Inashangaza! Simba Yashinda, Lakini Mashabiki Watoa Lawama Kwa Doumbia – Video

Global Publishers
August 28, 2026
78 views
0 Comments


Baadhi ya mashabiki wa Simba wameonekana kutoridhishwa na kiwango cha mshambuliaji wa klabu hiyo, Ibrahim Doumbia, licha ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union FC.

Mchezo huo umechezwa katika Uwanja wa Isamuyo, ambapo shabiki wa Simba, wametoa maoni yao kuhusu kiwango cha Doumbia wakati akizungumza na mtangazaji wetu Official Diana, mara baada ya mchezo kumalizika.

Watu Wawili Wafariki Baada ya Kujinyonga Dagailoi, Babati – Video

Global Publishers
August 28, 2026
6 views
0 Comments

Watu wawili, wakazi wa Kijiji cha Dagailoi, Kata ya Sigino, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti baada ya kujinyonga.

Tukio la kwanza lilitokea Agosti 22, 2026, ambapo mwanaume aliyefahamika kwa jina la Petro Moya anadaiwa kujinyonga baada ya kutokea mvutano kuhusu bili ya maji ya Shilingi 6,000 kati yake na mama yake mzazi.

Inadaiwa kuwa Petro alipewa fedha hizo na mama yake kwa ajili ya kulipia bili ya maji, lakini alizitumia kwa shughuli nyingine. Baada ya mama yake kumdai fedha hizo, Petro alichukua uamuzi wa kujinyonga.

Tukio la pili limetokea asubuhi ya leo, Agosti 27, 2026, ambapo mwanaume mwingine aliyefahamika kwa jina la Mohamed Abdilai amefariki dunia baada ya kujinyonga.

Inadaiwa kuwa Mohamed alichukua uamuzi huo baada ya baba yake mzazi kumtaka arejee nyumbani, kufuatia kushindwa kulipa kodi ya nyumba ya Shilingi 10,000.

Mwandishi wa Global TV, Hosea El Nino, amefika katika Kitongoji cha Dagailoi kufuatilia undani wa matukio hayo.

TANESCO NA MAHAKAMA NYANDA ZA JUU KUSINI ZAIMARISHA MAHUSIANO KULINDA MIUNDOMBINU YA UMEME

Dodoma

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeeleza umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa karibu na Mahakama katika kushughulikia changamoto zinazohusu miundombinu ya umeme, ikiwemo matukio ya uharibifu na hujuma dhidi ya miundombinu hiyo.

Akizungumza Agosti 27, 2026, baada ya watumishi wa Idara ya Mahakama, akiwemo Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Wasajili, Mahakimu, Watendaji na wafanyakazi wengine kufanya ziara katika Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera kwa lengo la kujifunza namna umeme unavyozalishwa, kusafirishwa na kusambazwa kwa wananchi, Meneja wa Huduma za Usalama wa TANESCO, Bw. Lenin Kiobya, amesema ziara hiyo imewapa watumishi hao uelewa wa namna Shirika linavyotekeleza majukumu yake, kuanzia uzalishaji, usafirishaji hadi usambazaji wa umeme kwa wananchi.

Amebainisha kuwa uelewa huo ni muhimu kwa Mahakama katika utekelezaji wa majukumu yake ya kutafsiri na kusimamia sheria, hususan inaposhughulikia kesi zinazohusiana na miundombinu ya umeme, ili masuala yanayogusa maslahi ya taifa yaweze kupewa uzito unaostahili.

Aidha, amesema kuwa TANESCO itaendelea kujenga ushirikiano na Mahakama katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwenye miundombinu yake, hatua inayolenga kusaidia kupunguza uhalifu na hujuma zinazoweza kuathiri huduma ya umeme nchini.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Fahamu Mtulya, amesema ziara hiyo katika Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera imewasaidia Majaji na Mahakimu kuelewa kwa kina umuhimu wa kulinda miundombinu yenye maslahi ya kitaifa, ikiwemo miundombinu ya TANESCO.

Amesema kuwa wamebaini kuwa ucheleweshaji wa mashauri yanayohusiana na uwekezaji na miundombinu ya TANESCO unaweza kuwa na gharama kubwa, hivyo wamekubaliana kuyapa kipaumbele mashauri yanayohusu miundombinu hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Pia, amebainisha kuwa uharibifu wa miundombinu yenye maslahi ya kitaifa, ikiwemo miundombinu ya umeme na reli, huhusisha makosa ya uhujumu uchumi yenye adhabu kali, huku akisisitiza umuhimu wa wadau wa sheria, ikiwemo Bunge, kushirikiana kubaini na kuziba mianya ya kisheria inayoweza kujitokeza.

Aidha, amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya taasisi za umma, ikiwemo ya TANESCO, akieleza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda mali za taifa. Amesema Mahakama pia itatumia Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme.

Naye, Kaimu Meneja wa Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera, Mhandisi William Modest, amesema kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha megawati 80 kupitia mashine mbili, kila moja ikiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 40. Umeme huo huingizwa kwenye gridi ya taifa kwa matumizi ya wananchi na shughuli za kiuchumi.

Aidha, ametoa wito kwa Majaji kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji na madhara ya kilimo holela kinachoweza kuzuia mtiririko wa maji kuelekea Bwawa la Mtera.

Amebainisha kuwa Kituo cha Mtera kina umuhimu mkubwa katika upatikanaji wa umeme nchini, huku kikihudumia zaidi ya vijiji 12. Bwawa la Mtera pia lina umuhimu katika shughuli za uvuvi na kilimo, huku Mto Ruaha ukitoa maji kwa skimu mbalimbali za kilimo katika Nyanda za Juu Kusini.

 

Maganya: Jumuiya ya Wazazi Yaunga Mkono Nchimbi Kuvuliwa Uanachama – Video

Global Publishers
August 28, 2026
0 views
0 Comments

Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Maganya, amesema jumuiya hiyo inaunga mkono uamuzi wa kumvua uanachama wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Maganya ameyasema hayo Agosti 27, 2026, akiwa Misungwi, mkoani Mwanza, wakati wa ufunguzi wa sherehe za Wiki ya Wazazi Kitaifa.

Amesema msimamo huo unatokana na hatua zilizochukuliwa na chama dhidi ya Dkt. Nchimbi, huku akisisitiza umuhimu wa wanachama kuheshimu katiba, kanuni na maamuzi ya chama.

Baada ya Kimya, Mwijaku Amtaka Maua Sama Aachie Muziki Mpya

Mjadala kuhusu kurejea kwa msanii wa Bongo Fleva, Maua Sama, katika muziki umeibuka upya baada ya mwanahabari na mchambuzi wa burudani Mwijaku kumtaka msanii huyo kuanza kutoa kazi mpya.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram leo, Agosti 27, 2026, Mwijaku ametoa ujumbe mfupi lakini wenye uzito kwa Maua Sama, akisisitiza kuwa mashabiki wake bado wanahitaji kusikia muziki mpya kutoka kwake.

“Tunataka nyimbo mpya,” aliandika Mwijaku.

Kauli hiyo imeibua hisia mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya mashabiki wakionyesha hamu ya kumuona Maua Sama akirejea studio na kuendelea na safari yake ya muziki.

Maua Sama ni miongoni mwa wasanii wa kike waliowahi kufanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva na Afro-Pop nchini Tanzania.

Alijenga jina kupitia nyimbo mbalimbali zilizopokelewa na mashabiki, ikiwemo “Iokote”, ambayo ilichangia kuongeza umaarufu wake katika tasnia ya muziki.

Kwa kipindi cha hivi karibuni, mashabiki wamekuwa wakisubiri kusikia kazi mpya kutoka kwa msanii huyo, huku maisha yake binafsi yakionekana kuchukua sehemu kubwa ya muda wake.

Ujumbe wa Mwijaku umeongeza matarajio kwa mashabiki wanaotamani kumuona Maua Sama akirudi kwenye muziki.

Kwa kuwa tayari ana historia na msingi wa mashabiki katika tasnia hiyo, kurejea kwake kwa kazi mpya kunaweza kuongeza ushindani katika muziki wa kike na kutoa hamasa mpya kwa mashabiki wa Bongo Fleva.

Kwa sasa, bado haijafahamika iwapo Maua Sama amepanga kutoa kazi mpya, lakini ujumbe wa Mwijaku umeweka wazi jambo moja mashabiki bado wanaisubiri sauti yake.

Stori na Nasra Kassim | GPL -TUDACO

SERIKALI YAZINDUA ‘UGHAIBUNI LOAN’ – Matukio Daima Habari

✅Kuwezesha vijana kumudu mahitaji ya msingi anapoenda kufanya kazi nje ya nchi

Serikali imesema itaendelea kuhakikisha vijana nchini wanaendelea kunufaika na fursa za nje ya nchi na zenye staha kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Agosti 27,2026 wakati wa uzinduzi wa mkopo wa Ughaibuni Loan unaoratibiwa na Benki ya CRDB pamoja na kuwaaga vijana 130 kati ya 530 wanaotarajia kwenda kufanya kazi nje ya nchi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi amesema Serikali inatambua ajira za nje ya nchi kama nyenzo muhimu ya kupanua fursa za ajira, kuongeza kipato cha vijana, kukuza ujuzi na kuwajengea uzoefu wa kimataifa.

“Matokeo ya jitihada hizi yamewezesha Watanzania 14,613 kupata ajira nje ya nchi tangu Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani. Kati ya Julai 2025 hadi sasa, Watanzania 8,428 wameunganishwa na waajiri nje ya nchi,” amesema Dkt. Munisi.

Amesema mafanikio hayo yameifanya Tanzania kuendelea kuaminika kuwa na nguvu kazi salama na yenye staha duniani.

Kuhusu uzinduzi wa Ughaibuni Loan, Dkt. Munisi amesema mkopo huo unalenga kuwawezesha vijana waliopata ajira nje ya nchi kupata fedha nafuu za kugharamia maandalizi ya safari ikiwemo tiketi ya ndege, bima na visa.

“Ughaibuni Loan siyo msaada bali ni mkopo wa uwezeshaji. Nawasihi vijana wahakikishe wanafanya marejesho ili na wengine wapate fursa,” amesisitiza.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CRDB, Bw. Pendason Philemon amesema benki imetenga jumla ya Shilingi bilioni 250 kwa miaka mitano kutoa mikopo ya kati ya Sh. 500,000 hadi milioni 20 kwa kila kijana kulingana na gharama za kufika kwa mwajiri wake.

“Kigezo muhimu ni kuwa na mkataba au barua ya ajira iliyothibitishwa na wakala. Marejesho yatakuwa kwa miezi 24 na tunatoa kipindi cha neema cha miezi 2 kwa riba ya asilimia 15,” amesema Philemon.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala Binafsi wa Ajira TRAA, Bw. Abdala Khalid amesema mkopo huo utawaepusha vijana na watu wasio na nia njema.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Zuhura Yunus amesema Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi,Ajira na Mahusiano inaendelea kutafuta masoko ya uhakika ya ajira ikiwemo Saudi Arabia, Oman, Qatar, Denmark na Ujerumani.

Mmoja wa wanufaika, Dickson Tadeo Mbaga amesema kupitia mkopo huo aliweza kugharamia visa, tiketi na bima. “Ninawasihi vijana wenzangu wachangamkie fursa hii,” amesema.

Serikali imesema itaendelea kuhakikisha vijana 530 wanaokwenda kufanya kazi ughaibuni katika fani mbalimbali ikiwemo ujenzi wanalindwa na kazi zao zinakuwa zenye staha.

 

Droo Ya UEFA Yatoa Mapambano Makali, Barca, Man United Na Atletico Zapata Wapinzani Wazito

MONACO : Droo ya hatua ya  Ligi ya mabingwa (league phase ya UEFA Champions League) msimu wa 2026/27 imefanyika usiku wa kuamkia leo Agosti 28, 2026 mjini Monaco, huku timu 36 zikijua wapinzani wao katika hatua hiyo ya mashindano.

Kwa mujibu wa mfumo mpya wa mashindano hayo, kila timu itacheza jumla ya mechi nane dhidi ya wapinzani tofauti, nne nyumbani na nne ugenini. Timu hizo zimegawanywa katika pots nne, huku kila timu ikipangiwa wapinzani wawili kutoka kila pot.

Miongoni mwa mapambano yanayotarajiwa kwa hamu kubwa ni kati ya Barcelona na Manchester City. Barcelona pia imepangwa kukutana na Paris Saint-Germain (PSG), Aston Villa, Sporting CP, Feyenoord, Galatasaray, Como na Sabah.

Barcelona itamkaribisha Manchester City nyumbani, kabla ya kusafiri kwenda Paris kukutana na mabingwa watetezi, PSG. Pia itakuwa na safari kwenda Uturuki kucheza dhidi ya Galatasaray na Azerbaijan kukutana na Sabah.

Kwa upande mwingine, Atlético Madrid imepangiwa kukutana na wapinzani wakubwa, akiwemo Bayern Munich, Liverpool na Manchester United, jambo linalofanya ratiba yake kuwa miongoni mwa zinazotarajiwa kwa hamu kubwa katika hatua hiyo.

Mabingwa watetezi, PSG, wataingia msimu huu wakiwa na lengo la kutetea taji lao baada ya kuifunga Arsenal kwa mikwaju ya penalti katika fainali ya msimu uliopita.

Hatua ya league phase ya Champions League msimu wa 2026/27 itaanza Septemba 8, 2026, huku timu nane zitakazomaliza katika nafasi za juu kwenye msimamo zikifuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora.

RATIBA YA LIGI YA MABINGWA ULAYA 2026/27

Hatua ya League Phase

  • Mechi za 1: 8–10 Septemba 2026

  • Mechi za 2: 13–14 Oktoba 2026

  • Mechi za 3: 20–21 Oktoba 2026

  • Mechi za 4: 3–4 Novemba 2026

  • Mechi za 5: 24–25 Novemba 2026

  • Mechi za 6: 8–9 Desemba 2026

  • Mechi za 7: 19–20 Januari 2027

  • Mechi za 8: 27 Januari 2027

Hatua ya Mtoano

  • Play-off: 16/17 na 23/24 Februari 2027

  • Hatua ya 16 Bora: 9/10 na 16/17 Machi 2027

  • Robo Fainali: 6/7 na 13/14 Aprili 2027

  • Nusu Fainali: 27/28 Aprili na 4/5 Mei 2027

  • Fainali: 5 Juni 2027, Estadio Metropolitano, Madrid.

WAPINZANI WA TIMU KUU

Barcelona

  • Manchester City

  • PSG

  • Aston Villa

  • Sporting CP

  • Feyenoord

  • Galatasaray

  • Como

  • Sabah

Manchester City

  • PSG

  • Barcelona

  • Sporting CP

  • Porto

  • Napoli

  • RB Leipzig

  • AEK Athens

  • Lens

PSG

  • Barcelona

  • Manchester City

  • Roma

  • Aston Villa

  • Galatasaray

  • Villarreal

  • Slovan Bratislava

  • Como

Real Madrid

  • Arsenal

  • Inter Milan

  • PSV

  • Roma

  • RB Leipzig

  • Shakhtar Donetsk

  • LASK

  • AEK Athens

Atlético Madrid

  • Bayern Munich

  • Manchester United

  • Liverpool

  • PSV

  • Fenerbahçe

  • Bodø/Glimt

  • Viking

  • Stuttgart

Bayern Munich

  • Arsenal

  • Atlético Madrid

  • Manchester United

  • Real Betis

  • Bodø/Glimt

  • Lille

  • Slavia Prague

  • Viking Stavanger

Liverpool

Arsenal

  • Real Madrid

  • Bayern Munich

  • Borussia Dortmund

  • Real Betis

  • Lille

  • Napoli

  • Slavia Prague

  • Sabah

MANCHESTER UNITED – CHAMPIONS LEAGUE 2026/27

  1. Bayern Munich — Nyumbani
  2. Atlético Madrid — Ugenini
  3. AS Roma — Nyumbani
  4. Sporting CP — Ugenini
  5. RB Leipzig — Nyumbani
  6. Villarreal — Ugenini
  7. Sabah FC — Nyumbani
  8. Como — Ugenini

Stori na Ashura Karimu | GPL- TUDACO

CCM KUMFUTA DKT. NCHIMBI UANACHAMA: JE, ANAKOMA MOJA KWA MOJA KUWA MAKAMU WA RAIS?

 

WAKILI PAUL KISABO ANAKUJA NA JIBU HILI  KUWA  HAPANA.

Ibara ya 47(4)(c) ya Katiba inaweka uanachama na udhamini wa chama cha siasa kama moja ya sifa za mtu kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais. Aidha, Ibara ya 47(4)(d) inamtaka mtu huyo kuwa na sifa zinazomwezesha kuwa Mbunge au Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Hivyo, kuwa mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa ni sharti la kikatiba katika uteuzi wa Makamu wa Rais.

Hata hivyo, baada ya mtu kushika nafasi hiyo, mazingira ya kukoma kuwa Makamu wa Rais yanaainishwa na Ibara ya 50(2) ya Katiba. Kwa mazingira ya Dkt. Emmanuel Nchimbi, Ibara ya 50(2)(c) inaeleza kuwa Makamu wa Rais ataendelea kushika kiti chake hadi atakapojiuzulu, huku Ibara ya 50(2)(h) ikitambua kukoma kushika nafasi hiyo vinginevyo kwa mujibu wa masharti ya Katiba.

Muhimu zaidi, Ibara ya 50(2) haisemi kwamba Makamu wa Rais anakoma kushika nafasi yake moja kwa moja anapopoteza uanachama wa chama kilichomdhamini.

Hii ni tofauti na nafasi ya Mbunge. Ibara ya 71(1)(e) ya Katiba inaeleza wazi kwamba Mbunge ataacha kuwa Mbunge iwapo ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwa mwanachama wake wakati alipochaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge.

Kwa hiyo, pale Katiba ilipotaka kupoteza uanachama wa chama kusababishe kupoteza nafasi ya kikatiba, imeeleza hivyo wazi. Masharti kama hayo hayajawekwa katika Ibara ya 50 kuhusu Makamu wa Rais.

Dkt. Nchimbi aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu tarehe 25 Agosti 2026 na kubainisha kwamba kujiuzulu kwake kutaanza kutumika tarehe 4 Septemba 2026.

Ibara ya 149(2) ya Katiba inaweka msingi muhimu kuhusu muda wa kuanza kutumika kwa kujiuzulu: pale mtu anapowasilisha kujiuzulu kwake kwa maandishi na kutaja tarehe ambayo kujiuzulu huko kutaanza kutumika, kujiuzulu huko kunakuwa na athari kuanzia tarehe aliyobainisha.

Kwa hiyo, kwa tafsiri ya masharti haya ya Katiba, kufutwa kwa uanachama wa CCM pekee hakumalizi moja kwa moja nafasi ya Dkt. Nchimbi kama Makamu wa Rais. Kwa kuwa katika barua yake alibainisha tarehe 4 Septemba 2026 kuwa ndiyo tarehe ya kuanza kutumika kwa kujiuzulu kwake, basi kujiuzulu huko kunaanza kuwa na athari za kikatiba tarehe hiyo.

Paul Kisabo

Wakili

Ayra Starr Aandika Historia Billboard, “Starrgirl” Yaingia Namba 4 Duniani

Mwimbaji wa Nigeria, Ayra Starr, ameendelea kuonyesha nguvu ya muziki wa Afrika katika soko la kimataifa baada ya album yake mpya “Starrgirl” kuingia katika nafasi ya nne kwenye Billboard World Albums Chart.

Mafanikio hayo yanaifanya “Starrgirl” kuwa miongoni mwa miradi iliyofanya vizuri kwenye chati hiyo, huku Ayra Starr akiendelea kujenga jina lake katika soko la muziki duniani.

Hii ni mara ya kwanza kwa Ayra Starr kuingia kwenye Billboard World Albums Chart kupitia album yake kama msanii wa solo, hatua inayochukuliwa kuwa moja ya mafanikio makubwa katika safari yake ya muziki pamoja na kuongeza heshima kwa muziki wa Nigeria.

Album hiyo ilitolewa rasmi Agosti 14, 2026, kupitia Mavin Records na Republic Records, ikiwa ni album yake ya tatu ya studio.

“Starrgirl” inafuatia album zake mbili zilizotangulia, “19 & Dangerous” iliyotoka mwaka 2021 na “The Year I Turned 21” iliyotolewa mwaka 2024.

Album hiyo ina jumla ya nyimbo 16, huku Ayra Starr akiwashirikisha baadhi ya majina makubwa kutoka Nigeria na kimataifa, akiwemo Wizkid, Rema, ZAYN, Leon Thomas, kwn, Theodora na Danny Ocean.

Miongoni mwa nyimbo zinazopatikana kwenye album hiyo ni “Gimme Dat” akiwa na Wizkid, “Who’s Dat Girl” akiwa na Rema na “Heaven Baby” akiwa na ZAYN.

“Starrgirl” Yawa Mbele ya Album ya Tyla

Katika Billboard World Albums Chart, “Starrgirl” imeingia katika nafasi ya nne, ikiwa nyuma ya miradi mitatu ya K-pop.

Nafasi ya tano imechukuliwa na album “APOP” ya msanii wa Afrika Kusini, Tyla, hivyo Ayra Starr ameweka “Starrgirl” mbele ya album hiyo katika chati.

Mafanikio hayo yamekuja ndani ya muda mfupi tangu album hiyo itoke, jambo linaloendelea kuongeza uzito wa Ayra Starr katika muziki wa Afrobeats na soko la muziki la kimataifa.

Kwa kuingia katika nafasi ya nne kwenye Billboard, Ayra Starr anaendelea kuthibitisha kuwa wasanii wa Afrika wana uwezo wa kushindana katika majukwaa makubwa ya muziki duniani na kuvuka mipaka ya bara hilo.

Stori na Razaku Ramadhan | GPL – TUDACO