Rais Mwinyi Atangaza Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, ACT-Wazalendo Yapata Nafasi Nne

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, hatua inayokamilisha uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kuwajumuisha viongozi kutoka Chama cha ACT-Wazalendo.

Mabadiliko hayo yametangazwa leo, Oktoba 3, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu Zanzibar.

Katika mabadiliko hayo, ACT-Wazalendo imepata nafasi nne za uwaziri.

Mawaziri hao ni Nassor Ahmed Mazrui, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Afya; Omar Said Shaaban, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda; Dkt. Nasra Nassor Omar, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale; pamoja na Dkt. Mohamed Ali Suleiman, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu.

Aidha, Rais Mwinyi ametangaza mabadiliko ya muundo wa baadhi ya Wizara, ikiwa ni pamoja na kuhamishia masuala ya Mipango katika Ofisi ya Rais, Ikulu, pamoja na kuanzishwa kwa Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji.

Katika mabadiliko hayo, Shaaban Ali Othman ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, anayeshughulikia Mipango na Usimamizi wa Utendaji Serikalini.

Masoud Ali Mohamed ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, anayeshughulikia Uhusiano wa Jamii.

Mudrik Ramadhan Soraga amepewa nafasi ya Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, huku Ali Suleiman Ameir Mrembo akiteuliwa kuwa Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji.

Mabadiliko hayo pia yamewagusa Naibu Mawaziri katika Wizara mbalimbali, zikiwemo Afya, Kilimo, Elimu, Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Fedha, Utalii na Mambo ya Kale, pamoja na Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji.

Akizungumza wakati akitangaza mabadiliko hayo, Rais Mwinyi amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya maridhiano kati ya CCM na ACT-Wazalendo kuhusu uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mawaziri na Naibu Mawaziri wote walioteuliwa na waliohamishwa wanatarajiwa kuapishwa Jumatatu, Oktoba 5, 2026, saa 8:00 mchana.

Moto wa Nations League: Nani Atatoka na Tabasamu?

Wakali wa ubashiri Tanzania wanazidi kukukumbusha kuwa pesa hapa hazikauki, unachotakiwa kufanya wewe ni kutengeneza jamvi lako la ushindi na ubeti sasa. Ufaransa, Ubelgiji, Uturuki na wengine wapo kwaajili yako.

Pointi 3 kugombaniwa kwenye mchezo wa Czechia dhidi ya Hispania ambao unaonekana kuwa na tofauti kubwa kwenye ubora na mwenendo wa timu hizi. Hispania inaingia kwenye mchezo ikiwa kileleni kwenye Kundi A3 kwa pointi sita baada ya kuifunga Uingereza 3-2 na Croatia 4-1, huku Czechia ikiwa bado haina pointi baada ya kupoteza dhidi ya Croatia na Uingereza.

Hispania iko kwenye kiwango kizuri sana, hasa kwenye safu ya ushambuliaji. Lamine Yamal ndiye mchezaji anayevutia zaidi machoni baada ya kufunga mabao mawili na kutoa assist dhidi ya Croatia.

Kasi yake, uwezo wa kucheza mmoja dhidi ya mmoja na ubunifu wake vinaweza kuwa tatizo kubwa kwa ulinzi wa Czechia. Zaidi ya hapo, Hispania ina viungo wenye uwezo wa kutawala mpira kama Pedri, Rodri na Fabián Ruiz, hivyo inaweza kuilazimisha Czechia kutumia muda mwingi bila mpira. Suka jamvi hapa na Meridianbet.

Pesa ipo kupitia michezo ya Kasino ya Mtandaoni kama vile, Keno, Aviator, Poker, Roulette, Wild Icy Fruits, Super Heli na mingine kibao. Jiunge leo kwa kutembelea tovuti ya meridianbet.co.tz au piga *149*10# kisha uanze safari yako ya ushindi.

Kwa Czechia, changamoto kubwa ni kwamba wanahitaji kubadili kabisa mwenendo wao. Wamepoteza mechi mbili za kwanza na wamefunga bao moja pekee. Pia watamkosa Pavel Šulc, ambaye alitolewa kwa kadi nyekundu dhidi za Uingereza. Hilo linaweza kupunguza zaidi ubunifu wao mbele.

Hispania ndiyo timu yenye nafasi kubwa zaidi ya kushinda, lakini Czechia ikiwa itadhibiti dakika za mwanzo inaweza kuifanya mechi iwe ngumu. Natarajia Hispania kutawala mpira, kutengeneza nafasi nyingi na hatimaye kupata ushindi.

Mechi nyingine ni hii ya Croatia dhidi ya Uingereza ambao wanakutana kwenye mchezo muhimu wa UEFA Nations League, ambapo vijna wa Tuchel wanaingia uwanjani wakiwa na morali ya hali ya juu baada ya kupata ushindi wao mechi iliyopita dhidi ya Czechia.

Croatia inatoka kwenye kipigo kizito cha 4-1 dhidi ya Hispania hivyo, kwa Croatia huu ni mchezo wa kurekebisha makosa na kujirudisha kwenye ushindani, wakati Uingereza wanataka kuendeleza momentum baada ya kuanza kampeni kwa kupoteza 3-2 dhidi ya Hispania.

Uingereza wanaonekana kuwa na faida kwenye ubora wa safu ya ushambuliaji wakiongozwa na mshambuliaji wao Harry Kane ambao bado ni silaha kubwa katika eneo la mwisho, huku Anthony Gordon akiwa katika hali nzuri baada ya kufunga dhidi ya Czechia. Jude Bellingham, Bukayo Saka na Morgan Rogers pia wanaweza kuleta kasi na ubunifu, hivyo Croatia itahitaji kuwa makini sana inapopoteza mpira. Jisajili hapa.

Wakati Croatia wao wana wachezaji wenye uzoefu mkubwa pia kama vile Luka Modrić, Mateo Kovacic na Ivan Perisic bado unaweza kuwa muhimu katika kudhibiti mchezo.

Timu hiyo imetoka kupokea kipigo cha 4-1 dhidi ya Hispania kilionyesha kwamba wanapobanwa na timu yenye ubora mkubwa, safu yao ya ulinzi inaweza kuachwa wazi.

Uingereza pia wanahitaji kuwa makini kwa sababu ushindi wao wa Czechia haukuwa mchezo mwepesi kabisa; walisaidiwa na Czechia kubaki na wachezaji 10 tangu dakika ya 23. Croatia, ikiwa na wachezaji 11 na ikicheza kwa nidhamu, inaweza kuwa mtihani mkubwa zaidi kwa Tuchel. Bashiri hapa.

SPIKA ZUNGU AFUNGUA KIKAO CHA KAMATI TENDAJI YA IPU JIJINI ARUSHA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amefungua kikao cha Kamati Tendaji ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kilichofanyika leo tarehe 3 Oktoba, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Spika Zungu amewakaribisha wajumbe hao jijini Arusha na kuwahakikishia kuwa maandalizi yote kuelekea Mkutano Mkuu wa IPU yamekamilika na kwamba Tanzania inajivunia kwa mkutano huu mkubwa wa kibunge duniani kufanyika hapa nchini na kwenda kujadiliana masuala mbalimbali yanayoikumba dunia.

Katika hotuba yake, Spika Zungu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira wezeshi na utekelezaji madhubuti uliofanikisha maandalizi na uratibu wa mkutano huo mkubwa nchini.

Vilevile, amempongeza Rais wa IPU (ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, kwa uongozi wake thabiti, imara na madhubuti katika kipindi chote cha miaka mitatu ya uongozi wake kwenye umoja huo.

Kabla ya kuhitimisha maelezo yake, Spika Zungu amewasihi wajumbe wote kutumia fursa hiyo kutembelea na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo jijini Arusha na kote nchini Tanzania.

Kikao hicho cha Kamati Tendaji kimeongozwa rasmi na Rais wa IPU, Mhe. Dkt. Tulia Ackson.

Kikao hicho cha Kamati Tendaji ya IPU ni maalum kuelekea kuanza kwa Mkutano wa 153 wa IPU kesho Oktoba 04, 2026 ambapo itawakutanisha washiriki 2,000 kutoka nchi wanachama 183 wa IPU wakiwemo Maspika, Makatibu, Wabunge na Maafisa mbalimbali.

 

MAKAMU WA RAIS AWASILI MISRI KUMWAKILISHA RAIS KATIKA MKUTANO WA NANE WA NUSU MWAKA WA UMOJA WA AFRIKA (AU)

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amewasili Jijini New Alamein nchini Misri kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Nane wa Uratibu wa Katikati ya Mwaka wa Umoja wa Afrika (8th African Union Mid-Year Coordination Summit) pamoja na mikutano mingine ya ngazi ya Juu ya Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda.

 

Mkutano huo unafanyika katika mji wa New Alamein, nchini Misri kuanzia tarehe 02 Oktoba 2026, chini ya kaulimbiu “Africa on the Land of El Alamein.”

 

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Al Alamein, Makamu wa Rais amepokelewa na Waziri wa Michezo na Vijana wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Gohar Nabil, Balozi wa Tanzania nchini Misri Mhe. Meja Jenerali Richard Makanzo, pamoja na maafisa mbalimbali wa Serikali ya Misri na Tanzania.

 

Mara baada ya kuwasili, Mhe. Makamu wa Rais amepokea taarifa kuhusu maandalizi ya Tanzania kushiriki mkutano huo, ambao unawakutanisha viongozi wa juu wa nchi 15 wanachama wa Umoja wa Afrika na Taasisi mbalimbali za Kimataifa na Kikanda kwa lengo la kujadili na kuratibu masuala muhimu yanayohusu maendeleo na ushirikiano wa Bara la Afrika.

 

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano wake ndani ya Umoja wa Afrika na kuchangia katika mijadala kuhusu utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Bara la Afrika, ikiwemo uchumi, amani, usalama na ushirikiano miongoni mwa mataifa ya Afrika.

 

Makamu wa Rais anamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo, ikiwa ni mwendelezo wa Tanzania kushiriki katika majukwaa ya kikanda na kimataifa yanayojadili masuala yenye maslahi kwa Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

03 Oktoba 2026

Alamein – Misri.

 

DKT. MWIGULU AAGIZA UCHUNGUZI WA MAJENGO YA HOSPITALI YA WILAYA YA BUNDA YALIYOTITIA

*_▪︎ Aagiza wahusika kuwajibishwa iwapo uzembe utathibitika_*

*_▪︎ Aelekeza kodi ya klinka iondolewe ili kupunguza bei ya saruji_*

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza kupatiwa taarifa za uchunguzi kuhusu majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Bunda yaliyotitia, akitaka hatua zichukuliwe dhidi ya waliohusika iwapo itathibitika kuwa kulikuwa na uzembe.

Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo, Jumamosi, Oktoba 3, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika Nyamuswa, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, baada ya kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bunda.

“Nimeambiwa Waziri wa Afya alishatengeneza timu na ikafanya kazi na TAKUKURU ameshafanyia kazi. Nizipate hizo taarifa ili hawa waliofanya makosa haya wawajibike kule kule walipo. Lazima wawajibike. Hii kuharibu wilaya hii na kuhamishiwa ukaharibu na wilaya nyingine, hii haikubaliki,” amesema.

Amesema wakati wa ukaguzi huo amekuta majengo mawili yakiwa yametitia na kupewa maelezo kuwa hali hiyo imesababishwa na uwepo wa maji katika eneo la mradi pamoja na udongo wa mfinyanzi.

“Namuuliza kwa nini majengo yametitia? Wanasema kwa sababu yamejengwa karibu na chanzo cha maji. Chanzo cha maji kile kimekuja baada ya kujenga msingi? Si kilikuwepo pale pale? … Wanasema udongo huu ni wa mfinyanzi,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kufuatilia suala hilo ili kubaini ukweli wa kilichosababisha majengo hayo kutitia na kuhakikisha wananchi hawapati adhabu kutokana na uzembe katika utekelezaji wa miradi ya Serikali.

Amesema Serikali pia inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha maeneo yaliyobaki ya ujenzi wa hospitali hiyo ili wananchi waendelee kupata huduma za afya katika eneo lao.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na kupanda kwa bei ya saruji, ikiwemo kuelekeza kuondolewa kwa kodi kwenye klinka, malighafi inayotumika katika uzalishaji wa saruji.

“Nimewaelekeza Mamlaka ya Mapato waondoe kodi kwenye klinka, malighafi inayotumika kwenye uzalishaji wa saruji ili upatikanaji wa saruji uwe wa uhakika na bei iweze kuwa bei himilivu,” amesema.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha upatikanaji wa saruji unaendelea kuwa wa uhakika na bei yake inakuwa himilivu kwa wananchi, akibainisha kuwa katika baadhi ya maeneo bei imekuwa ikipanda hadi kufikia zaidi ya Sh. 25,000, Sh. 27,000 na katika baadhi ya mikoa kufikia Sh. 32,000 kwa mfuko.

Kuhusu huduma za afya, Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa wananchi hawapaswi kuchangishwa fedha za mafuta kwa ajili ya magari ya Serikali, hususan magari ya wagonjwa yanayotumika kuokoa maisha.

“Hatuwezi tukawa na magari ya Serikali yana mafuta, halafu ambulance ya kunusuru maisha ya wagonjwa tuchangishane mafuta. Haya ni mambo ya mazoea ambayo hatutaki kuwa utaratibu wa Serikali,” amesema.

Amesema mwananchi yeyote atakayeombwa fedha za mafuta kwa ajili ya gari la wagonjwa anatakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.

Dkt. Mwigulu pia amesisitiza umuhimu wa wagonjwa walio katika hali mbaya kupewa huduma ya dharura mara moja kabla ya kukamilisha taratibu nyingine za kiutawala.

“Mgonjwa aliyezidiwa amefika, hatua ya kwanza apelekwe moja kwa moja kwenye kitanda apate huduma. Hata kumwandikisha mtamwandikisha akiwa ameshapata huduma ya kwanza. Kanusuru kwanza maisha yake. Usifanye itifaki kwenye maisha,” amesema.

Kuhusu upatikanaji wa dawa, amesema Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba, hivyo amewataka viongozi na watendaji wa afya kuhakikisha dawa zinawafikia wananchi waliokusudiwa na matumizi yake yanafuatiliwa ipasavyo.

Hospitali ya Wilaya ya Bunda ilianza kutekelezwa tarehe 8 Mei, 2019, ikiwa ni miongoni mwa hospitali 67 za awamu ya kwanza za halmashauri zilizolenga kusogeza huduma za afya za ngazi ya hospitali karibu na wananchi. Hadi sasa, Serikali imetoa jumla ya Sh. bilioni 5.39 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Hospitali hiyo imeanza kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo huduma za wagonjwa wa nje, maabara, afya ya uzazi na mtoto, kujifungua, radiolojia, kulaza wagonjwa, huduma za macho, meno na huduma za dharura.

DKT. MWIGULU AKAGUA MRADI WA HOSPITALI YA WILAYA YA BUNDA.

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Oktoba 03, 2026 amekagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara ambapo mpaka sasa kiasi cha shilingi bilioni 5.3 kimeshatolewa hadi sasa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo, Dkt. Mwigulu amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua kazi kubwa inayofanywa na watumishi katika sekta ya afya kwenye kuwahudumia Watanzania.

Aidha, Dkt. Mwigulu amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kuboresha mazingira ya huduma za afya. 

“Lakini pia tutaendelea kuboresha na kuhakikisha kwamba watumishi hawakwamishwi na vitendea kazi wala mazingira ya kazi katika uhudumiaji katika sekta hiyo ya afya”.

Lengo kuu la mradi huo ni kutoa huduma za ngazi ya Hospitali ambazo hazikua zikipatikana maeneo haya na wananchi walilazimika kuzifuata mbali kama Bunda Mjini au Mugumu-Serengeti .

 

Trump Akabiliwa na Kesi Mpya Mahakama ya Juu Marekani

WASHINGTON: Rais wa Marekani, Donald Trump, anatarajiwa kukabiliwa na mfululizo wa kesi katika Mahakama ya Juu ya Marekani wakati muhula mpya wa mahakama hiyo wa miezi tisa unapoanza, huku baadhi ya kesi zikihusu mipaka ya mamlaka ya rais na sera zake za uhamiaji.

Mahakama hiyo yenye majaji tisa, ikiwa na majaji sita wenye misimamo ya kihafidhina dhidi ya watatu, ilimaliza muhula wake uliopita Juni ikiwa imetoa maamuzi yaliyompa Trump ushindi katika baadhi ya masuala, huku pia ikimzuia katika sera nyingine.

Katika muhula mpya, mahakama tayari imekubali kusikiliza kesi mbili muhimu zinazohusiana na sera kali za Trump kuhusu uhamiaji na mpango wa kuwafukuza wahamiaji kwa wingi.

Moja ya kesi hizo inahusu sera ya kuwazuia baadhi ya wahamiaji bila kuwapa nafasi ya kusikilizwa kuhusu dhamana, huku nyingine ikihusu mamlaka ya Serikali kuwapeleka watu wanaofukuzwa nchini Marekani katika nchi nyingine badala ya nchi zao.

Utawala wa Trump pia umepeleka mbele ya Mahakama ya Juu rufaa zinazohusu marufuku ya watu waliobadili jinsia kuhudumu katika jeshi, kupunguzwa kwa ruzuku za utafiti wa kitaaluma, uteuzi wa waendesha mashtaka wa shirikisho pamoja na kusimamishwa kwa maombi ya hifadhi katika mpaka wa Marekani na Mexico.

Mahakama hiyo inatarajiwa kuamua katika kipindi kijacho ni kesi zipi kati ya hizo itazisikiliza.

Mamlaka ya Rais Yaendelea Kuwa Mjadala

Katika kipindi cha utawala wa Trump, Mahakama ya Juu imekuwa ikikabiliwa na kesi zinazohusu matumizi makubwa ya mamlaka ya urais.

Profesa wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Syracuse, Jenny Breen, amesema mahakama hiyo imekuwa ikiruhusu kwa kiasi kikubwa juhudi za utawala wa Trump kupanua wigo wa mamlaka ya rais.

Hata hivyo, Trump pia amepata baadhi ya vikwazo mahakamani.

Katika muhula uliopita, majaji walizuia sera yake ya ushuru mpana kwa bidhaa zinazoingia Marekani, hatua dhidi ya gavana wa Benki Kuu ya Marekani (Federal Reserve), pamoja na juhudi za kubadilisha sheria kuhusu uraia wa kuzaliwa.

Mahakama pia ilizuia hatua ya Trump ya kupeleka wanajeshi wa National Guard katika eneo la Chicago.

Pamoja na maamuzi hayo, Mahakama ya Juu imeendelea kuruhusu utekelezaji wa baadhi ya sera za Trump wakati kesi kuhusu uhalali wake zikiendelea katika mahakama za chini.

Miongoni mwa sera hizo ni hatua za uhamiaji, sera zinazowahusu watu waliobadili jinsia na kupunguzwa kwa baadhi ya ruzuku za utafiti.

Katika uamuzi muhimu wa mwaka uliopita, mahakama pia ilipanua mamlaka ya rais juu ya baadhi ya taasisi huru za Serikali, hatua iliyobadili kwa kiasi kikubwa tafsiri ya mipaka ya mamlaka ya urais.

Profesa wa Harvard Law School, Daphna Renan, amesema katika mazingira ambayo Mahakama ya Juu imewahi kumpinga Trump, mara nyingi imefanya hivyo kwa kutekeleza sheria zilizopitishwa na Congress.

Trump Awakosoa Majaji Aliowateua

Trump mwenyewe amekuwa akikosoa baadhi ya maamuzi ya majaji waliowahi kuteuliwa na yeye katika muhula wake wa kwanza.

Katika kipindi cha hivi karibuni, amewakosoa majaji Neil Gorsuch, Brett Kavanaugh na Amy Coney Barrett, akidai hawajaendelea kuwa waaminifu kwake kama alivyotarajia. Trump pia amesema anajutia kuwateua baadhi yao.

Uteuzi wa majaji hao uliimarisha idadi ya majaji wenye misimamo ya kihafidhina katika Mahakama ya Juu, ambayo tangu mwaka 2020 imekuwa ikitoa maamuzi yaliyobadili sera mbalimbali za Marekani, ikiwemo haki za utoaji mimba, umiliki wa silaha, haki za kidini na mamlaka ya taasisi za Serikali.

Kesi Nyingine Mbele ya Mahakama

Miongoni mwa kesi zinazoweza kuendelea kuipa Mahakama ya Juu nafasi ya kuamua kuhusu mipaka ya mamlaka ya Trump ni ile inayohusu marufuku ya watu waliobadili jinsia kuhudumu katika jeshi la Marekani.

Katika kesi nyingine inayotarajiwa kusikilizwa, utawala wa Trump unaunga mkono changamoto dhidi ya sheria za jimbo la Washington zinazolinda haki za watoto waliotoroka makwao ambao ni transgender na wanaotafuta huduma za afya zinazohusiana na mabadiliko ya kijinsia katika vituo vya hifadhi.

Aidha, kesi inayotarajiwa kusikilizwa Desemba inahusu changamoto dhidi ya sheria za majimbo zinazoweka vikwazo kwa umiliki wa bunduki aina ya assault-style rifles.

Kesi hizo zinaweza kuongeza mjadala kuhusu mgawanyo wa mamlaka kati ya Rais, Congress na Mahakama, huku Mahakama ya Juu ikiendelea kuamua kiwango ambacho sera za utawala wa Trump zinaweza kutekelezwa chini ya Katiba na sheria za Marekani.

Kyle Simbwa Aibuka Msanii Mpya wa Apple Music Afrika Mashariki

KAMPUNI kubwa ya muziki duniani, Apple Music, imemtangaza mwanamuziki kutoka Uganda, Kyle Simbwa, kuwa msanii mpya wa programu yake ya Up Next Afrika Mashariki, hatua inayompa nafasi ya kuonekana zaidi katika jukwaa la muziki la kimataifa.

Simbwa anatokea Kasangati, mji mdogo uliopo nje ya Kampala, Uganda, na amekuwa akijenga muziki wake kwa kuchota msukumo kutoka katika aina mbalimbali za muziki, ikiwemo R&B na Soul za miaka ya 1990, Synth-pop ya miaka ya 1980, A.O.R., muziki wa Disney TV, Afrobeats na Hip-Hop.

Mchanganyiko huo wa vyanzo tofauti vya muziki umemsaidia kujenga sauti yake inayochanganya Afrobeat na Alté, huku akijikita katika kutengeneza mtindo unaomtambulisha kama msanii wa kizazi kipya cha Afrika Mashariki.

Akizungumza na Apple Music kuhusu kuchaguliwa kwake kwenye mpango wa Up Next Afrika Mashariki, Simbwa amesema hatua hiyo ina maana kubwa kwake na anaamini inawakilisha kizazi kipya cha wasanii wa Afrika wanaojenga utambulisho wao kupitia muziki.

“Kuchaguliwa kwenye Up Next Afrika Mashariki na Apple Music kunamaanisha mengi kwangu kwa sababu mimi ni sehemu ya kizazi cha wasanii wa Kiafrika kinachojenga kitu ambacho ni chetu kipekee,” amesema Simbwa.

Ameongeza kuwa anatamani muziki wake uwafikie watu wengi zaidi na kuwafanya waelewe chimbuko lake la kisanii.

“Nataka watu wasikie muziki wangu, wahisi ninakotoka, na waone jinsi unavyoweza kusafiri mbali,” amesema.

Akizungumzia mipango yake ya mwaka 2026, Simbwa amesema analenga kuongeza kasi katika kazi zake za muziki na kuendelea kuiwakilisha Uganda pamoja na Afrika Mashariki katika majukwaa makubwa.

“2026 ni wa kuchukua kila kitu nilichokuwa nakijenga na kukisukuma mbele zaidi. Rekodi zaidi, kufuatilia mawazo makubwa zaidi, na kuendelea kuiwakilisha Uganda na Afrika Mashariki kwenye jukwaa kubwa zaidi,” amesema.

Simbwa pia anahusika kwa karibu katika hatua mbalimbali za utengenezaji wa muziki wake, kuanzia uandishi wa nyimbo, utayarishaji, urekodi hadi uchanganyaji.

Ushiriki huo wa moja kwa moja katika mchakato wa ubunifu umempa nafasi ya kujaribu mitindo mbalimbali na kuendelea kukuza sauti yake binafsi.

Baada ya kuachia mradi wake wa kwanza, “Person,” mwaka 2025, Simbwa ameendelea kujenga katalogi yake kupitia nyimbo kama “Mwana Gwe,” “Love Me or Don’t,” na “East African Girl.”

Ukuaji wake katika upande wa maonyesho ya moja kwa moja pia umeendelea kuonekana, ikiwa ni pamoja na kutumbuiza katika Xpressions na Afro Urban, ambako amepata nafasi ya kushirikiana jukwaani na wasanii kama Mike Kayihura na Kohen Jaycee.

Kwa sasa, Simbwa anaanza sura mpya ya safari yake ya muziki kupitia “East African Summer,” EP yenye nyimbo saba inayogusa mada za mapenzi, maisha ya usiku, uhuru, safari na uzoefu wa pamoja unaoendelea kuunda utamaduni mpya wa vijana wa Afrika Mashariki.

Kupitia uteuzi huo wa Apple Music, Simbwa anaingia katika hatua mpya ya safari yake ya muziki huku akilenga kuitambulisha sauti yake na ya Afrika Mashariki kwa hadhira pana zaidi.

SERENGETI RALLY 2026 YAZINDULIWA MOROGORO GARI 24 KUTIMUA VUMBI

 

Na Lilian Kasenene, Morogoro

Matukio Daima Media 

Mashindano ya mbio za magari ya Serengeti Rally of Tanzania 2026 yamezinduliwa rasmi mkoani Morogoro, huku magari zaidi ya 24 yakitarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho katika viwanja vya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), eneo la Msitu wa Shamba la Miti Morogoro.

Uzinduzi wa mashindano hayo umefanyika katika Kiwanda cha Serengeti na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Mhe. Mussa Kilakala, ambaye amewataka washiriki na watazamaji kuzingatia usalama wakati wote wa mashindano.

Mhe. Kilakala pia amesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira, akiwataka washiriki, mashabiki na wananchi wanaokwenda kushuhudia mashindano hayo kuhakikisha shughuli zao haziathiri uoto wa asili na mazingira ya Msitu wa Shamba la Miti Morogoro.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Kamishna Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Uzalishaji Mbegu za Miti, Dkt. Hamza Kateti, amesema TFS itaendelea kusimamia na kulinda mazingira katika maeneo ya misitu, ambayo ni muhimu kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Dkt. Kateti amewahimiza wananchi kutumia fursa ya mashindano hayo kujifunza kuhusu uhifadhi na kufanya utalii wa ikolojia kwa kutembelea hifadhi na maeneo mbalimbali ya asili yanayopatikana mkoani Morogoro na yanayosimamiwa na TFS.

Kwa upande wa madereva, wameeleza kuridhishwa na hali ya njia iliyotumika katika maandalizi ya mashindano hayo, wakisema ina changamoto zinazohitajika katika mbio za magari na hivyo kutoa nafasi ya ushindani.

Dereva Kartik Valambia, anayeshiriki katika mashindano hayo, amesema njia hiyo imewaandaa vizuri madereva na kutoa fursa ya kuonyesha uwezo wao wa kuendesha magari katika mazingira yenye changamoto.

Naye dereva Tufail Amin amesema ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa kutokana na ubora na changamoto za njia, huku kila dereva akiingia kwenye mashindano akiwa na mkakati wa kufanya vizuri.

Mashindano hayo yanashirikisha zaidi ya magari 24, ambapo magari tisa yanashiriki katika African Rally Championship (ARC). 

Timu kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia na India zinashiriki katika mashindano hayo yanayofanyika katika maeneo ya TFS mkoani Morogoro.

Magari hayo yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho , huku mashabiki wakitarajia kushuhudia ushindani mkubwa katika njia zenye changamoto za Msitu wa Shamba la Miti Morogoro

Shigongo Awataka Watanzania Kulinda Amani na Umoja – Video

Global Publishers
October 3, 2026
84 views
0 Comments

Mbunge wa Buchosa, Erick James Shigongo

BUCHOSA, MWANZA: Mbunge wa Buchosa, Erick James Shigongo, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano uliopo nchini, akisisitiza kuwa wananchi wote ni ndugu bila kujali tofauti zao za kisiasa, kidini au kikabila.

Shigongo ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi uliofanyika katika Kijiji cha Bulyahilu, Kata ya Iligamba, Jimbo la Buchosa.

Amesema amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, hivyo wananchi wana wajibu wa kuilinda na kuhakikisha tofauti zinazoweza kujitokeza hazivunji umoja wao.

“Watanzania wote ni ndugu,” amesema Shigongo, akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na kuheshimiana katika shughuli zao za kila siku.

Aidha, ametoa wito kwa vyama vya siasa kushirikiana kwa maslahi ya taifa, akisisitiza umuhimu wa kuweka mbele masuala yanayowagusa wananchi na maendeleo ya nchi.

Mbunge huyo amewataka pia wananchi kutobaguana kwa misingi ya dini wala kabila, bali kuendelea kujenga jamii inayozingatia umoja, mshikamano na kuheshimiana.

Shigongo ni Mbunge wa Jimbo la Buchosa na amekuwa akifuatilia masuala mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo kupitia shughuli za Bunge na mikutano na wananchi.