WATU SABA WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA AFISA ARDHI KILOMBERO

Na Matukio Daima Media,Morogoro

JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Afisa Ardhi wa Mji mdogo wa Ifakara Wilayani Kilombero yaliyotokea Wilayani Kilombero, Mkoani Morogoro.

Hatua hiyo imechukuliwa na Jeshi hilo baada ya kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo, ambapo watuhumiwa hao wamekamatwa kwa ajili ya kuhojiwa na baada ya uchunguzi watafikishwa mahakamani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, mauaji hayo yametokea Julai 19 mwaka huu, majira ya saa 2 usiku katika Kitongoji cha Kapolo CCM, Kata ya Kibaoni, Tarafa ya Ifakara, Wilaya ya Kilombero, baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumba ya marehemu akiwa pamoja na familia yake.

Kamanda Kantimbo amesema watu hao walivunja mlango wa nyuma wa nyumba hiyo na kuingia ndani, kisha kumshambulia marehemu kwa kutumia silaha zenye ncha kali na kusababisha kifo chake papo hapo.

Amesema baada ya tukio hilo Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi na kufanikiwa kuwakamata watu hao saba wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo.

Kamanda Kantimbo amesema uchunguzi zaidi wa tukio hilo bado unaendelea na ukikamilika, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Mwisho

 MATUKIO DAIMA MEDIA IMETEULIWA KUWANIA TUZO ZA SKA2026 TUNAOMBA KURA YAKO WAWEZA KUPIGA KURA KIRAHISI KULIKO KUPITIA LINK HII

⬇️⬇️

BONYEZA HAPA KUINGIA KUPIGA KURA ZOTE NNE