Na Fadhili Abdallah,Kigoma
VIJANA nchini wametakiwa kuzingatia suala la Amani na usalama kwa nchi yao ili fedha zinazotolewa kwa ajili ya shughuli za uwezeshaji wa miradi ya kiuchumi kwa vijana ziweze kutekelezwa na kuleta tija kwa vijana hao.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Wazo Mwang’onda alisema hayo wakati wenge wa uhuru ulipotembelea kikundi cha umoja wa madereva wa bodaboda Makere halmashauri ya wilaya Kasulu mkoani Kigoma ambapo alisema kuwa Amani na usalama ukivurugika nchini hakuna kijana yeyote atafaidika na mabilioni ya shilingi ynayotolewa na serikali kwa vijana hao.
Alisema kuwa serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 200 kwa ajili ya kuinua shughuli za kiuchumi za vijana lakini pia msisitizo umetolewa kwa halmashauri kutumia mapato ya ndani kwa ajili ya uwezeshaji wa shughuli za kiuchumi za vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ambapo halmashauri ya wilaya Kasulu kwa mwaka uliopita imetoa kiasi cha Zaidi ya shilingi Bilioni moja kwa ajili ya mpango huo.
Awali mwenyekiti wa kikundi cha madereva bodaboda Makere, George Kagoma alisema kuwa tangu mwaka 2018 kikundi hicho kilipoanzishwa hadi sasa kimekopeshwa kiasi cha shilingi milioni 70.5 kutoka mapato ya ndani ya halmashauri ya wilaya Kasulu na tayari kiasi cha shilingi milioni 50.0 kimerejieshwa.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa baada ya kumaliza mkopo uliobaki wanatarajia kuomba mkopo mwingine kwa ajili ya kununua basi la abiria kwa ajili ya kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kwamba kwa maisha yao yamekuwa na mafanikio makubwa kwa kuweza kujenga nyumba, kusomesha watoto wao na kuhudumia vizuri familia zao.
Mwisho.



