Mmiliki wa Leeds na Rangers Afungwa Baada ya Kukamatwa Katika Operesheni ya Ukahaba

Ohio, Marekani — Mmoja wa wamiliki wa klabu za Leeds United na Rangers, Jed York, amehukumiwa kifungo cha siku moja gerezani nchini Marekani baada ya kukamatwa katika operesheni ya polisi iliyohusisha tuhuma za ukahaba.

York, ambaye pia ni mmiliki mkuu wa timu ya NFL ya San Francisco 49ers, alikamatwa Jumapili, Agosti 23, katika eneo la East Palestine, Ohio, wakati wa operesheni iliyofanywa na polisi kwa kushirikiana na Mahoning Valley Human Trafficking Task Force.

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, York alidaiwa kujibu tangazo la siri lililowekwa mtandaoni na maafisa waliokuwa wakifanya uchunguzi. Inadaiwa alipanga kulipa dola 140 kwa ajili ya kufanya tendo la ngono.

Awali, York alishtakiwa kwa kosa la kujihusisha na ukahaba. Hata hivyo, waendesha mashtaka baadaye walibadilisha shtaka hilo na kuwa tabia isiyo na nidhamu (disorderly conduct). Pia alishtakiwa kwa kumiliki chombo kilichotumika katika kutenda kosa, huku simu yake ikitajwa kuwa ilitumika kuwasiliana na tangazo hilo.

York alikubali no contest katika mahakama ya Ohio, hatua ambayo si kukiri rasmi hatia, lakini inamruhusu mahakama kutoa hukumu.

Mahakama ilimhukumu kifungo cha siku moja kwa kila kosa, huku vifungo hivyo vikienda kwa wakati mmoja. Muda aliokuwa tayari ameshikiliwa ulihesabiwa kama sehemu ya adhabu hiyo.

Mbali na kifungo hicho, York alitozwa faini ya dola 1,150. Pia alitakiwa kukamilisha kozi ya mtandaoni, huku dola 160 zikielekezwa kwa Mahoning Valley Human Trafficking Task Force.

Baada ya kukamatwa, York aliachiliwa kwa dhamana ya dola 5,000 kabla ya kurejea mahakamani kukamilisha mchakato wa kesi.

Tukio hilo limeibua maswali kuhusu mustakabali wa York katika michezo, hasa kutokana na nafasi yake kama mmiliki wa timu ya San Francisco 49ers. NFL imesema inalifahamu suala hilo na italipitia kwa kuzingatia sera yake ya mwenendo binafsi inayowahusu pia wamiliki wa timu.

Katika soka la Uingereza na Scotland, York ni sehemu ya umiliki wa Leeds United na Rangers kupitia maslahi yanayohusishwa na 49ers Enterprises. Hadi sasa, klabu hizo hazijatoa kauli ya kina kuhusu tukio hilo.

Hata hivyo, York hakuhukumiwa kwa shtaka la ukahaba lenyewe baada ya shtaka hilo kubadilishwa. Alikubali mashtaka mawili madogo, akahukumiwa kifungo cha siku moja kilichohesabiwa kama muda aliokuwa tayari ameshikiliwa, na kutozwa faini ya dola 1,150.

Stori na Erick Elibariki | GPL – TUDACO

*WAZIRI MKUU AWATAKA WATANZANIA KUIMARISHA MALEZI, KULINDA AMANI NA KUTIMIZA WAJIBU*

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Watanzania kuendelea kuimarisha malezi ya watoto na vijana, kulinda amani, kuheshimu tofauti na kutimiza wajibu wao kwa taifa, akisisitiza kuwa haki na wajibu haviwezi kutenganishwa.

Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo Jumanne, Agosti 25, 2026, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Baraza la Maulid la Kitaifa lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Akiwasilisha salamu za Rais, Waziri Mkuu amesema maadhimisho hayo yanapaswa kuwa fursa ya kutafakari, kujifunza na kuyaishi kwa vitendo maisha na mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW), yakiwemo wema, huruma, upendo na kusaidiana, huku akiwataka Watanzania kuendelea kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika masuala ya maendeleo na malezi, huku akisisitiza umuhimu wa wazazi, jamii na viongozi wa dini kuongeza uangalizi kwa watoto na vijana ili kuwalinda dhidi ya mmomonyoko wa maadili na athari za matumizi mabaya ya teknolojia na mitandao ya kijamii. Amesema pamoja na juhudi zilizofanyika kwa miaka mingi katika kuimarisha malezi na ulinzi wa mtoto wa kike, mazingira ya sasa yanahitaji pia kuimarishwa kwa malezi na ulinzi wa mtoto wa kiume.

“Kwa mazingira ya sasa, naweza kudiriki hata kusema kwamba kwa mazingira ya sasa, mtoto wa kiume yuko kwenye mazingira ya hatari zaidi. Kwa hiyo, tuongeze malezi bila kubagua kwamba tumlee zaidi yupi. Wote sasa hivi watoto wako katika mazingira ya hatari.”

Aidha, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji kuendelea kuwepo kwa utawala bora, amani, usalama na utulivu, akisisitiza kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda haki za wengine na kutunza amani ya nchi.

“Na ili tufike hapo, tuendelee kumuombea Rais wetu na tuendelee kuiombea nchi yetu ili tuendelee kuwa na amani na tuendelee kuwa na uimara kama ambavyo taifa letu limeshuhudia kwa kipindi kirefu.”

Kuhusu amani na utulivu, Waziri Mkuu amesema Tanzania inaendelea kuheshimu haki na uhuru wa wananchi, ikiwemo uhuru wa kuabudu na kushiriki katika masuala ya kisiasa, lakini akasisitiza kuwa uhuru huo lazima uende sambamba na kutimiza wajibu na kuheshimu haki za wengine.

“Haki na wajibu inaenda pamoja kwamba unapotaka kupokea kwa mikono miwili haki unayostahili, haki yako hiyo isivunje haki ya wengine. Na hapo ndipo ambapo Katiba yetu imeweka wajibu.”

Ametoa wito kwa viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa na wananchi kwa ujumla kuendelea kujenga utamaduni wa kuheshimu tofauti na kuepuka lugha za chuki na uchochezi, akisisitiza kuwa migogoro ya ndani ya jamii na kuvuruga amani ya Taifa havina mshindi.

“Migogoro ya sisi kwa sisi ya wenyewe kwa wenyewe ni migogoro isiyo na mshindi. Kuvunja amani katika taifa hapana mshindi. Hapana mshindi. Hakuna anayeshinda. Kuvuruga taifa hamna mshindi. Hakuna anayeshinda.”

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeiry bin Ally, amewataka viongozi waliochaguliwa katika ngazi mbalimbali za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kufanya kazi kwa bidii na uadilifu, kwa kuzingatia mafundisho ya dini pamoja na miongozo na taratibu za taasisi, akiwataka kusimamia haki, maadili na kutoa mwongozo sahihi kwa jamii.

“Kinachotakiwa kwenu nyinyi ni kufanya kazi. Sio hadithi na maneno, ni kufanya kazi kama ambavyo Mungu ametuambia hapa. Fanyeni kazi. Na fanyeni kazi kwa kusimamia haki na maadili na kutoa mwongozo katika jamii ili jamii ipate kutengenea.”

Mufti pia amesisitiza umuhimu wa Waislamu kuendelea kuishi kwa amani, upendo na kusaidiana, huku akihimiza kuimarishwa kwa malezi ya watoto na vijana ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili, matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vya ukatili.

“Muislamu wa kweli ni yule ambaye watu wako salama kutokana na ulimi wake na mkono wake, na muumini wa kweli ni yule watu wanaomwamini kwa damu zao na mali zao.”

Waziri Mkuu amewapongeza Waislamu wote kwa Maadhimisho ya Maulid na kuwatakia heri, baraka na fanaka, huku akisisitiza kuwa Watanzania wa dini mbalimbali wanapaswa kuendelea kuishi kwa upendo, kuheshimiana na kuilinda amani na mshikamano wa taifa.

RAIS SAMIA ARIDHIA OMBI LA DKT. NCHIMBI KUJIUZULU

NA MATUKIO DAIMA MEDIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokea rasmi barua ya ombi la kujiuzulu kwa Makamu wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, na kuridhia ombi hilo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo, Agosti 25, 2026, na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Nchimbi ameomba kujiuzulu katika nafasi hiyo kuanzia Septemba 4, 2026.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Rais Samia ameridhia ombi hilo na kwamba taratibu za kikatiba za kumpata Makamu wa Rais mwingine zitachukuliwa.

Taarifa hiyo imesainiwa na Balozi Dkt. Moses M. Kusiluka, Katibu Mkuu Kiongozi.

Ikulu Yathibitisha Dkt. Nchimbi kujiuzulu Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Global Publishers
August 25, 2026
0 views
0 Comments

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokea na kuridhia ombi la kujiuzulu kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kuanzia tarehe 4 Septemba 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi leo, Agosti 25, 2026, Rais Samia amekubali ombi hilo la Nchimbi la kujiuzulu nafasi hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa taratibu za kikatiba za kumpata Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwingine zitachukuliwa.

Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses M. Kusiluka, tarehe 25 Agosti 2026.

Dk Kiruswa achangia Sh milioni 6 ujenzi darasa la awali – HabariLeo

ARUSHA: Juhudi za wananchi wa Kitongoji cha Lailupa, Kijiji cha Meirugoi, Kata ya Gelai-Meirugoi wilayani Longido mkoani Arusha, za kujitolea kujenga darasa la shule ya awali (chekechea) lenye thamani ya Sh milioni 12, zimemgusa Mbunge wa Jimbo hilo, Dk Steven Kiruswa, ambaye ameamua kugharamia hatua ya mwisho ya ukamilishaji wa jengo hilo kwa Sh milioni 6 kutoka kwenye fedha zake binafsi.

Wananchi hao walimweleza Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini, wakati akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika kata hiyo, ambapo walimsimamisha na kumueleza changamoto ya watoto wao kusoma chini ya mti bila kujali mvua au jua.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Lailupa, Ndung’anak Mepukor, alisema jitihada za akina mama, vijana pamoja na viongozi wa mila maarufu kama Laigwanani, ziliwezesha kumshawishi Mbunge huyo kufika eneo hilo na kujionea hali halisi ya mazingira ambayo watoto walikuwa wakipata elimu.

Alisema baada ya kufika eneo hilo, Kiruswa aliona wananchi walikuwa wamefanya sehemu kubwa ya kazi, lakini ujenzi ulikuwa haujakamilika kutokana na kukosekana kwa mlango mmoja, madirisha sita, mabati 60, madawati 20, mbao pamoja na hatua za upigaji plasta.

“Wananchi tulijitahidi kwa nguvu zetu wenyewe, kila kaya ilitoa mchango wa fedha, wengine waliuza mifugo na wengine walishiriki katika uchimbaji wa msingi, ujenzi na kubeba matofali ili watoto wetu wapate sehemu salama ya kusomea,” alisema Mepukor.

Alisema baada ya kuona jitihada hizo na changamoto ya watoto kusoma chini ya mti, Mbunge Kiruswa aliamua kubeba gharama za kukamilisha ujenzi huo kwa Sh milioni 6.

Akizungumza baada ya kutoa ahadi hiyo, Kiruswa aliwapongeza wananchi wa Lailupa kwa moyo wa kujitolea na kusema hatua hiyo imempa faraja kubwa kwa kuona jamii ikishiriki katika kuboresha elimu.

Alisema ameamua kuchangia kukamilika kwa darasa hilo ili kuwawezesha watoto kusoma karibu na makazi yao na kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu.

Kiruswa alisema suala la kuhakikisha watoto wanapata elimu bora ni jukumu la kila mwananchi, huku akieleza kuwa juhudi za wananchi zinapaswa kuungwa mkono na serikali pamoja na viongozi wao.

Aidha, alisema atahakikisha shule hiyo ya awali inasajiliwa na kupata mwalimu mwenye sifa, kwani kwa sasa inategemea mwalimu wa kujitolea ambaye hana sifa rasmi za ualimu.

“Lengo langu ni kuhakikisha ifikapo Januari mwakani shule hii inakuwa imesajiliwa, inatambulika na serikali na watoto wanafundishwa na mwalimu mwenye sifa,” alisema.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Gelai-Meirugoi, Daniel Nasinda, alisema watoto wa Kitongoji cha Lailupa walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita 10 kwenda na kurudi kutafuta elimu, hali iliyokuwa hatarishi kutokana na uwepo wa wanyama wakali katika eneo hilo.

Alisema uamuzi wa wananchi kujenga darasa hilo umeleta matumaini mapya kwa watoto na wazazi, kwani sasa watapata mazingira salama ya kujifunzia karibu na makazi yao.

Rais Samia Awatakia Waislamu Kheri katika Maadhimisho ya Maulid

Global Publishers
August 25, 2026
48 views
0 Comments

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewatakia Waislamu na Watanzania wote kheri na baraka katika Maadhimisho ya Sikukuu ya Maulid.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rais Samia amesema Maulid inapaswa kuwa ukumbusho wa kuendelea kuishi kwa upendo, huruma, uvumilivu na kuwajali wengine katika jamii.

Amesisitiza umuhimu wa Watanzania kusherehekea Maulid kwa amani na furaha, huku wakidumisha umoja na mshikamano unaoendelea kuijenga Tanzania.

Rais Samia pia amemuomba Mwenyezi Mungu kuendelea kuibariki Tanzania, kuitunza katika amani na utulivu, pamoja na kuwawezesha wananchi kuijenga nchi kwa maendeleo na ustawi wa wote.

“Tusherehekee kwa amani na furaha huku tukidumisha umoja na mshikamano wetu. Mwenyezi Mungu Mtukufu aendelee kuibariki nchi yetu, kuitunza katika amani na utulivu, na kutuwezesha kuijenga kwa maendeleo na ustawi wa wote,” amesema Rais Samia.

Dk Nchimbi Atangaza Kujiuzulu Umakamu wa Rais na Kustaafu Siasa

Global Publishers
August 25, 2026
828 views
0 Comments

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel John Nchimbi, ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo na kustaafu siasa pamoja na utumishi wa umma.

Dk Nchimbi ametoa taarifa hiyo leo Jumanne, Agosti 25, 2026, akisema amemwandikia Rais Samia Suluhu Hassan barua ya kumjulisha kuhusu uamuzi wake wa kujiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais, kuanzia Septemba 4, 2026.

Katika taarifa yake, Dk Nchimbi amesema uamuzi huo umetokana na ahadi aliyompa Rais Samia wakati alipoteuliwa kushika nafasi hiyo, kwamba angeendelea kumsaidia katika majukumu yake kwa uaminifu na uwezo wake wote, na angeachia nafasi hiyo iwapo angehisi Rais anahitaji mabadiliko.

“Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa Mhe. Rais anatamani mabadiliko, hivyo nimeamua kutimiza ahadi yangu,” amesema Dk Nchimbi katika taarifa yake.

Aidha, amemshukuru Rais Samia pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa imani waliyoonyesha kwake, huku akiwashukuru Watanzania kwa ushirikiano na kumuunga mkono katika kipindi chake cha utumishi.

Dk Nchimbi amesisitiza kuwa licha ya kustaafu siasa na utumishi wa umma, ataendelea kuwa raia mwema na kulitumikia taifa katika nafasi nyingine.

Kujiuzulu kwake kunakuja ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu alipoanza kushika nafasi ya Makamu wa Rais, na endapo uamuzi huo utaidhinishwa, hatua hiyo itakuwa miongoni mwa matukio ya kipekee katika historia ya uongozi wa Tanzania.

Video: Simanzi Kihesa, Mrembo wa Miaka 23 Afariki Ndani ya Chumba Chake

Global Publishers
August 25, 2026
48 views
0 Comments


Mkazi wa Mtaa wa Kihesa, Halmashauri ya Mji wa Njombe, Edina Chaula, mwenye umri wa miaka 23, amefariki dunia baada ya kudaiwa kupata tatizo la kupaliwa na chakula akiwa ndani ya chumba chake.

Tukio hilo liliripotiwa Agosti 23, 2026, katika Mtaa wa Kihesa, mkoani Njombe.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi Mahamoud Banga, Edina alikutwa amefariki dunia ndani ya chumba chake baada ya kupata tatizo la kupaliwa na chakula.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa chakula hicho kilidaiwa kuziba njia yake ya hewa na kusababisha hali ya dharura iliyosababisha kifo chake.

Tukio hilo limeacha simanzi kwa ndugu, jamaa na wakazi wa eneo hilo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linaendelea na taratibu za uchunguzi ili kubaini kwa undani mazingira ya tukio hilo na kuthibitisha chanzo cha kifo.

Tukio hilo linakumbusha umuhimu wa kuchukua tahadhari wakati wa kula na kutoa msaada wa haraka kwa mtu anayepaliwa, kwani kuziba kwa njia ya hewa ni hali ya dharura inayoweza kuhatarisha maisha.

Marekani Yaiondoa Syria Kwenye Orodha ya Wafadhili wa Ugaidi

WASHINGTON — Marekani imeiondoa rasmi Syria kwenye orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi, hatua inayowakilisha mabadiliko makubwa katika sera ya Washington kuelekea taifa hilo la Mashariki ya Kati.

Syria iliwekwa kwenye orodha hiyo mwaka 1979, na kwa miongo kadhaa hatua hiyo iliambatana na vikwazo mbalimbali vya kiuchumi, kifedha na kibiashara.

Uamuzi huo unakuja wakati serikali mpya ya Syria chini ya Rais Ahmed al-Sharaa ikijaribu kujenga upya uhusiano wa nchi hiyo na mataifa ya Magharibi baada ya miaka ya vita na migogoro.

Washington imeeleza kuwa mabadiliko katika uongozi na sera za Damascus, pamoja na hatua za kupambana na ugaidi, yamekuwa miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa katika kubadili msimamo wake.

Kuondolewa kwa Syria kwenye orodha hiyo kunaweza kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa nchi hiyo, ikiwamo kuvutia uwekezaji wa kimataifa, kuimarisha biashara na kurahisisha baadhi ya miamala ya kifedha. Hata hivyo, hatua hiyo haimaanishi kwamba vikwazo vyote vinavyolenga Syria na watu au taasisi maalumu vimeondolewa.

Kwa mujibu wa taarifa za serikali ya Marekani, Syria imekuwa ikikabiliwa na vikwazo mbalimbali tofauti na uteuzi wake kama nchi inayofadhili ugaidi. Baadhi ya hatua hizo zililenga mali za maafisa na watu waliotuhumiwa kuhusika na ukiukaji wa haki za binadamu au shughuli nyingine zilizolengwa na Marekani.

Hatua hiyo pia inakuja sambamba na mabadiliko katika mtazamo wa Marekani kuhusu Hay’at Tahrir al-Sham (HTS), kundi lililokuwa likihusishwa na al-Qaeda na ambalo liliwekwa kwenye orodha ya mashirika ya kigaidi ya Marekani mwaka 2014.

Kwa ujumla, uamuzi wa Washington unaashiria kuondoka taratibu kwenye sera ya muda mrefu ya kuitenga Syria na kuelekea katika ushirikiano unaolenga usalama, utulivu wa kisiasa na ujenzi wa uchumi wa nchi hiyo.

Hata hivyo, Marekani bado inatoa tahadhari kali kuhusu usalama nchini Syria kutokana na vitisho vya ugaidi, utekaji nyara, machafuko na mapigano katika baadhi ya maeneo.

Kwa Syria, kuondolewa kwenye orodha hiyo kunaweza kuwa hatua muhimu katika juhudi za kuirejesha nchi hiyo kwenye mfumo wa uchumi wa kimataifa. Kwa Marekani, ni ishara kwamba sera yake kuelekea Damascus imeanza kubadilika kwa kiwango kikubwa baada ya zaidi ya miongo minne ya Syria kuwa chini ya hadhi ya nchi inayofadhili ugaidi.

Stori Na Erick Elibariki | GPL -TUDACO

BREAKING..DKT NCHIMBI AJIUZULU SIASA NA UTUMISHI WA UMMA

Makamu wa Rais Dr Emmanuel John Nchimbi amemwandikia barua Rais wa JMT kuwa ameamua kustaafu siasa na utumishi wa Umma hivyo ni sahihi kusema amejiuzulu nafasi yake ya Umakamu wa Rais kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri.

Taarifa imechapishwa kwenye ukurasa wake rasmi ila bado kurasa rasmi za Ofisi ya Makamu wa Rais hazijapandisha taarifa hiyo.