani ya mapafu.

Kupitia CookFund, teknolojia mbalimbali za nishati safi zimeanza kutumika, zikiwemo majiko ya umeme, majiko ya bayoethanoli, majiko banifu, pamoja na matumizi ya gesi na mkaa mbadala.

Kizimkazi yaaga kero ya maji, Rais Samia atoa neno

Unguja. Rais, Samia Suluhu Hassan amesema kero ya maji iliyodumu kwa muda mrefu Kizimkazi na maeneo mengine ya Kusini Unguja, imefikia mwisho, baada ya kuzindua miradi miwili ya maji huku akiwataka wananchi kuitunza miundombinu hiyo.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Agosti 13, 2026, alipozungumza na wananchi wa Kizimkazi Kibuteni, Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kuzindua miradi hiyo ikiwa ni sehemu ya shughuli za Tamasha la Kizimkazi.

Miradi hiyo inahusisha chanzo cha maji chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 2.4 kwa siku na tanki lenye ujazo wa lita milioni moja.

Rais Samia amesema Kizimkazi na Kusini kwa jumla zinakabiliwa na changamoto kubwa ya maji kwa muda mrefu, lakini utekelezaji wa miradi hiyo umeiwezesha Serikali kumaliza tatizo hilo.

“Leo tatizo la maji tumelihitimisha. Ndugu zangu wa Kusini, Kibuteni na Kizimkazi, tujipongeze sana,” amesema.

Amesema chanzo cha maji Kizimkazi kilijengwa mwaka 1974 kikiwa na tanki lenye ujazo wa lita 150,000, lakini baadaye kilishindwa kukidhi mahitaji kutokana na ukuaji wa eneo hilo na uwekezaji ulioongezeka.

Amesema Serikali haikuangalia mahitaji ya sasa pekee, ambayo ni takribani lita 500,000, bali imezingatia mahitaji ya baadaye kutokana na ongezeko la watu, miji na uwekezaji.

Rais Samia amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hiyo, akisema Serikali imetumia fedha na utaalamu mkubwa kuitekeleza.

“Tumetengenezewa, tutunze tusiharibu. Tunajua tulipotoka, tulikuwa na tatizo kubwa la maji. Leo tumepata ufumbuzi wa maji, tutunze miundombinu hii na sisi tuwe walinzi kuilinda sisi wenyewe,” amesema.

Katika ziara hiyo, Rais Samia amepanda mti, amepokea gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Kizimkazi na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Chuo cha Amali unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar.

Kuhusu Kituo cha Afya Kizimkazi, amesema kinaendelea kuboreshwa na sasa kinatarajiwa kutoa huduma zinazokaribia kiwango cha hospitali ya wilaya, ikiwamo huduma za dayalisisi kwa gharama nafuu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizindua Mradi wa Maji Kizimkazi katika moja ya matukio kuelekea kilele cha Tamasha la Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja Agosti 13, 2026.

Amesema kituo hicho pia kitakuwa na chumba maalumu cha mazoezi ya viungo kitakachotumiwa na wachezaji pamoja na watoto wanaozaliwa wakiwa na changamoto mbalimbali.

Amesema uwanja wa mpira wa Samia Academy unaojengwa katika eneo hilo unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu au Januari 2027, hivyo kituo hicho kitakuwa muhimu katika kutoa huduma za afya kwa wachezaji.

Pia, amesema gari la wagonjwa lililotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) litasaidia kuboresha huduma za afya katika kituo hicho.

Rais Samia amesisitiza kuwa, wananchi wanapaswa kutunza miradi hiyo kwa kuwa ni uwekezaji unaolenga kuboresha maisha yao.

“Hii ni maisha yetu, fursa yetu, uchumi na ustawi wa wananchi,” amesema.

Pia, amewataka wananchi kuendelea kulinda amani na kuunga mkono maendeleo yanayotekelezwa na Serikali.

‘Maji yamefika vijiji 10,756’

Waziri wa Maji, Juma Aweso amesema Serikali imefanya maendeleo makubwa katika sekta ya maji na kufikisha huduma hiyo kwa asilimia 85 kwa wananchi nchini.

Amesema kati ya vijiji 12,333 vilivyopo Tanzania, 10,756 vimefikiwa na huduma ya maji, huku vijiji 1,575 vikiwa katika hatua za kukamilisha miradi.

“Hakuna kijiji kitakachopitwa bila kupewa maji,” amesema Aweso.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizindua Mradi wa Maji Kizimkazi katika moja ya matukio kuelekea kilele cha Tamasha la Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja Agosti 13, 2026.

Amesema utekelezaji wa miradi ya Kizimkazi umetokana na maelekezo ya Rais Samia na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi yaliyolenga kuhakikisha tatizo la maji katika eneo hilo linamalizika.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis amesema wananchi wameanza kuona faida ya mradi huo na kuahidi kulinda miundombinu yake.

Baadhi ya wananchi wameeleza furaha yao, wakisema changamoto ya maji iliyodumu kwa miaka mingi sasa inaanza kuwa historia.

Mwachumu Haji, mkazi wa Kizimkazi, amesema hali ya upatikanaji wa maji ilikuwa mbaya, lakini sasa matumaini ya kupata huduma hiyo yameongezeka.

Juma Kamis Juma amesema wananchi watahakikisha wanailinda miradi hiyo kwa sababu wanaufahamu uchungu wa kukosa maji.

Aliyedai fidia ya Sh40 milioni kwa kulea mimba ya mtoto asiye wake, agonga mwamba kortini

Singida. Omary Mgana, amegonga mwamba katika jitihada zake za kudai fidia ya Sh40 milioni kutoka kwa mke wake wa zamani, Hadija Willa, akidai alimficha ujauzito wa mwanaume mwingine wakati akifunga naye ndoa mwaka 1997.

Omary alidai Sh10 milioni alizotumia katika huduma za ujauzito na kujifungua, pamoja na Sh30 milioni alizodai kutumia kumlea na kumsomesha mtoto huyo hadi kufikia utu uzima.

Alidai aligundua mwaka 2021, kwamba mtoto huyo ambaye wakati huo alikuwa na miaka 24, hakuwa wake. Pia, aliiomba mahakama iamuru kuondolewa kwa ubini wake katika nyaraka za mtoto huyo.

Hata hivyo, Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Singida imetupilia mbali rufaa yake na kusimamia uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Singida uliokataa madai hayo.

Katika hukumu iliyotolewa Agosti 14, 2026 na Jaji, Ayoub Mwenda na kuwekwa kwenye tovuti ya Mahakama Agosti 17, 2026, ilieleza Omary alishindwa kuthibitisha kuwa alifichwa ujauzito huo.

Jaji alisema madai ya kurejeshewa fedha yangekuwa na msingi kama Hadija angeuficha ujauzito wakati wa ndoa, lakini ushahidi ulionyesha Omary alikuwa akijua hali hiyo.

“Nimepitia ushahidi uliopo na sijaona kasoro katika hitimisho la mahakama ya chini. Kama ilivyoelezwa kwa usahihi na mahakama ya chini, mdaiwa angeweza kuhukumiwa kwa kosa la kuficha ujauzito iwapo tu, katika siku ya harusi angeulizwa kama ana ujauzito au la, jambo ambalo halikutokea,” alisema.

Kwa mujibu wa Jaji Mwenda, kumbukumbu za kesi zinaonyesha swali aliloulizwa Hadija siku ya ndoa lilikuwa kama alikuwa tayari kufunga ndoa na Omary.

“Hakuna sheria inayomlazimisha mwanamke kusema kwa hiari kama ana mimba wakati wa kujiandaa kufunga ndoa ikiwa hajaulizwa,” alisema.

Hivyo, Jaji alisema ushahidi ulionyesha Hadija alimweleza Omary kabla ya ndoa kwamba alikuwa na ujauzito wa mwanaume mwingine.

Hadija katika utetezi wake alisema wakati Omary alipokuwa akimchumbia, alimweleza kuwa alikuwa na mwanaume mwingine aliyempa ujauzito, lakini Omary alisisitiza kumuoa akisema nyumba ya ndoa haizai mtoto haramu.

Walipofunga ndoa mwaka 1997, Hadija alikuwa na ujauzito wa miezi minne hadi mitano na alijifungua Oktoba 10, 1997.

Awali alimpa mtoto jina Mohamed Joseph, lakini Hadija alieleza kuwa Omary ndiye aliyesisitiza jina libadilishwe na baadaye mtoto akaitwa Juma Omary Juma Mgana.

Katika madai yake, Omary alisema alimtunza mtoto huyo akiamini ni wake, akigharamia huduma za ujauzito, kujifungua, malezi na elimu.

Alisema mwaka 2021 ndipo Hadija alipomweleza kuwa mtoto huyo si wake. Hata hivyo, katika shauri la talaka namba 14 la 2024, mahakama ilimwamuru kuendelea kumhudumia mtoto huyo kwa kutumia mapato ya kodi ya nyumba kugharamia matibabu na elimu hadi atakapofikia utu uzima.

Omary pia alidai kuwa mwaka 2006 Hadija alibadili msimamo na kutangaza kuwa Juma hakuwa mtoto wake, jambo lililosababisha mtoto huyo kuhamishiwa kwa mjomba wake na baadaye shangazi yake.

Juma aliyetoa ushahidi kama shahidi wa pili wa utetezi, alikanusha kupokea fedha kutoka kwa Omary kwa ajili ya elimu, akisema alisoma shule ya Serikali ambayo haikuwa na ada.

Jaji Mwenda pia alikataa madai ya Omary kwamba alitumia Sh1.5 milioni kumlipia Hadija gharama za kujifungua, akisema hakuwasilisha ushahidi kuthibitisha fedha hizo zilitumika kwa matibabu.

Kuhusu madai ya matumizi ya fedha za kodi, Jaji alisema katika shauri la talaka mahakama iligawa nyumba kwa asilimia 50 kwa 50, hivyo mapato yake hayakuwa ya mtoto huyo pekee.

“Hata kama mdaiwa asingekuwa na sehemu ya asilimia 50 ya nyumba hiyo, jambo ambalo si kweli, mlalamikaji alishindwa kuwasilisha ushahidi wowote kuthibitisha mdaiwa alikuwa akikusanya kiasi cha Sh225,000 kwa mwezi kama ilivyodaiwa,” alisema.

Jaji pia alisema Omary hakuthibitisha hasara au madhara halisi yaliyosababishwa na mwenendo wa Hadija.

“Msongo wa mawazo pekee, bila uthibitisho, hauwezi kuwa sababu halali ya kutoa fidia ya jumla,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa kuwa Omary alijua ujauzito huo kabla ya ndoa, hakukuwa na udanganyifu uliosababisha hasara au madhara.

“Kama ilivyobainishwa kwa usahihi na mahakama, mtoto huyo alilelewa kama sehemu ya familia; hivyo, madai ya kurejeshewa gharama hayana msingi wa kisheria. Rufaa hii inakataliwa na uamuzi wa Mahakama ya Wilaya unasimama,” alisema.

Hata hivyo, kuhusu gharama za kesi, Jaji alisema kwa kuwa pande hizo bado zinashirikiana katika kulea watoto wengine, haikuwa mwafaka kumuamuru Omary kuzilipa kwa kuwa hatua hiyo isingeleta amani na maelewano katika familia ambayo imesambaratika.

DCEA yateketeza ekari 603 za bangi Morogoro

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeanza operesheni maalumu ya kuharibu mashamba ya bangi mkoani Morogoro, baada ya kubaini wakulima kuhamia maeneo ya mbali ndani na nje ya Hifadhi ya Mikumi.

Katika operesheni maalumu iliyofanyika kwa siku 14 katika vijiji vya Visengele na Lugenge wilayani Mvomero, DCEA imeteketeza ekari 603 za bangi,   kukamata magunia 49 ya bangi na watuhumiwa 13 kwa tuhuma za kujihusisha na kilimo cha dawa hizo za kulevya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatatu Agosti 17, 2026 Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo operesheni hiyo ni mwendelezo wa kampeni maalumu ya kudhibiti dawa za kulevya zinazozalishwa nchini, hususani bangi, huku akieleza kuwa mamlaka imebaini baadhi ya wakulima wamehamia maeneo ambayo hayajawahi kufikiwa na operesheni za awali.

Amesema pamoja na operesheni kufanyika katika maeneo hayo tangu mwaka 2023, bado wananchi wameendelea kulima bangi ndani ya Hifadhi ya Mikumi na maeneo ya nje ya hifadhi.

“Katika operesheni tulizozifanya safari hii tumegundua kwamba wamelima mbali zaidi ya maeneo ambayo operesheni zilishafanyika awali, wakidhani mamlaka itashindwa kufika katika maeneo hayo,” amesema Lyimo.

Lyimo amesema ukubwa wa mashamba yaliyobainika unaonyesha kuwa kilimo cha bangi bado ni changamoto katika baadhi ya maeneo ya Morogoro, hasa ndani ya hifadhi na katika vijiji vinavyozunguka maeneo ya mapori.

“Maeneo haya yako mbali sana na vijiji na makazi ya wananchi, lakini mamlaka itaweka intelijensia ya kutosha ili kuhakikisha kwamba hizi operesheni na hawa wahalifu tutaendelea kuwakamata,” amesema.

Masaji si tiba ya kila maumivu, wataalamu waonya

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameonya wananchi dhidi ya kukimbilia huduma za masaji wanapopata maumivu ya mgongo, shingo, miguu au misuli bila kwanza kufahamu chanzo cha tatizo, wakisema kufanya hivyo kunaweza kutoa nafuu ya muda huku ugonjwa ukiendelea kukua.

Wamesema baadhi ya maumivu yanayodhaniwa kuwa ya uchovu au mkazo wa misuli yanaweza kuhitaji tathmini ya kitaalamu ili kubaini chanzo na kupewa matibabu au mazoezi yanayolenga kurejesha uwezo wa mwili.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani wa Hospitali ya Medinova, Selestine Mpiri, anasema dhana inayowachanganya wananchi ni kuamini kuwa fiziotherapia na masaji ni huduma moja.

“Massage mara nyingi inalenga kutoa unafuu wa muda mfupi. Misuli ikikaza ukafanyiwa masaji utajisikia vizuri, lakini hiyo inaweza kuwa ni ya muda mfupi. Fiziotherapia inalenga kutafuta mzizi wa tatizo na kuhakikisha unafanyiwa mazoezi au utaratibu unaoweza kusaidia tatizo liondoke na lisirudi tena,” anasema.

Anasema tatizo si masaji yenyewe, bali kuitumia kama tiba ya kila aina ya maumivu bila kufanyiwa tathmini ya kitaalamu.

Kwa mfano, anasema baadhi ya wagonjwa waliowahi kufika hospitalini wakiwa na dalili zinazofanana na kiharusi, walibainika baada ya uchunguzi kuwa hawakuwa na kiharusi wala tatizo la ubongo na walisaidiwa kwa fiziotherapia.

“Nilikuwa na wagonjwa watatu vijana ambao walikuja wakiwa wamepooza upande mmoja wa uso. Baada ya kuwafanyia uchunguzi, tulibaini hawakuwa na kiharusi wala tatizo la ubongo. Walipewa fiziotherapia na wakapona,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Mpiri, fiziotherapia haiwahusu watu waliopata ajali au kufanyiwa upasuaji pekee, bali inaweza kusaidia changamoto mbalimbali zinazohusu misuli, mifupa, mishipa ya fahamu, mfumo wa upumuaji na utendaji wa mwili.

“Fiziotherapia ni kubwa zaidi ya tunavyofikiria. Kuna magonjwa ya upumuaji, kizunguzungu na matatizo ya misuli ya nyonga ambayo yanaweza kusaidiwa kwa tiba hii,” anasema.

Anasema udhaifu wa misuli ya nyonga unaweza kuhusishwa na changamoto za kudhibiti mkojo na kwamba, kwa baadhi ya watu, mazoezi maalumu yanaweza kusaidia kuimarisha misuli hiyo.

Hatari ya masaji ya nguvu

Wataalamu pia wanaonya matumizi ya nguvu kubwa wakati wa masaji, hasa kwa watu wenye maumivu ya mgongo ambayo chanzo chake hakijajulikana.

Baadhi ya watoa huduma hutumia uzito wa mwili, ikiwamo kukanyaga mgongo, kwa madai ya kumsaidia mteja kujisikia mwepesi.

Hata hivyo, wataalamu wanasema shinikizo kubwa linaweza kuwa hatari kwa mtu mwenye tatizo la mifupa, pingili za mgongo, mishipa ya fahamu au jeraha ambalo halijagundulika.

Dk Mpiri anawataka watu wenye maumivu ya muda mrefu au yanayorudia kutafuta ushauri wa kitaalamu badala ya kutegemea masaji kila wanapohisi maumivu.

Anasema hata uchovu wa mwili unaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, yakiwamo kazi nzito, kukaa au kusimama kwa muda mrefu, kukosa usingizi na mkazo wa misuli.

Hata hivyo, anasema uchovu unaodumu au unaoambatana na dalili nyingine unaweza kuhitaji uchunguzi wa kitabibu.

Akizungumza na Mwananchi mwishoni mwa juma, mtaalamu mwingine wa fiziotherapia wa Medinova, Witney Lema, anasema huduma hiyo inahusika na tiba ya utengamao na mazoezi tiba bila kutumia dawa, huku ikilenga matatizo ya misuli na mifupa pamoja na magonjwa ya mfumo wa fahamu kwa watu wazima na watoto.

“Wengi wetu tunaonekana kusumbuliwa na matatizo ya misuli na mifupa. Tunaumwa migongo, shingo, miguu na tunapata ajali. Baada ya ajali au kuvunjika mifupa, baadhi hushindwa kutembea vizuri tena. Fiziotherapia imekuja kusaidia katika changamoto hizi,” anasema.

Anasema tiba hiyo hutumia mbinu mbalimbali, ikiwamo tiba kwa mikono na vifaa vya kielektroniki, kulingana na hali ya mgonjwa.

Dk Mpiri anawataka wananchi pia kutotumia mazoezi wanayoyaona kwenye Youtube kama mbadala wa tathmini ya mtaalamu.

“Tunatakiwa tujue kwamba mazoezi, ili yafae zaidi, yanatakiwa yawe individualized (yalengwe kwako). Mtaalamu wa fiziotherapia pia atakurekebisha unapofanya mazoezi vibaya,” anasema.

Anasema mazoezi yanapaswa kuzingatia umri, ukubwa wa mwili na hali ya kiafya ya mtu, hivyo mazoezi ya mtu mwenye miaka 20 hayawezi kutumika kwa mtu wa miaka 60 bila tathmini.

Dk Imran Asif Bajwa anasema fiziotherapia huanza kwa tathmini ya mgonjwa na wakati mwingine huhitaji ushirikiano wa wataalamu mbalimbali kulingana na tatizo litakalobainika.

“Kupona kwa mgonjwa hakutegemei daktari mmoja au wawili, bali timu kubwa. Mgonjwa anaweza kuja kwa mtaalamu, lakini wakati wa assessment (tathmini) tunaweza kubaini anahitaji kumuona daktari wa mifupa. Tutafanya kazi kwa pamoja,” anasema.

Kwa nini GB 128 za simu yako zinawahi kujaa? Fanya hivi…

Dar es Salaam. Miaka iliyopita, simu yenye nafasi ya kuhifadhi taarifa ya GB32 au GB64 ilionekana kuwa na uwezo mkubwa, lakini mabadiliko ya matumizi ya simu janja yamefanya nafasi hiyo kujaa kwa haraka.

Leo, hata simu yenye GB 128 inaweza kumlazimu mtumiaji kusafisha taarifa mara kwa mara, hasa anayepiga picha nyingi, kurekodi video, kucheza michezo mikubwa au kutumia mitandao ya kijamii kwa kiwango kikubwa.

Sababu kubwa ni ongezeko la ukubwa wa picha, video na programu. Simu nyingi za kisasa zina uwezo wa kurekodi video za ubora wa juu, huku baadhi zikiruhusu kurekodi video zenye ubora wa hali ya juu unaofikia (4K) na hata viwango vya juu zaidi kulingana na aina ya kifaa.

Kwa mujibu wa Apple Support, kwa mfano, inaonyesha kuwa baadhi ya iPhone zinaweza kurekodi video ya 4K na kwamba teknolojia ya ProRes inaweza kutumia nafasi kubwa ya kuhifadhi, kiasi kwamba baadhi ya uwezo wa kurekodi hutegemea ukubwa wa uhifadhi ‘storage’ wa simu.

WhatsApp nayo inakula nafasi

Kwa watumiaji wengi, si kamera pekee inayojaza storage. Programu za mawasiliano kama WhatsApp zinaweza kuhifadhi kwa muda mrefu picha, video, nyaraka, sauti na faili nyingine zinazotumwa kwenye makundi na mazungumzo binafsi.

Tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi kwa mtu aliye kwenye makundi mengi yanayotuma video na picha kila siku ambapo itakulazimu uzime auto-download.

Kwa upande wa Android, Google inashauri watumiaji kuingia sehemu ya Settings > Storage ili kuona ni aina gani ya faili au programu zinazotumia nafasi kubwa na kuanza kuziondoa zisizo muhimu.

Google pia inaeleza kuwa (backup) za WhatsApp kwenye Android sasa zinahesabiwa katika nafasi ya kuhifadhi ya akaunti ya Google, huku video zikiwa miongoni mwa vitu vinavyoweza kuongeza ukubwa kwa haraka.

GB 128 haimaanishi nafasi yote ipo wazi

Jambo jingine ambalo mtumiaji anapaswa kulifahamu ni kwamba namba iliyoandikwa kwenye boksi, kama GB 128, si lazima iwe nafasi yote atakayoiona akiwa anaanza kutumia simu.

Sehemu ya nafasi hiyo hutumika na mfumo wa uendeshaji, programu zilizokuja na simu na mafaili mengine ya mfumo. Kadri mtumiaji anavyoongeza programu na taarifa zake nafasi iliyobaki hupungua.

Hivyo, mtu anayenunua simu ya GB 128 kwa sababu anaona ina nafasi kubwa anapaswa kujiuliza pia ataitumia kwa shughuli gani.

Njia rahisi ni kuanza kwa kuangalia sehemu ya Storage kwenye simu ili kubaini kinachotumia nafasi kubwa.

Picha na video muhimu zinaweza kuhifadhiwa kwenye huduma za cloud au kuhamishiwa kwenye kompyuta au kifaa kingine cha kuhifadhi. Google, kwa mfano, inaruhusu watumiaji wa Android kusimamia nafasi kwa kuondoa picha na video ambazo tayari zimehifadhiwa kwenye Google photos, pamoja na faili zilizopakuliwa na programu ambazo hazitumiki.

Google Help, pia kuna simu za Android zinazoweza ku-archive programu zisizotumiwa mara kwa mara, badala ya kuzifuta kabisa. Google inaeleza kuwa hatua hiyo inaweza kuondoa sehemu ya programu inayotumia nafasi huku taarifa na ikoni yake vikibaki ili iweze kurejeshwa baadaye.

Kwa mtumiaji anayefanya matumizi ya kawaida kama kupiga picha chache, kutumia WhatsApp, mitandao ya kijamii, kusoma habari na kupiga simu, GB 128 inaweza kutosha ikiwa atasimamia vizuri taarifa zake.

Lakini kwa mpiga picha, mtengeneza maudhui, mcheza michezo mikubwa au mtu anayerekodi video nyingi, GB 256 au zaidi inaweza kuwa chaguo lenye nafasi kubwa zaidi ya matumizi ya muda mrefu.

Kabla ya kununua simu, si muhimu kuangalia storage pekee. Mnunuzi anapaswa pia kuangalia aina ya kamera, ubora wa video, ukubwa wa programu anazotumia, kama kifaa kinaunga mkono memory card na kama kina uwezo wa kutumia huduma za cloud.

Kwa kifupi, GB 128 si ndogo moja kwa moja, lakini inaweza kuwa ndogo kulingana na matumizi ya mwenye simu. Kadri simu inavyotumika kama kamera, ofisi, burudani na kituo cha kuhifadhi mafaili, ndivyo nafasi kubwa ya kuhifadhi inavyokuwa muhimu zaidi.

Asimulia alivyojifungua katikati ya tetemeko la ardhi

Dar es Salaam. Maria Florida, 39, ameeleza furaha yake baada ya kujifungua salama mtoto wake wa nne kwa njia ya upasuaji, huku tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.7 likitikisa eneo la Nusa Tenggara Mashariki mwa Indonesia.

Florida alikuwa tayari ameshaanza kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Nagekeo wakati tetemeko hilo lilipoanza. Hata hivyo, madaktari waliendelea na huduma huo licha ya mazingira magumu yaliyosababishwa na mtikisiko huo.

Tetemeko hilo lilisababisha kukatika kwa umeme hospitalini hapo, hivyo madaktari walilazimika kutumia mwanga wa tochi kuendelea na upasuaji hadi kufanikisha kumleta duniani mtoto huyo.

Baada ya kujifungua mtoto wa kike, Florida alimpa jina Gempita Soli Wona,   linalohusishwa na neno la Kiindonesia linalomaanisha tetemeko la ardhi.

Mtoto huyo alizaliwa akiwa na uzito wa kilo 1.3 na kwa mujibu wa taarifa za madaktari afya yake inaendelea kuimarika.

Tetemeko hilo lilitokea Agosti 15, 2026 na kuleta madhara makubwa mashariki mwa Indonesia, likisababisha vifo vya watu wasiopungua 54, majeruhi zaidi ya 130 na kuwalazimisha maelfu ya wakazi kuondoka katika maeneo yaliyoathirika.

Kutokana na mitikisiko kuendelea na baadhi ya miundombinu ya hospitali kuathirika, mtoto huyo amewekwa katika mashine maalumu ya kuhifadhi joto iliyowekwa nje ya jengo la hospitali.

Florida amewashukuru madaktari kwa kujitoa na kuendelea na upasuaji huo licha ya hatari iliyokuwapo.

Wakati tukio hilo likitoa simulizi ya matumaini, idadi ya watu waliofariki kutokana na tetemeko hilo imefikia 53, huku shughuli za uokoaji zikiendelea katika maeneo yaliyoathirika.

Waokoaji wamefanikiwa kupata miili mingine sita, hali iliyoongeza idadi ya vifo kutoka 47 hadi 53.

Zaidi ya watu 135 wameripotiwa kujeruhiwa, huku nyumba zaidi ya 900 zikiharibiwa na maelfu ya watu kulazimika kuondoka katika makazi yao kutokana na hofu ya mitetemeko zaidi.

Takriban watu 5,000 wamehama makazi yao na kuhamia maeneo salama likiwa la  Kisiwa cha Flores.

Tetemeko hilo pia limesababisha maporomoko ya ardhi na kuziba baadhi ya barabara, hali iliyowapa changamoto waokoaji kuwafikia watu waliokwama katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Kukatika kwa umeme na mawasiliano kumeongeza ugumu wa shughuli za uokoaji, huku mamlaka zikiendelea kuratibu juhudi za kuwafikia waathirika na kutoa msaada wa dharura.

Misaada inayotolewa inajumuisha chakula, mahema na mahitaji mengine muhimu kwa watu walioathirika.

Jose Chameleone alivyoibua shangwe akitumbuiza kilele tamasha la Kizimkazi

Unguja. Msaanii wa kimataifa kutoka Uganda, Jose Chameleone ameibua shangwe wakati akitumbuiza katika kilele cha tamasha la Kizimkazi.

Katika tamasha hilo linalofanyika leo Agosti 14, 2026 viwanja vya Mwehe Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, msanii huyo amepata fursa kutumbuiza nyimbo zake mbili, Jamila na Mama Mia.

Katika kibao chake cha Jamila, alishuka kutoka katika jukwaa la burudani na kusogelea meza kuu walipokaa viongozi wakuu wa kitaifa kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Baada ya kufika katika jukwaa hilo, Rais Samia Suluhu Hassan alishuka kutoka kwenye kiti chake alipokuwa amekaa na kuongea na msanii huyo kisha kucheza naye wimbo huo wa mbona umeniacha.

Baada ya hapo aliondoka huku akiibua shwangwe kubwa kwa wananchi na viongozi waliofurika katika viwanja hivyo kwa ajili ya kusherehekea sherehe hizo.

Katika tamasha hilo pia wasanii wengine wa ndani na nje ya Tanzania wamepata fursa ya kutumbuiza.

Miongoni mwa wasanii hao ni Mrisho Mpoto, Sholo Mwamba, kikundi cha ngoma kutoka Dodoma cha Mahenza na ngoma ya asili ya Kizimkazi ya Shomoo.