Golugwa Kuendelea Kutoa Ushahidi wa Kumtetea Lissu leo – Video

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Amani Golugwa, leo Septemba 3, 2026, anaendelea kutoa ushahidi wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.

Golugwa alianza kutoa ushahidi wake jana, Septemba 2, 2026, akiwa shahidi wa tatu wa upande wa utetezi, baada ya shahidi wa pili, ambaye ni Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, kukamilisha ushahidi wake.

Katika ushahidi wake jana, Golugwa aliongozwa na Lissu na kueleza mambo mbalimbali, ikiwemo chimbuko la kampeni ya “No Reforms, No Election” ya CHADEMA, matukio yaliyohusiana na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 pamoja na ripoti mbalimbali za kimataifa zilizotoa madai kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025.

Aidha, Golugwa alieleza namna uongozi ndani ya CHADEMA unavyopatikana pamoja na majukumu yanayohusishwa na nafasi yake ya Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho.

Katika mwendelezo wa ushahidi wake leo, Golugwa ataendelea kuongozwa na Lissu katika kutoa utetezi wake.

Kesi hiyo yenye namba 19605/2025 inasikilizwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.

Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, kama ilivyorekebishwa mwaka 2023.

Lissu: Unasema kwamba mkutano uliandaliwa na Sekretariet, waeleze waheshimiwa majaji hii Sekretariet ni akina nani?

Golugwa: Hii Sekretariet ninayoizungumzia ni Katibu Mkuu wa Chama, Manaibu Katibu wawili kwa maana ya Bara na Zanzibar, Makatibu wa Mabaraza matatu ya chama, BAWACHA, BAVICHA na BAZECHA.Pia Wakurugenzi wa Chama pamoja na wataalam wawili ambao wameteuliwa na Mwenyekiti kuwa sehemu ya Sekretariet ya chama.

Lissu: Jumla watu wangapi hapo kwa hesbau yako

Golugwa:14 Lissu: Kwa muundo wa Chama Sekretariet ya Chadema ni chombo cha aina gani?

Golugwa: Sekretariet ya Chadema ndicho chombo cha kiutendaji kinachofanya kazi kila siku za kichama kwa niaba ya Kamati Kuu ya Chama

Lissu:Sasa Shahidi umesema Katibu Miuu alikuja na wazo kwamba muandae mkutano muwaandae watia nia hao watia nia ni akina nani?

Golugwa: Hao watia nia ni wanachama wa Chadema ambao aidha walipitishwa kuwa wagombea kwenye uchaguzi wa 2020 katika nafasi za udiwani, ubunge na Urais na kwamba bado nia yao ya kutaka kugombea nafasi hizo bado walikuwa nayo. Na wengine katika kundi hilo la watia nia ni wale ambao hawajawahi kugombea wala kupitishwa kwenye nafasi hizo nilizozitaja kwa maana mwaka 2025 na wao wakataka kutia nia wapitishwe kugombea nafasi hizo. Hao ndio watia nia.

Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji hao watia nia walikua wanatia nia ya kugombea nafasi gani

Golugwa:Waheshimiwa majaji hao watia nia walikuwa wanatia nia ya kugombea kwenye uchaguzi wa mwaka 2025.

Lissu:Waeleze waheshimiwa majaji lengo la kuwaita hao watia nia kwenye huo mkutano wa tarehe 3 Aprili lilikuwa lengo gani?

Golugwa: Lengo lilikuwa ni kuwaeleza na kuwafafanulia juu ya msimamo wa Chama uliopitishwa na mkutano kwa maana ya wazo la No Reforms No Elections, na msimamo huo ukawa umefafanuliwa na Kamati Kuu ya chama kwa kuazimiwa hilo ndilo lilikuwa lengo.

Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji unaposema No Reform No Elections, huu msimamo ulikuwa unahusu nini hasa?

Golugwa: Msimamo huu ulianza au ulizaliwa baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024.

Nikiwa Katibu wa Kanda ya Kaskazini, Katibu Mkuu alituambia Makatibu wa Kanda atuandikie ripoti ya uchaguzi wa Serikali za mitaa jinsi ulivyofanyika, na mimi kama mtendaji ambaye nilikuwa sehemu ya uchaguzi huo kwa kusimamia kanda ya Kaskazini nilitoa ripoti kwa kuonesha madudu mengi ya hivyo yaliyojitokeza.

Na Katibu Mkuu alitutaka tuandike maoni yetu ya kuhusiana na nini chama kifanye kutokana na hayo yaliyojitokeza, kwa hivyo mimi kwenye ripoti niliandika na waheshimiwa majaji naomba nitumie maneno exactly maneno niliyoandika yalikuwa maneno makali “Kwa ushenzi huu niliouona chama kisishiriki uchaguzi mwingine wowote mpaka kushinikiza mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi”.

Na Makatibu wenzangu kutoka katika kanda 9 kila mmoja kwa lugha yake wote tulitoa taarifa au ripoti yenye pendekezo zinazofanana na ndipo Kamati Kuu ikaketi ikayachakata mapendekezo ya Makatibu wa Kanda na wajumbe wenyewe wa Kamati Kuu ikatafakari kwa jinsi wanavyojua, basi nadhani tarehe 10 Desemba 2024, Mwenyekiti wa Chama wakati huo Mh. Freeman Mbowe akatoa tamko rasmi la chama, msimamo wa Kamati Kuu yaliyoazimiwa kwamba hatutakuwa tayari kwenda kwenye uchaguzi mwingine wowote bila mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi.

Lissu: Shahidi hebu waeleze waheshimiwa majaji kwa kifupi ni ushenzi gani uliouona.

Golugwa: Waheshimiwa majaji ushenzi ni mwingi.

Lissu: Waeleze majaji kwa ufahamu wako taarifa ya watazamaji wa uchaguzi wa SADC walisemaje juu ya huo uchaguzi.

Shahidi: Walisema uchaguzi wa Tanzania umeshindwa kukidhi Vigezo vya chaguzi kwa viwango vya chaguzi za kidemokrasia. Pia kulikuwa na Vitisho kwa viongpzi wa vyama vya upinzani na hivyo mazingira ya kiushindani hayakuwa sawa. Pia hakukuwa na uwazi katika mchakato mzima wa uchaguguzi. Kulikiwa na udanganyifu katika mchakato wa uchaguzi vurugu Siku ya uchaguzi hivyo uchaguzi wa Tanzania umekosa uhalali wa kuitwa uchaguzi.

Lissu: Waeleze Majaji watazamani wa Uchagauzi huo wa Jumuiya ya Ulaya EU walisemaje juu ya uchaguzi huo

Shahidi: Watazamaji wa Jumuiya ya Ulaya kwanza walisema wamesikitishwa na matukio ya vurugu yaliyotokea siku ya uchaguzi na kupelekea kuvuruga uchaguzi na wamesikitishwa na uharibifu wa mali na wamesikitishwa na mtandao kuzimwa mawasiliano na wamesikitishwa na taarifa za mauaji.