Mbinu za kuvunja ukimya wa wanafunzi darasani

Dodoma. Mwalimu anaingia darasani. Anaandika swali ubaoni. Anageuka na kuwauliza wanafunzi: “Nani anaweza kujibu swali hili?”  Kimya.

Anaangalia upande wa kushoto. Kimya. Anaangalia upande wa kulia. Bado kimya. Wanafunzi wanatazamana, wengine wanaangalia chini, na wachache wanatabasamu kwa aibu. Mwalimu anaishia kusema: “Hivi kweli hakuna anayejua?”

Lakini pengine tatizo si kwamba wanafunzi hawajui. Tatizo linaweza kuwa tumewazoesha kukaa kimya.

Tukirudi nyuma kidogo katika maisha yetu ya utotoni, wengi wetu tulikulia katika mazingira ambayo mtoto alifundishwa kusikiliza zaidi kuliko kuzungumza.

Watu wazima wanapozungumza, mtoto alitakiwa kukaa kimya. Ukijaribu kuingilia mazungumzo, unaweza kusikia: “Kaa kimya! Unaongea nini wewe?” Au, “Funga mdomo, watu wazima wanaongea.”

Ujumbe huu unapojirudia mara nyingi, mtoto hujifunza jambo moja muhimu: kuongea mbele ya watu wazima kunaweza kuwa hatari.

Mtoto anakua. Anaingia shule. Anaendelea na sekondari. Anafika chuo kikuu. Lakini ile hofu ya kuzungumza mbele ya mwenye mamlaka wakati mwingine inasafiri naye.

Darasani, mwalimu anaonekana kuwa ndiye mwenye maarifa yote. Mwanafunzi anaingia akiwa na mtazamo kwamba yeye amekuja kupokea ‘madini’ kutoka kwa mwalimu. Mwalimu anajua; mwanafunzi anapaswa kusikiliza.

Matokeo yake ni darasa ambalo mwalimu anaweza kuzungumza kwa dakika 60, huku wanafunzi 60 wakiwa wasikilizaji.

Lakini elimu ya kisasa inataka zaidi ya kusikiliza. Inahitaji mwanafunzi afikiri, aulize, ajadili, apinge, aeleze na ajenge maarifa pamoja na wengine.

Hapo ndipo mbinu maarufu kwa Kiingereza ijulikanayo kwa jina la ‘Think–Pair–Share’ inapoweza kuwa muhimu.

Ni mbinu rahisi, lakini yenye nguvu. Mwalimu anauliza swali. Badala ya kumtaka mwanafunzi ajibu mara moja mbele ya darasa, anampa muda wa kwanza kufikiri mwenyewe (think), kisha  azungumze na mwanafunzi mwenzake (pair) na mwisho mawazo yanashirikishwa na darasa zima (share).

Kwa nini mbinu hii inaweza kufanya kazi vizuri katika mazingira yetu? Kwa sababu mwanafunzi anaweza kuwa na ujasiri mkubwa zaidi wa kuzungumza na mwanafunzi mwenzake kuliko kuzungumza moja kwa moja mbele ya mwalimu na darasa zima.

Fikiria mwanafunzi ameulizwa swali mbele ya wanafunzi 80. Anajua jibu, lakini anaogopa. Anafikiri, “Nikisema vibaya watanicheka.” Anaogopa mwalimu kusema hajui. Anaogopa wenzake kumwona hajui.

Lakini mwalimu akisema: “Kaa na mwenzako kwa dakika mbili, jadilini swali hili,” mazingira yanabadilika.

Mwanafunzi anamwambia mwenzake, “Mimi nimeelewa hivi…”

Mwenzake anajibu, “Mimi nimeona hivi…”

Wanalinganisha mawazo. Wanarekebishana. Wanajenga jibu.

Baada ya hapo mwalimu anaweza kusema: “Sasa niambieni, mwenzako amekuambia nini?”

Hapa kuna ujanja mkubwa wa kisaikolojia.

Mwanafunzi hatakiwi tena kusema, “Jibu langu ni hili.” Anaweza kusema, “Mwenzangu amesema…”

Hii inapunguza hofu ya kukosea. Ni rahisi zaidi kueleza wazo ambalo umesikia kutoka kwa mwenzako kuliko kusimama mbele ya watu na kutangaza kwamba “hili ndilo jibu langu.”

Hivyo hatua hii ndogo inaweza kuwa mwanzo wa kujenga ujasiri wa kitaaluma.

Baada ya muda, mwanafunzi ambaye jana aliogopa kusema neno moja mbele ya darasa, anaweza kuanza kuzungumza. Leo anazungumza na mwenzake. Kesho anashiriki katika kikundi baadaye anainua mkono. Hatimaye anaweza kusimama mbele ya darasa na kueleza wazo lake mwenyewe.

Kwa hiyo, Think–Pair–Share si tu mbinu ya kufanya wanafunzi washiriki somo. Inaweza kuwa daraja la kumtoa mwanafunzi kwenye utamaduni wa ukimya na kumuingiza katika utamaduni wa mazungumzo na ujenzi wa maarifa.

Hata hivyo, kuna jambo muhimu ambalo walimu tunapaswa kulielewa: ukimya si lazima uwe ujinga.

Mwanafunzi anayekaa kimya anaweza kuwa anajua. Anaweza kuwa na wazo zuri. Anaweza hata kuwa na jibu sahihi kabisa. Lakini anaweza kukosa ujasiri wa kulisema.

Kwa hiyo, kabla hatujasema “wanafunzi wetu hawajui”, tujiulize: Je, tumewajengea mazingira ya kuwaambia wanachojua?

Darasa halipaswi kuwa mahali ambapo mwalimu pekee ndiye mwenye haki ya kuzungumza. Mwalimu anaweza kuwa mwezeshaji wa maarifa, lakini wanafunzi pia wana uzoefu, mawazo, maswali na mitazamo inayoweza kulifanya darasa liwe hai.

Labda tunahitaji kubadilisha kidogo ujumbe tuliokulia nao. Badala ya mtoto kuambiwa kila mara: “Kaa kimya, watu wazima wanaongea.” Darasani tumwambie: “Fikiri, zungumza na mwenzako. Sikiliza. Kisha shiriki.”

Hii ni kwa sababu wakati mwingine, mwanafunzi hahitaji kushinikizwa kuzungumza mbele ya watu 60. Anahitaji tu kupewa mtu mmoja wa kwanza wa kuzungumza naye.

Hapo ndipo Think–Pair–Share inapoanzia. Na pengine, hapo ndipo safari ya kuvunja ukimya wa mwanafunzi wa Kitanzania inaweza kuanzia.

BIDHAA ZA CHAKULA ZISIZOKIDHI MATAKWA YA VIWANGO ZATEKETEZWA .

 Na Mwandishi Wetu.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeendelea kuonesha dhamira yake ya kulinda afya za wananchi baada ya kuteketeza tani 39 za bidhaa za chakula ambazo hazikukidhi matakwa ya viwango, zenye thamani ya takribani Shilingi milioni 149.

Zoezi hilo la uteketezaji lililofanyika leo, Agosti 17, 2026, katika eneo la Mbezi Gongoni, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ni sehemu ya juhudi za TBS katika kuhakikisha bidhaa zinazopatikana sokoni zinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Kwa mujibu wa Meneja wa TBS Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bi. Noor Meghji, bidhaa hizo zilikamatwa kupitia ukaguzi wa mara kwa mara uliofanywa na wakaguzi wa shirika hilo katika kipindi cha Julai hadi Agosti mwaka huu.

Amesema ukaguzi huo umebaini kuwa baadhi ya bidhaa za chakula zinazouzwa katika masoko mbalimbali hazikuzingatia matakwa ya viwango, jambo ambalo linaweza kuhatarisha afya za watumiaji.

Bi. Meghji alieleza kuwa changamoto kubwa iliyobainika ni uwepo wa bidhaa nyingi ambazo hazikuwa na alama ya ubora pamoja na kukosa maelezo sahihi kwenye vifungashio.

Alifafanua kuwa baadhi ya bidhaa hizo hazikuwa na taarifa zilizoandikwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza, kinyume na matakwa ya Sheria ya Viwango nchini inayotaka maelezo ya bidhaa yawe wazi ili kumwezesha mtumiaji kuelewa bidhaa anayotumia na viambata vilivyomo.

“Ni muhimu kwa watumiaji kusoma maelezo yote yaliyopo kwenye vifungashio kabla ya kutumia bidhaa yoyote. Hii itawasaidia kufahamu bidhaa wanazonunua pamoja na kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyotakiwa,” alisema Bi. Meghji.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara kuzingatia sheria na kuhakikisha bidhaa wanazoziingiza au kuziuza zinakidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika.

Hatua ya TBS kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara sokoni imeendelea kupongezwa na wadau mbalimbali kutokana na mchango wake katika kulinda afya za wananchi pamoja na kuimarisha mazingira salama ya biashara.

Kupitia ukaguzi huo, bidhaa ambazo hazikidhi viwango huondolewa sokoni mapema kabla hazijasambazwa kwa watumiaji, jambo ambalo limeendelea kusaidia kupunguza hatari ya matumizi ya bidhaa zisizo salama.

Hatua hiyo inaonesha wazi kuwa TBS, inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kulinda afya ya jamii kwa vitendo kupitia ukaguzi endelevu unaosaidia kuhakikisha bidhaa zinazofika kwa watumiaji zinakuwa salama, zenye ubora na zinazokidhi matakwa ya sheria za nchi.

NAIBU WAZIRI NDERIANANGE AWATIA MOYO WENYE ULEMAVU IRINGA ATAKA WACHANHAMKIE FURSA YA MIKOPO

  

NA MATUKIO DAIMA

MEDIA

IRINGA.Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na anayeshughulika na watu wenye  Ulemavu, Ummy Nderianange amewataka watu wenye ulemavu kutumia mikopo inayotolewa na Serikali kama fursa ya kujikwamua kiuchumi na kubadili maisha yao, badala ya kuichukulia kama msaada au hisani.

Naibu Waziri ameyasema hayo leo, Agosti 17, 2026, katika Ofisi za Mkoa wa Iringa, wakati wa ziara yake ya kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi na kijamii.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu kupata mikopo na fursa nyingine za kiuchumi, huku akibainisha kuwa kiasi kikubwa cha fedha tayari kimetolewa kwa wanufaika nchini. 

Amesema awali watu wenye ulemavu nchini walikuwa wameweza kukopa kiasi cha takribani shilingi bilioni 5, lakini takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa kiwango hicho kimeongezeka na kufikia shilingi bilioni 23, jambo alilolitaja kuwa ni ongezeko kubwa linaloonesha mwamko wa watu wenye ulemavu katika kutumia fursa za uwezeshaji.

Amesema ongezeko hilo ni ishara kuwa watu wenye ulemavu wameanza kutambua na kutumia fursa zinazotolewa kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi, hivyo kuwataka kuendelea kujitokeza na kutumia fursa hizo kwa maendeleo yao na familia zao.

“Mafanikio ya baadhi ya watu wenye ulemavu waliopata mikopo yanapaswa kutumika kama mfano na kuwahamasisha wengine kuchangamkia fursa hizo”

Aidha Waziri Ummy  ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kujitathmini katika utoaji wa mikopo kwa watu wenye ulemavu, akibainisha kuwa kiwango kilichotolewa katika manispaa hiyo bado ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo. 

“Serikali za mitaa zinapaswa kuhakikisha fursa za mikopo zinawafikia walengwa, huku wakitenga pia maeneo maalumu ambayo watu wenye ulemavu wanaweza kufanya shughuli za uzalishaji na biashara”

Naibu Waziri huyo amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Serikali na viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu mkoani Iringa, akisema ushirikiano huo unarahisisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu,amesema viongozi wa Serikali na wawakilishi wa watu wenye ulemavu wanapaswa kuwa karibu zaidi ili kuhakikisha changamoto na mahitaji ya kundi hilo yanafikishwa kwa mamlaka husika kwa wakati.

Ameeleza kuwa Serikali pia inaendelea kuhamasisha uwepo wa maeneo maalumu yenye huduma mbalimbali kwa watu wenye ulemavu, ambapo wanaweza kupata huduma kwa pamoja na kuendesha shughuli za kiuchumi. 

Amesema maeneo hayo yanaweza kuwa na shughuli za biashara, ubunifu na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, hivyo kuwawezesha watu wenye ulemavu kupata kipato na kujitegemea badala ya kutegemea msaada.

Kwa upande wake, Mmoja wa walemavu wa ngozi (Albino) Sambala amewaomba viongozi wa mkoa, wilaya na halmashauri kuendelea kutenga sehemu ya bajeti kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu, pamoja na kutafuta maeneo kwa ajili ya shughuli zao za uzalishaji. 

Amesema hatua hizo zinaendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa tabasamu, huku akisisitiza kuwa mafanikio ya watu wenye ulemavu yatakuwa sehemu muhimu ya kutimiza dhamira hiyo.

Akisoma taarifa ya manispa  katika ziara ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu wa Watu Wenye Ulemavu, shughuli hizo zimewezesha baadhi ya wanufaika kuongeza mitaji ya biashara, kuboresha maisha yao na wengine kuweza kuajiri watu katika shughuli zao, Halmashauri imeeleza kuwa moja ya changamoto kubwa iliyopo ni baadhi ya wanufaika kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati.

Akizungumzia changamoto hiyo, viongozi wa watu wenye ulemavu wamesema bado kuna haja ya kuongeza elimu kuhusu mikopo hiyo, hususan kwa kuwa baadhi ya wanufaika wamekuwa wakiichukulia kama msaada au hisani kutoka Serikalini. 

“Elimu hiyo inapaswa kutolewa kabla ya vikundi kupokea fedha, ili wanufaika waelewe masharti ya mikopo, matumizi sahihi ya fedha na wajibu wao wa kurejesha,wamependekeza kuwepo kwa utaratibu endelevu wa kutoa elimu kwa wanufaika wa mikopo, badala ya kufanya hivyo siku chache kabla ya fedha kutolew,elimu ya mara kwa mara itasaidia kuwawezesha watu wenye ulemavu kuelewa fursa zilizopo, kuendesha shughuli zao kwa ufanisi na kuongeza uwezekano wa kurejesha mikopo kwa wakati”alisema 

TAZAMA VIDEO BOFYA LINK HII

Wabunifu zaidi ya 300 kushiriki maonyesho Tanga

Tanga. Wabunifu zaidi ya 300 kutoka maeneo mbalimbali nchini wanatarajiwa kushiriki Maonyesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yatakayofanyika kwa wiki mbili kuanzia kesho, Agosti 18, 2026, katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara mkoani Tanga.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho hayo, huku Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akitarajiwa kuyafunga Agosti 24, 2026.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Burian akizungumza leo ofisini kwake jijini Tanga, amesema maandalizi ya maonyesho hayo yanaendelea vizuri na zaidi ya washiriki 300 tayari wamewasili mkoani humo na wameanza kuandaa mabanda yao.

Amesema washiriki watapata fursa ya kuonyesha bunifu, bidhaa na shughuli mbalimbali zinazohusiana na elimu, ujuzi na teknolojia.

“Maonyesho haya yanalenga pia kutoa fursa kwa wabunifu kuonyesha kazi zao, kubadilishana uzoefu na kupata fursa za kukuza bunifu zao,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Kwa upande wake, Kaimu Mratibu wa Kituo cha Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Flavian Sanga, amesema chuo hicho kitashiriki kwa kuonesha bunifu mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian akizingumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ujuzi elimu na ubunifu katika viwanja vya shule ya sekondari Usagara jijini Tanga   

Amesema sehemu kubwa ya bunifu hizo inalenga kuboresha huduma katika sekta ya afya na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Naye Shaphii Hamisi kutoka Chuo cha Uhandisi na Teknolojia cha Al-Maktoum, amesema wamewasilisha bunifu zinazolenga kusaidia kupunguza msongamano wa magari katika maeneo yenye taa za barabarani.

Amesema pia wamekuja na mfumo wa kuuza maji kwenye vioski bila kuhitaji uwepo wa muuzaji wakati wote.

Kwa mujibu wa waandaaji, maonyesho hayo yatatoa nafasi kwa wabunifu kutoka sekta mbalimbali kukutana, kujifunza kutoka kwa wenzao na kutafuta fursa za kuendeleza kazi zao.

Aidha, yanatarajiwa kuwa jukwaa la kuonesha namna elimu, ujuzi, teknolojia na ubunifu vinavyoweza kutumika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Bunge lasogezwa mbele kupisha sherehe za Maulid

Dar es Salaam. Baada ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kutangaza kuwa Jumanne Agosti 25 Agosti, 2026 itakuwa ni Sikukuu ya Maulid, mkutano wa nne wa Bunge umesogezwa mbele na sasa utaanza Jumatano Agosti 26.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Agosti 17,2026 na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma ya  ofisi ya Bunge, imeeleza mabadiliko hayo yamefanyika ili kutoa fursa kwa Waislam wote na Watanzania kwa ujumla kusherehekea sikukuu hiyo ambayo kitaifa itafanyika Jijini Dar es Salaam.

“Kwa mujibu wa hoja iliyotolewa bungeni na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu  Nchemba Juni 26, 2026, mkutano wa nne wa Bunge la  13 umepangwa kuanza siku ya Jumanne Agosti , 2026.”

“ Hata hivyo, kufuatia taarifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kuutangazia umma kuwa siku ya Jumanne Agosti  25 Agosti, 2026 itakuwa ni Sikukuu ya Maulid.”

“Mheshimiwa Spika kwa mamlaka yake chini ya Kanuni ya 35 (4) na (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2025 anapenda kuwataarifu Waheshimiwa wabunge na umma wote wa Tanzania, kuwa mkutano wa nne wa Bunge utaanza siku ya Jumatano Agosti 26, 2026 saa 3:00 asubuhi,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari leo Agosti 17, 2026, Katibu Mkuu wa Bakwata, Nuhu Mruma, amesema Maulid hayo yatasomwa usiku wa Agosti 24, katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Wakati Baraza la Maulid litafanyika Jumanne Agosti 25, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) na mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Agizo la Chalamila Stendi ya Magufuli lapingwa

Dar es Salaam. Abiria wameendelea kupinga uamuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wa kutaka mabasi ya mikoani kuanzia na kumalizia safari katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, wakitaka suala hilo litazamwe upya kwa kuzingatia masilahi ya abiria, hususan wanaoishi mbali na Mbezi Luis.

Uamuzi huo umeibua kumbukumbu ya agizo kama hilo lililowahi kutolewa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, ambalo pia lilikumbana na malalamiko kutoka kwa wananchi na hatimaye kubadilishwa.

Makalla, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, alitoa agizo hilo Julai 2021, akitaka mabasi yanayoingia na kutoka Dar es Salaam kutumia Kituo cha Mabasi cha Magufuli kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria. Agizo hilo lilitolewa wakati akisikiliza kero za wafanyabiashara katika kituo hicho, ambao walilalamikia baadhi ya mabasi kupakia na kushusha abiria nje ya kituo, hivyo kupunguza wateja katika eneo hilo.

Hata hivyo, agizo hilo lilikutana na upinzani kutoka kwa wananchi waliodai kuwa kulazimisha abiria wote kufika Mbezi Luis kungeongeza gharama na usumbufu, hasa kwa wanaotoka au kuelekea maeneo ya kusini na katikati ya jiji.

Malalamiko hayo yalihusu pia abiria waliokuwa wakishushwa Magufuli baada ya safari ndefu, kisha kulazimika kutafuta usafiri mwingine kwenda maeneo yao ya makazi ilihali baadhi ya mabasi yanayowashusha yanaelekea wanakokwenda.

Hoja hiyo ilifikia Serikali Kuu, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi kwa wakati huo, Innocent Bashungwa, Agosti 30, 2022, alimtaka Makalla kukutana na wadau na wamiliki wa mabasi, ili kuweka utaratibu shirikishi usiowaongezea wananchi adha.

Bashungwa alisema wakati huo kuwa baadhi ya abiria wanaoingia Dar es Salaam kupitia Magufuli walihitaji mabasi hayo kuendelea hadi vituo vya mabasi vilivyojengwa na sekta binafsi mjini ili kuwafikisha karibu na maeneo yao.

Alisisitiza kuwa lengo la Serikali la kutumia Kituo cha Magufuli linaweza kutekelezwa bila kuwaongezea wananchi gharama za kutafuta usafiri mwingine baada ya kushushwa Mbezi Luis.

Baadaye, Makalla aliruhusu vituo binafsi vilivyohakikiwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kuendelea kutoa huduma, kwa sharti la mabasi kuingia na kutoka Kituo cha Magufuli.

Chalamila alitoa agizo hilo Agosti 11, 2026, akizitaka kampuni za mabasi zinazotoa huduma nje ya Kituo cha Mabasi cha Magufuli kuhamia kituoni hapo na kuanza kutoa huduma zake kutoka eneo hilo.

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa muda wa siku sita kwa kampuni hizo kutekeleza agizo hilo, akisisitiza kuwa ifikapo leo, Agosti 17, 2026, mabasi yote ya masafa marefu yanapaswa kuwa yameondoka katika vituo vingine na kurejea Kituo cha Magufuli.

Gazeti hili lilifika katika maeneo yenye ofisi za kampuni mbalimbali za mabasi, ikiwamo Ubungo, Shekilango, Manzese, Argentina na Magomeni, na kubaini kuwa shughuli za usafirishaji wa abiria bado zinaendelea kama kawaida.

Baadhi ya abiria waliozungumza na gazeti hili walipinga agizo hilo, akiwamo Leonard Munisi aliyesema viongozi wanapotoa maamuzi wanapaswa kuzingatia mabadiliko ya maisha na mahitaji ya abiria, akisema miundombinu ya usafiri iliyopo inapaswa kutumika kwa manufaa ya abiria.

 “Kama suala ni mapato ya Kituo cha Magufuli, Serikali inaweza kuangalia namna ya kuongeza tozo kidogo kwa mabasi yanayopakia au kushusha abiria nje ya kituo hicho. Serikali isiangalie tu mapato, iangalie pia ubinadamu na namna ya kuwasogezea wananchi huduma karibu,” amesema.

Naye William Makali amesema agizo hilo linaweza kuwaongezea abiria usumbufu, ikiwamo kuvutwa mabegi na wapiga debe, kutapeliwa na hata kuibiwa wanapofika Magufuli kutafuta usafiri.

“Sisi tunaishauri Serikali iangalie changamoto zilizopo na kufanya uamuzi kwa masilahi mapana ya abiria ili vituo vilivyo nje ya Magufuli viendelee kufanya kazi kwa kuwa vina faida nyingi kuliko hasara,” amesema.

Kwa upande wake, Elly Mumbungu, mkazi wa Mbagala, amesema agizo hilo litawaumiza wananchi wa kipato cha kawaida, akisema mabasi yanayowafikisha maeneo ya Mbagala, Mbande, Kigamboni na Chanika yamekuwa yakirahisisha maisha yao.

“Sasa ukiniambia nishuke Mbezi, gharama ya kutoka huko hadi nyumbani nani atabeba? Maisha ni magumu,” amesema.

Baadhi ya wamiliki na wadau wa usafirishaji wa mabasi nchini wameitaka Serikali kulitazama kwa jicho la ziada agizo hilo, wakisema utekelezaji wake unaweza kuwaongezea changamoto abiria.

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo, amesema baada ya Kamati Tendaji kukutana, wamekubaliana kuwasiliana na viongozi wa Serikali ili kujadiliana kuhusu agizo hilo.

“Hadi sasa bado tunaendelea kufanya jitihada za kwenda kuzungumza nao, na barua tayari zilishatumwa. Kwa hiyo, bado hatuna msimamo tulioufikia kuhusu jambo hilo zaidi ya kwenda kukubaliana kuongea na viongozi,” amesema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Tilisho, John Tilisho, amesema Serikali inapaswa kuwapa kipaumbele wamiliki ambao wamewekeza katika kujenga vituo na ofisi zao, ili wananchi wapate huduma karibu na maeneo wanayoishi.

Amesema kauli ya Chalamila, si mbaya, lakini ingekuwa vyema viongozi kutembelea vituo mbalimbali na kujionea changamoto zilizopo.

“Kwenda Mbezi ni jambo zuri, lakini kwa watu wanaosafiri kwenda mikoa ya Kaskazini itakuwa changamoto kwa sababu ya njia,” amesema.

Tilisho amesema barabara ya Goba ambayo baadhi ya mabasi yatapaswa kutumia ina changamoto kutokana na kuwa nyembamba na ina matuta mengi, hali ambayo inaweza kuongeza muda wa safari.

“Ukisema unatoka Stendi ya Magufuli kufika Moshi muda fulani, hicho kitu hakipo. Changamoto itakuwa kubwa,” amesema.

Amesema Serikali inaweza kushirikiana na wamiliki wa vituo binafsi kwa kuwawekea utaratibu wa kulipa tozo au ada zinazostahili badala ya kuwalazimisha kuhamia Magufuli.

Kwa upande wake, mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Esther Luxury, Joseph Ngelleuya, amesema hawapingani na Serikali na watafuata maelekezo yatakayotolewa, akisema mwisho wa siku anayebeba athari za uamuzi huo ni abiria.

“Tukishapewa maelekezo ni kuyafuata. Hatuwezi kupingana na Serikali. Tunawasikiliza na kutenda wanalolitaka, kwa sababu katika suala hili mwathirika ni mwananchi,” amesema.

Mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Shabiby, Ahmed Shabiby, amesema agizo la kuondoa vituo visivyo rasmi katikati ya Jiji linapaswa kuungwa mkono, lakini amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na masilahi ya abiria.

Amesema Latra inaruhusu mtu mwenye sifa na kituo kilichokidhi vigezo kuendesha shughuli hizo, hivyo vituo vilivyoidhinishwa vinapaswa kuruhusiwa kufanya kazi.

“Watu wakipata kituo ambacho kimekubaliwa na Latra waachwe waegeshe,” amesema.

Hata hivyo, Shabiby amesema mabasi yote yanapaswa kupitia Kituo cha Magufuli ili kukaguliwa na Serikali kukusanya mapato.

Ametoa mfano wa Dodoma, ambako mabasi huanzia katika vituo vyao, lakini hulazimika kupitia stendi kuu kwa ajili ya ukaguzi na malipo ya ushuru.

Amesema utaratibu huo unaweza kuleta usawa kwa Serikali kupata mapato huku abiria wakiruhusiwa kuanzia safari zao katika vituo vilivyo karibu nao.

Naye msemaji wa Kampuni ya Kimbinyiko, Hamisi Maneno, ameunga mkono agizo la Chalamila, akisema uegeshaji wa mabasi katika maeneo yasiyo rasmi umeongeza msongamano na kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.

Amesema suluhisho ni kuwa na vituo maalumu, huku akitaka mabasi yote yalazimishwe kupitia stendi kwa ajili ya ukaguzi na ulipaji wa ushuru.

Ametolea mfano eneo la Urafiki, akisema limekuwa likitumika kama eneo la maegesho kwa namna inayosababisha changamoto kwa watumiaji wengine, huku baadhi ya vituo vikikosa huduma muhimu kwa abiria.

Kaimu Meneja wa leseni Latra, Pateli Ngereza, amesema kwa Mkoa wa Dar es Salaam mabasi yote yanayotoka Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Ziwa  yanapaswa kuishia kituo cha mabasi kilichopo Mbezi Louis (yaani Magufuli Bus Terminal).

Huku yale mabasi yanayotoka Mikoa ya Kusini yakipaswa kuishia kituo cha mabasi Mbagala kilichopo Wilaya ya Temeke jijini humo.

Imeandikwa na Tuzo Mapunda, Nasra Abdallah, Habel Chidawali (Dodoma) na Janeth Joseph (Kilimanjaro)

TRA Songwe kuanzisha klabu za kodi shule za sekondari

Songwe. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Songwe imeanza mchakato wa kuanzisha klabu za kodi katika shule zote za sekondari mkoani humo, ikiwa ni mkakati wa kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.

Klabu hizo zinalenga pia kuwawezesha wanafunzi kufahamu masuala ya kodi na kuyafikisha katika jamii, hususan umuhimu wa kudai na kutoa risiti wakati wa manunuzi na kufanya biashara.

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Songwe, Angetile Kitalile, amesema hayo leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, wakati wa uzinduzi wa klabu ya kodi katika Shule ya Sekondari Mlowo wilayani Mbozi.

Amesema hadi sasa mamlaka hiyo imefanikiwa kuanzisha klabu saba katika shule za sekondari mkoani humo na mpango ni kuzifikia shule zote katika halmashauri za mkoa huo.

“Mpaka sasa tumefanikiwa kufungua klabu saba za kodi katika shule za sekondari. Leo tumeifikia Shule ya Sekondari Mlowo iliyopo hapa Wilaya ya Mbozi, ikiwa ni mwendelezo wa mpango huu, tukiamini wanafunzi watasaidia kuifikisha elimu hiyo katika jamii wanayoishi,” amesema.

Kitalile amesema klabu hizo ni miongoni mwa njia zinazotumiwa na TRA kutoa elimu kwa walipa kodi wa sasa na kuwaandaa walipa kodi wa baadaye.

Amesema wanafunzi watakaopata elimu hiyo wataweza kuelewa wajibu wa kila mwananchi katika kulipa kodi na umuhimu wa kudai risiti wanaponunua bidhaa au kupata huduma.

Kwa mujibu wa Kitalile, elimu hiyo pia itasaidia kujenga utamaduni wa kufuata taratibu za kodi na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mchango wa kodi katika maendeleo ya Taifa.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mlowo, Sophia Luoga, amepongeza hatua hiyo akisema itawajengea wanafunzi uzalendo na kuwafanya kuwa mabalozi wazuri wa masuala ya kodi katika familia na jamii.

Amesema matarajio yao ni kuona elimu inayotolewa kupitia klabu hizo ikisaidia kizazi cha sasa na kijacho kuelewa wajibu wa kulipa kodi wakati wa kununua au kuuza bidhaa.

“Wanafunzi wataelewa kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kulipa kodi na kwamba wakati wa kununua bidhaa au kufanya biashara, ni muhimu kutoa na kudai risiti ili Taifa lipate mapato ya kuendeleza miradi ya maendeleo,” amesema.

Baadhi ya wanafunzi walioshiriki kuanzishwa kwa klabu hiyo wamesema mpango huo utawasaidia kupata uelewa zaidi kuhusu masuala ya kodi, ikiwamo umuhimu wa kudai na kutoa risiti sahihi wanaponunua bidhaa au kufanya biashara.

Wamesema watatumia elimu watakayoipata kuwafikishia wazazi, ndugu na wananchi wengine ili kuongeza uelewa kuhusu ulipaji kodi na mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

GLOBAL EDUCATION LINK YAPELEKA WANAFUNZI 198 CHINA NA 189 INDIA

 

 

Na Matukio Daima Media , Dar es Salaam

GLOBAL Education Link (GEL) imewakabidhi nyaraka rasmi za safari wanafunzi 387 wa Kitanzania wanaotarajia kwenda kuendelea na masomo ya elimu ya juu nchini China na India, huku wakihimizwa kutumia fursa hiyo kupata zaidi ya shahada kwa kujenga maarifa, ujuzi, teknolojia, mitandao ya kimataifa na uwezo wa kujitengenezea fursa za maisha.

Ukabidhi huo umefanyika kupitia mikutano miwili maalumu iliyofanyika Agosti 10 na 11, 2026 katika Ukumbi Mkuu wa Makao Makuu ya Global Education Link, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa pia na wazazi na walezi wa wanafunzi hao.

Kati ya wanafunzi hao, 198 wanaelekea nchini China na 189 wanaelekea nchini India kwa ajili ya kuanza masomo katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu.

Wazazi na walezi waliohudhuria mikutano hiyo kwa ajili ya kushuhudia ukabidhi wa nyaraka na kupata maelekezo kuhusu safari na maisha ya watoto wao watakapokuwa nje ya nchi.

Lengo kuu la mikutano hiyo lilikuwa kuwakabidhi wanafunzi nyaraka muhimu za safari ambazo zimekamilishwa na GEL kama sehemu ya huduma inayofanywa nataasisi hiyo  katika hatua mbalimbali za maandalizi yao, zikiwemo pasipoti, visa, tiketi za ndege, NOC (No Objection Certificate), cheti au kijitabu cha chanjo ya homa ya manjano (Yellow Fever Certificate) pamoja na nyaraka nyingine zinazohitajika na mamlaka husika kulingana na nchi, chuo na masharti ya safari ya mwanafunzi katika chuo husika.

Mbali na kukabidhiwa nyaraka hizo, wanafunzi pamoja na wazazi na walezi wao walipata maelekezo ya mwisho kuhusu taratibu za safari, uhamiaji, mazingira ya vyuo, makazi, bima ya afya, usalama, matumizi ya fedha, nidhamu na namna ya kukabiliana na mazingira mapya watakapofika katika nchi wanazokwenda.

Mtoa mada mkuu katika mikutano hiyo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Bw. Abdulmalik Mollel, akishirikiana na wawakilishi wa vyuo kutoka China na India waliotoa ufafanuzi kuhusu masomo, huduma za vyuo na maisha ya mwanafunzi wa kimataifa.

Global Education Link ni wakala wa vyuo vikuu vya nje ya nchi mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 19 katika kusaidia wanafunzi wa Kitanzania pamoja na wazazi na walezi wenye watoto wenye ndoto ya kupata elimu ya juu nje ya nchi.

Katika kipindi hicho, taasisi hiyo imekuwa ikitoa mwongozo katika hatua mbalimbali kuanzia ushauri wa kielimu, uchaguzi wa programu na chuo, maombi ya udahili, maandalizi ya nyaraka, visa, safari na maandalizi ya mwanafunzi kabla ya kuondoka nchini.

Akizungumza katika mikutano hiyo, Mollel aliwataka wanafunzi kutokwenda China na India kwa lengo la kupata cheti au shahada pekee, bali kutumia mazingira ya vyuo watakavyosoma kujenga uwezo mpana utakaowasaidia baada ya kuhitimu.

Alisema kwenda kusoma nje ya nchi kunamfungulia mwanafunzi mazingira mapya yenye teknolojia, maabara, warsha, vituo vya ubunifu, wataalamu pamoja na wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali, hivyo ni jukumu la mwanafunzi mwenyewe kutumia fursa hizo kwa manufaa yake na Taifa.

Aliwataka vijana hao kwenda zaidi ya masomo yao ya darasani kwa kutembelea maabara, warsha na vituo vya ubunifu na kujifunza kwa vitendo namna teknolojia na bidhaa mbalimbali zinavyozalishwa na kutumika katika kutatua changamoto za jamii.

Akitolea mfano mwanafunzi anayesomea Business Administration, alisema haipaswi kutosha kujifunza nadharia za usimamizi wa biashara pekee, bali mwanafunzi huyo anapaswa kutafuta maarifa kuhusu bidhaa, teknolojia, uzalishaji na mifumo mbalimbali ya viwanda ili aweze kuelewa kile anachoweza kukisimamia au kukigeuza kuwa biashara

16 mbaroni kwa tuhuma za kuchoma moto shamba, matrekta ya mwekezaji

Babati. Wakazi 16 wa Kijiji cha Kiru, wilayani Babati, Mkoa wa Manyara, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuvamia eneo la mwekezaji wa Dudumera Estate na kuchoma moto shamba pamoja na matrekta matatu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani, amethibitisha kushikiliwa kwa watu hao na kusema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, Makarani amesema tukio hilo lilitokea Agosti 15, 2026, katika Kijiji cha Kiru.

“Tunaendelea kuwashikilia watu 16 kwa tuhuma hizo na uchunguzi ukikamilika, hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa,” amesema kamanda huyo.

Baadhi ya wajumbe wa kamati ya usalama ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara, wakikagua maeneo ya kampuni ya Dudumera Estate yaliyochomwa moto na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kiru wilayani Babati mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

Amesema watuhumiwa hao wanadaiwa kushiriki kuchoma mali mbalimbali, zikiwamo shamba na matrekta matatu.

Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Babati, ikiongozwa na katibu tawala wa wilaya hiyo, Thobias Abwaro, leo imefika eneo la tukio na kujionea madhara yaliyosababishwa na moto huo.

Hata hivyo, Abwaro amelipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua ya kuwakamata watu hao huku akisema Serikali inaendelea kuchukua hatua nyingine zaidi kuhusu tukio hilo.

“Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Agosti 15, 2026, baada ya kundi la watu kudaiwa kuvamia eneo la mwekezaji huyo na kuchoma moto shamba lenye ukubwa wa takribani hekta 15,” amesema na kuongeza kuwa shamba hilo lilikuwa likilimwa miwa na mtama.

Kwa mujibu wa Abwaro, chanzo kinachodaiwa kusababisha tukio hilo ni mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi wa eneo hilo na mwekezaji, licha ya jitihada za viongozi wa Serikali za kutafuta suluhisho kufanyika.

Mwekezaji wa Dudumera Estate, Radhika Jeta, amesema tukio hilo limemsababishia hasara kubwa kutokana na uharibifu wa mali na kuvurugika kwa shughuli za uzalishaji shambani.

Amesema matrekta matatu yameteketea pamoja na mashamba yaliyokuwa yamepandwa miwa na mtama.

“Nimesikitishwa na tukio hilo la uchomaji moto, kwani mara nyingi tumekuwa tukishirikiana na wananchi na viongozi wa eneo hili. Mimi huwa nashiriki kutoa michango mbalimbali ya maendeleo,” amesema Jeta.

Akizungumzia tukio hilo, mlinzi wa eneo hilo, Hussein Twabatari, amesema usiku wa tukio alishtushwa na kundi la watu waliobeba silaha za jadi lililovamia eneo hilo.

Amesema alihofia usalama wake kutokana na namna uvamizi huo ulivyofanyika.

Wakati huohuo, tukio hilo limeathiri pia huduma ya umeme katika baadhi ya maeneo ya Tarafa ya Mbugwe.

Ofisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Manyara, Samuel Mandari, amesema watu wasiojulikana walichoma nguzo ya umeme na kusababisha baadhi ya maeneo kukosa huduma hiyo.

“Watu wasiojulikana wamechoma nguzo ya Tanesco na tukio hilo limesababisha hasara kwa shirika, na wakazi wa maeneo ya Magugu na jirani wamekosa huduma ya umeme,” amesema Mandari.Akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati leo Jumatatu Agosti 17, 2026, Makarani amesema tukio hilo lilitokea Agosti 15, 2026 katika Kijiji cha Kiru.

Shamba la miwa la kampuni ya Dudumera Estate lililochomwa moto na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kiru wilayani Babati mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

“Tunaendeleo kuwashikilia watu 16 kwa tuhuma hizo na uchunguzi ukikamilika hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa,” amesema kamanda huyo.

Amesema watuhumiwa hao wanadaiwa kushiriki kuchoma mali mbalimbali, zikiwamo shamba na matrekta matatu.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Babati, ikiongozwa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Thobias Abwaro, leo imefika eneo la tukio na kujionea madhara yaliyosababishwa na moto huo.

Hata hivyo, Abwaro amelipongeza Jeshi la Polisi  kwa hatua ya kuwakamata watu hao huku akisema Serikali inaendelea kuchukua hatua nyingine zaidi kuhusu tukio hilo.

“Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Agosti 15, 2026 baada ya kundi la watu kudaiwa kuvamia eneo la mwekezaji huyo na kuchoma moto shamba lenye ukubwa wa takribani hekta 15,” amesema na kuongeza kuwa shamba hilo lilikuwa likilimwa miwa na mtama.

Kwa mujibu wa Abwaro, chanzo kinachodaiwa kusababisha tukio hilo ni mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi wa eneo hilo na mwekezaji, licha ya jitihada za viongozi wa Serikali za kutafuta suluhisho kufanyika.

Mwekezaji wa Dudumera Estate, Radhika Jeta amesema tukio hilo limemsababishia hasara kubwa kutokana na uharibifu wa mali na kuvurugika kwa shughuli za uzalishaji shambani.

Matrekta ya kampuni ya Dudumera Estate yaliyochomwa na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kiru wilayani Babati mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

Amesema matrekta matatu yameteketea pamoja na mashamba yaliyokuwa yamepandwa miwa na mtama.

“Nimesikitishwa na tukio hilo la uchomaji moto kwani mara nyingi tumekuwa tukishirikiana na wananchi na viongozi wa eneo hili, mimi huwa nashiriki kutoa michango mbalimbali ya maendeleo,” amesema Jeta.

Alizungumzia tukio hilo, mlinzi wa eneo hilo, Hussein Twabatari amesema usiku wa tukio alishtushwa na kundi la watu waliobeba silaha za jadi lililovamia eneo hilo.

Amesema alihofia usalama wake kutokana na namna uvamizi huo ulivyofanyika.

Wakati huohuo, tukio hilo limeathiri pia huduma ya umeme katika baadhi ya maeneo ya Tarafa ya Mbugwe.

Ofisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Manyara, Samuel Mandari amesema watu wasiojulikana walichoma nguzo ya umeme na kusababisha baadhi ya maeneo kukosa huduma hiyo.

“Watu wasiojulikana wamechoma nguzo ya Tanesco na tukio hilo limesababisha hasara kwa shirika na wakazi wa maeneo ya Magugu na jirani wamekosa huduma ya umeme,” amesema Mandari.

UBORA WA SHULE ZA ST DOMINIC SAVIO ,WAPONGEZWA NA WAZAZI

NA MATUKIO DAIMA MEDIA

IRINGA

WAZAZI wa wanafunzi wanaosoma katika Shule za St. Dominic Savio mkoani Iringa wamepongeza uongozi wa shule hizo kwa kuandaa ziara za kielimu zinazowawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kuongeza uelewa nje ya mazingira ya darasa.

Wazazi hao wamesema ziara hizo ni sehemu muhimu ya elimu, kwa kuwa zinawapa wanafunzi fursa ya kujionea na kuelewa kwa vitendo mambo wanayofundishwa darasani, ikiwemo historia, utamaduni na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi wengine, Shukuru Mpelele, mkazi wa Zanzibar, amepongeza juhudi za shule hiyo za kuwapeleka wanafunzi kutembelea maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuongeza maarifa na ujuzi.

“Wazazi tuna wajibu wa kuendelea kushirikiana na walimu katika kugharamia na kuunga mkono programu za kielimu kama hizi, kwa kuwa manufaa yake kwa watoto ni makubwa na yanaweza kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye,” alisema Shukuru.

Alisema fursa hizo zikienziwa na kuendelea kutolewa, wanafunzi wengi zaidi wataweza kujifunza mambo mbalimbali yanayoongeza maarifa na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za maisha ya baadaye.

Aidha, Shukuru ameipongeza St. Dominic Savio kwa kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia, kusimamia nidhamu na kuwa na walimu wanaowasimamia wanafunzi kwa karibu, akisema mambo hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kufanya vizuri kitaaluma.

Ziara hiyo imewashirikisha jumla ya wanafunzi 117 pamoja na walimu saba kutoka Shule ya St. Dominic Savio ya mkoani Iringa, ambao wameelekea Zanzibar kwa ziara ya kielimu yenye lengo la kuwapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo.

Wakati wa ziara hiyo, wanafunzi wanatarajiwa kutembelea maeneo mbalimbali yenye umuhimu wa kihistoria, kiutamaduni na kimazingira, huku wakipata fursa ya kujifunza moja kwa moja kutoka katika mazingira wanayoyatembelea.TAZAMA MAHOJIANO YOTE BOFYA LINK HII

Akizungumza na Matukio Daima, Mratibu wa Shule za St. Dominic, Mussa Myula, alisema ziara hiyo imehusisha makundi ya wanafunzi yanayoongozwa na walimu wao katika maeneo mbalimbali yaliyopangwa kwa ajili ya kujifunza.

Myula alisema miongoni mwa maeneo yatakayotembelewa ni misitu ya Zanzibar, ambapo wanafunzi watapata fursa ya kujifunza kuhusu mazingira, uhifadhi wa misitu na umuhimu wa rasilimali hizo katika maisha ya jamii.

“Ziara hii pia inalenga kuwafanya wanafunzi wajifunze historia ya Zanzibar kwa kujionea wenyewe maeneo mbalimbali ambayo wamekuwa wakiyasoma katika vitabu na masomo ya darasani,” alisema.

Alisema elimu ya darasani pekee haitoshi, hivyo wanafunzi wanapopewa nafasi ya kutembelea maeneo wanayojifunza, huwa rahisi kuelewa zaidi kile wanachofundishwa na kupata maarifa kupitia uzoefu wa moja kwa moja.

Kwa mujibu wa Myula, wanafunzi hao pia wanatarajiwa kukutana na viongozi pamoja na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya vijana Zanzibar, hatua ambayo itawapa fursa ya kujifunza namna vijana wanavyoshiriki katika shughuli za kijamii na maendeleo katika maeneo yao.

“Lengo kubwa la Shule ya St. Dominic katika kuandaa ziara kama hizi ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujifunza mazingira mapya, kufahamu historia na tamaduni za maeneo mbalimbali, pamoja na kupata ujuzi ambao unaweza kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye,” alisema Myula.

Aliongeza kuwa shule itaendelea kuwapa wanafunzi fursa za kutembelea maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, akisisitiza kuwa ziara za kielimu ni sehemu muhimu ya kuwasaidia watoto kupanua uelewa, kujifunza kwa vitendo na kutambua fursa mbalimbali zilizopo katika jamii.

KUJIUNGA NA SHULE ZETU TAZAMA HABA CHINI ⬇️⬇️

TANGAZO LA ST DOMINIC BOFYA HAPA