Aishi na Uvimbe Miaka 20 Aomba Msaada wa Matibabu, Afunguka Mazito -Video

Global Publishers
September 1, 2026
1,680 views
0 Comments

Usemi wa Kiswahili “Kabla hujafa hujaumbika” unaakisi kwa kiasi kikubwa maisha ya Ester Juma, mwenye umri wa miaka 32, mkazi wa Tabata Barakuda jijini Dar es Salaam, ambaye kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa akiishi na uvimbe mkubwa usoni.

Ester anapitia wakati mgumu huku akihangaika kutafuta fedha kwa ajili ya matibabu na upasuaji wa kuondoa uvimbe huo ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa maisha yake ya kila siku.

Akizungumza kuhusu hali yake, Ester amesema amekuwa akikumbana na changamoto mbalimbali anapokuwa katika maeneo ya umma. Anaeleza kuwa baadhi ya watoto humkimbia wanapomuona, huku wakati mwingine hata mtoto wake mwenyewe akimuogopa kutokana na mabadiliko ya sura yake.

Changamoto hiyo, amesema, imemfanya kuishi maisha yenye maumivu na msongo mkubwa huku akiwa na matumaini ya kupata msaada wa matibabu.

Ester amesema aliwahi kufika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupata matibabu, lakini hakufanikiwa kuanza mchakato huo baada ya kushindwa kupata Shilingi 450,000 zinazohitajika kwa ajili ya vipimo.

Kwa sasa, Ester anaendelea kuomba msaada kutoka kwa wasamaria wema ili aweze kupata fedha za vipimo na hatimaye kufanyiwa upasuaji.

Mtu yeyote aliyeguswa na hali ya Ester na angependa kumsaidia anaweza kuchangia kupitia namba 0760 780914, jina Magoli Juma.

Kifo cha Kichanga: Mahakama Yampa Mwanafunzi wa Miaka 18 Miezi 12

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imempa mwanafunzi wa chuo mwenye umri wa miaka 18 adhabu ya miezi 12 kwa kosa la kusababisha kifo cha kichanga baada ya kujifungua.

Mahakama hiyo imempa mshtakiwa huyo masharti ya kutotenda kosa lolote, kuwa na mwenendo mzuri na kuripoti kila mwezi katika Kituo cha Polisi Chang’ombe, Temeke, kwa kipindi cha miezi 12.

Adhabu hiyo imetolewa, Agosti 31, 2026, na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, chini ya Jaji Mkwizu.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Amedeus Malya, amesema mshtakiwa alikuwa akikabiliwa na kesi ya jinai ya Jamhuri dhidi yake, iliyohusu kosa la kusababisha kifo cha kichanga na kukitupa chooni, kosa linalojulikana kama Infanticide.

Malya amesema shtaka hilo lilikuwa chini ya Kifungu cha 199 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16, kama ilivyorekebishwa mwaka 2023.

TUKIO LA NOVEMBA 2025

Kwa mujibu wa maelezo ya kesi hiyo, tukio hilo lilitokea Novemba 11, 2025, katika eneo la Mambo Street, Temeke, Dar es Salaam.

Mshtakiwa, ambaye alikuwa mama wa kichanga hicho, alidaiwa kujifungua mtoto wa kiume.

Mahakama ilielezwa kuwa wakati wa tukio hilo, mshtakiwa alikuwa bado hajapona kikamilifu kutokana na kujifungua, huku hali yake ya akili ikiwa imevurugika kufuatia uzazi huo.

Baada ya kujifungua, alidaiwa kufanya vitendo vilivyosababisha mtoto huyo kupoteza maisha.

Mtoto huyo aligundulika na kupelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu, lakini licha ya juhudi zilizofanywa na madaktari, alifariki dunia.

MWILI WAFANYIWA POST-MORTEM

Baada ya mtoto huyo kufariki, mwili wake ulipelekwa kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu (post-mortem) ili kubaini chanzo na mazingira ya kifo chake.

Jeshi la Polisi liliendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo na baadaye mshtakiwa alikamatwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.

Mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, na kukabiliwa na shtaka la kusababisha kifo cha kichanga.

Baada ya mwenendo wa kesi hiyo, Mahakama imetoa adhabu ya miezi 12 chini ya masharti ya kutotenda kosa lolote, kuwa na mwenendo mzuri na kuripoti kila mwezi katika Kituo cha Polisi Chang’ombe, Temeke.

Tanzania Yapata Mwakilishi Algeria, Mabula Asaini Js Kabylie

Global Publishers
September 1, 2026
54 views
0 Comments

Kiungo wa Kimataifa wa Tanzania, Alphonce Mabula Msanga, ametambulishwa rasmi kuwa mchezaji mpya wa klabu ya JS Kabylie ya Algeria.

Mabula, mwenye umri wa miaka 23, amejiunga na JS Kabylie kwa uhamisho huru, baada ya kumalizika kwa mkataba wake na klabu ya Şamaxı FK ya Azerbaijan.

JS Kabylie imethibitisha rasmi kukamilika kwa usajili wa kiungo huyo, Agosti 31, 2026, kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Kabla ya kujiunga na JS Kabylie, Mabula alikuwa akihusishwa na Kasımpaşa ya Uturuki pamoja na Yanga.

Hata hivyo, klabu hiyo haijaweka wazi urefu wa mkataba ambao Mabula amesaini, hivyo bado haijafahamika atabaki Algeria hadi lini.

Kuhamia JS Kabylie kunakuwa hatua nyingine muhimu katika safari ya soka ya Mabula, ambaye sasa anaendelea kujenga uzoefu wake nje ya Tanzania.

Baada ya kumaliza kipindi chake akiwa Azerbaijan, kiungo huyo sasa anajiunga na moja ya klabu zinazojulikana nchini Algeria, akitarajiwa kuongeza nguvu katika eneo la kiungo la JS Kabylie.

Usajili huo pia unampa Mabula nafasi ya kuendelea kujenga uzoefu wa kucheza soka la ushindani barani Afrika baada ya kipindi chake cha kucheza Ulaya.

Mabula sasa anatarajiwa kuanza rasmi ukurasa mpya wa maisha yake ya soka akiwa ndani ya kikosi cha JS Kabylie.

Askari Polisi Afariki Akiwa Mahabusu Kituo Cha Polisi Tanga – Video

Global Publishers
September 1, 2026
1,536 views
0 Comments

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi.

Tanga — Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limethibitisha kifo cha askari wake, H.1796 Koplo Mwita, aliyekuwa akishikiliwa kwa ajili ya uchunguzi katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Tanga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, tarehe 27 Agosti 2026 majira ya saa 1:03 usiku, Koplo Mwita alifariki dunia akiwa ndani ya chumba cha mahabusu katika kituo hicho.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kabla ya kifo chake, marehemu pamoja na afisa mmoja na askari watano wa Jeshi la Polisi wa vyeo mbalimbali walikuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za kijinai.

Jeshi la Polisi limesema baada ya kifo hicho, uchunguzi wa kisayansi uliofanywa na ndugu wa marehemu kushuhudia umebaini kuwa chanzo cha kifo kilikuwa kukosa hewa kutokana na kujinyonga.

Aidha, mwili wa marehemu umebakizwa na ndugu zake kwa ajili ya taratibu za mazishi, huku Jeshi la Polisi likisema linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Katika taarifa hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limewataka wananchi, waandishi wa habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuepuka kuanzisha au kusambaza taarifa zisizothibitishwa, pamoja na kutoa hitimisho lisilotokana na matokeo rasmi ya uchunguzi.

Jeshi hilo limeeleza kuwa kufanya hivyo ni upotoshaji ambao ni kinyume cha sheria.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limesisitiza kuwa linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na litahakikisha taratibu zote za kiuchunguzi zinafuatwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Imetolewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tanga, Agosti 31, 2026.

Tottenham Yapigwa Chenga, Ndiaye Aelekea Man City Kwa Bilioni

Manchester City imefikia makubaliano na Everton kwa ajili ya kumsajili winga wa Senegal, Iliman Ndiaye, katika dili lenye thamani ya hadi TSh bilioni 227.5.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Manchester City italipa takribani TSh bilioni 210 kama ada ya msingi ya uhamisho, huku TSh bilioni 17.5 zaidi zikiwa kwenye mfumo wa nyongeza kulingana na vigezo vilivyowekwa kwenye dili hilo.

Ndiaye, mwenye umri wa miaka 26, alijiunga na Everton akitokea Marseille mwaka 2024 na sasa anakaribia kuanza sura mpya ya maisha yake ya soka akiwa na Manchester City.

TOTTENHAM ILIMTAKA NDIAYE

Kabla ya Manchester City kuingia kwenye dili hilo, Tottenham Hotspur ilikuwa imefikia makubaliano na Everton kwa ajili ya kumsajili Ndiaye.

Hata hivyo, mpango huo ulivurugika baada ya mshambuliaji wa Tottenham, Richarlison, kushindwa kufikia makubaliano binafsi na Everton kuhusu kurejea katika klabu yake ya zamani.

Everton ilikuwa imewasilisha ofa ya takribani TSh bilioni 122.5 kwa ajili ya Richarlison, lakini makubaliano hayakufikiwa.

Richarlison baadaye alitoa ujumbe wa kihisia kupitia Instagram, akisisitiza kuwa hataki tena watu wengine kuamua mustakabali wake.

Mchezaji huyo wa Brazil alisema licha ya vurugu hizo, bado yuko chini ya mkataba na Tottenham na ataendelea kuwa tayari kuitumikia klabu hiyo.

Usajili wa Ndiaye umeibuka baada ya mpango wa Manchester City kumnunua mshambuliaji wa Liverpool, Cody Gakpo, kwa takribani TSh bilioni 280, kuonekana kushindikana.

City ilikuwa imeanza mazungumzo na Liverpool kuhusu Gakpo, huku Liverpool ikiwa tayari kumuuza mchezaji huyo ikiwa tu ingefanikiwa kupata mbadala wake.

Liverpool tayari imekamilisha usajili wa mshambuliaji wa Ufaransa, Bradley Barcola, kutoka Paris St-Germain kwa dili linaloweza kufikia takribani TSh bilioni 430.5.

Hata hivyo, klabu hiyo ilikuwa bado inataka kuongeza mshambuliaji mwingine iwapo Gakpo angeondoka.

Liverpool ilikuwa imekuwa ikifuatilia uwezekano wa kuwasajili Yankuba Minteh wa Brighton na Ismaila Sarr wa Crystal Palace, lakini thamani iliyowekwa na vilabu hivyo imekuwa kikwazo.

Kutokana na hali hiyo, Liverpool inatarajiwa kumbakiza Gakpo isipokuwa kama itafanikiwa kupata winga mwingine kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

TOTTENHAM SASA YAMFUATILIA MUDRYK

Baada ya kupoteza dili la Ndiaye, Tottenham sasa imeelekeza nguvu zake kwa winga wa Chelsea, Mykhailo Mudryk.

Spurs ipo kwenye mazungumzo ya kumsajili Mudryk kwa mkopo wa msimu mzima.

Hivyo, dili la Ndiaye limebadili kwa kiasi kikubwa mipango ya vilabu kadhaa katika saa za mwisho za dirisha la usajili, huku Manchester City ikionekana kuwa mshindi wa mbio hizo baada ya kufikia makubaliano ya hadi TSh bilioni 227.5 na Everton.

Messi Atangaza Kustaafu Timu Ya Taifa Argentina Baada Ya Miaka 21

Taifa laArgentina, limepokea habari ya kushtua katika ulimwengu wa soka baada ya Lionel Messi kutangaza rasmi kustaafu timu ya taifa ya Argentina, akifunga ukurasa wa miaka 21 wa kuitumikia nchi yake. Messi ametangaza uamuzi huo kupitia ujumbe kwenye mitandao ya kijamii leo, Agosti 31, 2026.

Messi, mwenye umri wa miaka 39, amecheza mechi 207 akiwa na Argentina tangu alipocheza mechi yake ya kwanza mwaka 2005. Katika kipindi hicho, ameiongoza Argentina kushinda Kombe la Dunia 2022 pamoja na mataji mawili ya Copa América.

Amesema katika kipindi chote alichokuwa akichezea Argentina, alijitoa kwa moyo wote kwa ajili ya jezi hiyo, akilenga kuwapa furaha mashabiki na kuwafanya wajivunie kuwa Waargentina kupitia soka.

“Nimejitoa kila kitu, si katika miaka ya hivi karibuni ambayo tulishinda kila kitu, bali tangu mwanzo. Nilipambana na kujitoa kwa ajili ya jezi hii ili kuwapa furaha na kuwafanya mjivunie kuwa Waargentina kupitia soka,” amesema.

Mchezaji huyo amesema anajua kuwa hatua mbalimbali zinaanza kufungwa na kustaafu timu ya taifa ni moja ya hatua zinazomuumiza zaidi, akisisitiza kuwa ataendelea kuipenda Argentina licha ya kutokuwa sehemu ya kikosi.

Amesema amefikia hatua ambayo hana zaidi ya kutoa, huku akiamini kuwa kuna wachezaji vijana wenye uwezo mkubwa wanaokuja nyuma yake ambao wanastahili kupata nafasi katika timu ya taifa.

Pia amewashukuru mashabiki kwa upendo na sapoti waliompa kwa kipindi cha miaka 20, akisema atakikumbuka kwa hisia kubwa kipindi cha kuimba na kushangilia pamoja nao akiwa ndani ya uwanja.

Aidha, ametoa shukrani kwa familia yake, makocha, wachezaji wenzake na viongozi wote aliowahi kufanya nao kazi, akisema anabeba kumbukumbu na matukio yasiyosahaulika katika safari yake ya timu ya taifa.

Amesema anaondoka akiwa na amani na fahari kwa kuwa aliweza, pamoja na wachezaji wenzake, kuwapa mashabiki nyakati walizokuwa wakiziota.

Katika ujumbe huo, mchezaji huyo pia amesema maneno hayo aliyaandika Julai 21, siku mbili baada ya fainali, lakini baada ya kufariki kwa baba yake, amekuwa na uhakika zaidi kuhusu uamuzi wake wa kustaafu.

Amehitimisha ujumbe wake kwa kusema:

“Asante Mungu kwa kunifanya kuwa Muargentina. Vamos Argentina!”

Mambo Sita Usiyoyajua Kuhusu Faida na Hasara za Pilipili

Global Publishers
September 1, 2026
2,118 views
0 Comments

Pilipili ni kiungo kinachotumiwa sana kwenye vyakula mbalimbali kutokana na ladha yake ya ukali. Ina kemikali iitwayo capsaicin ambayo ndiyo husababisha hali ya kuwaka mdomoni na pia imehusishwa na baadhi ya faida za kiafya.

Faida za kula pilipili

1. Huongeza kinga ya mwili

  • Pilipili ina vitamini C na virutubisho vingine vinavyosaidia mwili kupambana na baadhi ya maambukizi.

2. Husaidia mmeng’enyo wa chakula

  • Pilipili inaweza kuchochea uzalishaji wa majimaji ya tumboni yanayosaidia mmeng’enyo wa chakula.

3. Inaweza kusaidia kudhibiti uzito

  • Capsaicin imehusishwa na kuongeza matumizi ya nishati mwilini na kupunguza hamu ya kula kwa baadhi ya watu.

4. Husaidia mzunguko wa damu

  • Baadhi ya tafiti zinaonyesha capsaicin inaweza kusaidia afya ya mishipa ya damu na mzunguko mzuri wa damu.

5. Inaweza kupunguza maumivu

  • Capsaicin hutumiwa pia kwenye baadhi ya krimu za matibabu kwa ajili ya kupunguza maumivu ya misuli au mishipa.

6. Huongeza ladha ya chakula

  • Pilipili hufanya chakula kiwe na ladha zaidi na inaweza kusaidia baadhi ya watu kula kwa hamu.

Nani anatakiwa kuwa makini na pilipili?

  • Watu wenye kiungulia cha mara kwa mara.
  • Wenye matatizo ya tumbo yanayochochewa na vyakula vyenye ukali.
  • Watoto wadogo ambao hawajazoea vyakula vya pilipili.
  • Watu wanaogundua kuwa pilipili huwazidishia dalili fulani.

Kula pilipili kwa kiasi kunaweza kuwa sehemu ya lishe yenye afya kwa watu wengi, lakini kula nyingi kupita kiasi kunaweza kusababisha usumbufu hasa kwa wenye tumbo nyeti.

TANZANIA, SERBIA KUIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI, KUPANUA FURSA

Tanzania na Serbia zimekubaliana kuanzisha Tume ya Pamoja ya Uchumi kwa lengo la kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo.

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), na Waziri wa Mambo ya Nje wa Serbia, Mhe. Marko Đurić, pembezoni mwa Mkutano wa Kumbukizi wa Ngazi ya Juu wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowore (NAM), unaofanyika jijini Belgrade, Serbia.

Katika kikao hicho cha Mawaziri hao wa Mambo ya Nje, Tanzania imeainisha fursa katika kilimo, madini, nishati, miundombinu, usafirishaji, utalii, uvuvi na uchumi wa buluu, huku Serbia ikieleza utayari wa kuwa lango kwa wafanyabiashara wa Tanzania wanaolenga masoko ya Ulaya.

Viongozi hao pia wamejadili kuimarisha ushirikiano kati ya Shirika la Ndege Tanzania ( ATCL) na Shirika la Ndege la Serbia (Air Serbia) pamoja na kuongeza muunganiko wa usafiri wa anga kati ya Tanzania na Serbia.

Katika hatua nyingine, Tanzania imepongeza uamuzi wa Serbia wa kuanzisha Ubalozi wa Kudumu jijini Dodoma, na kueleza utayari wake wa kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia, biashara na uwekezaji.

Mhe. Kombo amesema Tanzania iko tayari kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na Serbia, huku Serikali za nchi hizo zikiendelea na mchakato wa kuanzisha Tume ya Pamoja ya Uchumi.

Mazungumzo ya viongozi hao yalihusisha pia sekta binafsi, ambapo ujumbe wa Tanzania wenye takribani washiriki 20 upo nchini Serbia, huku zaidi ya kampuni 40 za Serbia zikitarajiwa kushiriki katika mazungumzo ya kibiashara ya pande mbili

 

Sauti ya kipekee iliyotoka katika familia ya muziki – HabariLeo

KATIKA safari ndefu ya muziki wa Bongo Fleva, yapo majina ambayo yameweza kujenga heshima kutokana na kipaji, ubunifu na uwezo wa kudumu katika mioyo ya mashabiki.Miongoni mwa majina hayo ni mwanamuziki Banana Zoro, anayekumbukwa kwa sauti yake ya kipekee, mtindo wake wa uimbaji na nyimbo zilizogusa maisha ya jamii. Banana Zoro si jina geni katika tasnia ya muziki nchini. Ni msanii aliyekulia katika mazingira ambayo muziki ulikuwa sehemu ya maisha ya familia yake, hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kujenga msingi wa safari yake katika sanaa.

Katika mahojiano maalumu na HabariLeo Digital, Banana anaeleza kuwa alianza kujihusisha na muziki akiwa kijana, akichochewa na mazingira ya familia yake yaliyokuwa yamezungukwa na sanaa.Baba yake mzazi, Mzee Zahir Ally Zoro, alikuwa mwanamuziki anayeheshimika katika muziki wa dansi nchini Tanzania. Mazingira hayo yalimfanya Banana kukua akiwa karibu na muziki, jambo lililomvutia na hatimaye kumshawishi kuamua kujenga safari yake mwenyewe katika tasnia hiyo.

‘Mama Yangu’ yamtambulisha

Jina la Banana Zoro lilizidi kupata umaarufu baada ya kutoa wimbo ‘Mama Yangu’, uliopokelewa vizuri na mashabiki kutokana na ujumbe wake wa upendo, shukrani na kuthamini nafasi ya mama katika maisha ya mwanadamu. Baada ya mafanikio hayo, aliendelea kutoa kazi mbalimbali zikiwamo ‘Nipo Radhi’, ‘Nzela’, ‘Mama Kumbena’, ‘Mapenzi Gani’ na ‘Zoba’. SOMA: Kila mzigo wa taifa unahitaji bega la mzalendo (2)

Kazi hizo zilionyesha uwezo wake wa kuimba na kuwasilisha hisia kupitia muziki, huku zikimsaidia kujenga nafasi yake miongoni mwa wasanii waliotamba katika vipindi tofauti vya muziki wa Tanzania. Uwezo wa Banana kuchanganya ladha za R&B, Zouk na Bongo Fleva pia ulimfanya kuwa msanii mwenye mashabiki wa rika tofauti. Katika safari yake, amefanya kazi mbalimbali na wasanii wengine, akichangia katika kukuza muziki wa kizazi kipya.

Muziki wa live band

Kwa sasa, Banana Zoro amejikita zaidi katika muziki wa live band, akitumbuiza katika hoteli, kumbi za harusi, sherehe za send-off pamoja na hafla mbalimbali za serikali na taasisi. Anasema muziki wa moja kwa moja umekuwa sehemu muhimu ya safari yake, huku akisisitiza umuhimu wa wasanii kujenga uwezo wa kuimba bila kutegemea playback. Katika kuzungumzia kizazi kipya cha wanamuziki, Banana anawapongeza wasanii wanaozingatia ubora wa kazi zao na wenye uwezo wa kuimba moja kwa moja. Miongoni mwa wasanii anaowakubali, anawataja Nandy, King Music na Vanilla, akisema anavutiwa na namna wanavyowasilisha kazi zao.

Nidhamu ndiyo msingi

Kwa Banana Zoro, safari ndefu katika muziki haijajengwa na kipaji pekee. Anasema siri ya kudumu katika muziki na kuiongoza bendi yake kwa miaka mingi ni nidhamu ya kazi, kuheshimu mikataba na kujenga uaminifu kwa mashabiki pamoja na waandaaji wa matamasha. Anaeleza kuwa amekuwa akijenga uhusiano mzuri na wanamuziki anaofanya nao kazi na kuwasaidia kutimiza ndoto zao, licha ya baadhi yao kuondoka na kuendelea na miradi au fursa nyingine. Kwa upande wa mashabiki, Banana anasema amekuwa akipokea kwa upendo ishara mbalimbali za mapenzi kutoka kwao, hasa wanapomfuata baada ya maonesho au kwenye matamasha.

Mitandao imebadilisha muziki

Kama ilivyo kwa sekta nyingine, muziki umebadilika kutokana na ukuaji wa teknolojia na mitandao ya kijamii. Banana anasema TikTok, Instagram na YouTube ni miongoni mwa majukwaa yaliyobadilisha namna wasanii wanavyowafikia mashabiki. Anasema tofauti na zamani, ambapo redio na televisheni zilikuwa miongoni mwa njia kuu za kusambaza kazi za wasanii, sasa msanii anaweza kuwafikia mashabiki moja kwa moja kupitia mitandao hiyo. Hata hivyo, anasisitiza kuwa umaarufu wa wasanii wa zamani haupaswi kupuuzwa, kwa kuwa wengi walifanikiwa kujenga majina makubwa bila kutegemea mitandao ya kijamii iliyopo leo.

Ushauri kwa vijana

Kwa wasanii chipukizi wanaotaka kujenga safari ndefu katika muziki, Banana anawataka kuzingatia matumizi sahihi ya lugha katika utunzi wa nyimbo. Anasema matumizi ya misamiati ya muda mfupi na maneno yanayoweza kupoteza maana kadri miaka inavyosonga yanaweza kuathiri uimara wa kazi za wasanii. Kwa mtazamo wake, kazi nzuri ni ile inayoweza kusikilizwa leo na bado ikaendelea kuwa na maana kwa kizazi kijacho. Pia amesema yeye na timu yake wanaendelea kuunga mkono vipaji vya vijana kwa lengo la kuandaa kizazi kipya cha wasanii wa Bongo Fleva.

Urithi wa familia

Banana Zoro anatoka katika familia yenye historia kubwa katika muziki wa Tanzania. Alizaliwa pamoja na dada yake, Maunda Zoro, ambaye naye aliwahi kujulikana katika tasnia ya muziki kabla ya kufariki. Historia hiyo imeendelea kuwa sehemu ya utambulisho wa Banana, ambaye amebeba urithi wa familia huku akijenga jina lake mwenyewe katika muziki wa Tanzania. Mbali na muziki, Banana Zoro pia amejihusisha na uigizaji na kwa sasa ni sehemu ya tamthilia ya Huba. Katika maisha yake binafsi, Banana ni baba wa watoto watatu, wavulana wawili na msichana mmoja. Anasisitiza umuhimu wa kulinda familia na kutenganisha maisha binafsi na kazi.

Safari bado inaendelea

Leo, Banana Zoro anaendelea kuwa sehemu ya historia ya muziki wa Tanzania.Kutoka katika familia iliyobeba muziki kwa miaka mingi hadi kujenga safari yake mwenyewe, msanii huyo amedhihirisha kuwa kipaji pekee hakitoshi, bali kinahitaji kuambatana na nidhamu, ubunifu na uvumilivu. Safari yake ni simulizi ya msanii aliyerithi muziki kutoka katika familia, lakini hakubaki kuwa mrithi wa jina pekee. Alitengeneza sauti yake, akajenga mashabiki wake na kuacha alama yake katika muziki wa Tanzania.