Matukio Daima Media, Morogoro
Katibu wa Jumuiya ya Wanawake, UWT, Morogoro Mjini, Judith Laizer, ameamua kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa namna tofauti, baada ya kutumia sehemu ya siku hiyo kwa yeye na familia yake kuwafikia watoto yatima na wenye mahitaji maalum wanaolelewa katika Kituo cha Agape, Kihonda, Manispaa ya Morogoro.
Katika maadhimisho hayo, Judith alishirikiana na watoto hao kukata keki na kula pamoja, huku akiwapatia baadhi ya mahitaji ya kibinadamu.
Hatua hiyo ilifanya siku yake ya kuzaliwa kuwa ya kipekee, huku watoto hao wakipata fursa ya kufurahia na kusherehekea pamoja naye.
Judith amesema kwake, kusherehekea siku ya kuzaliwa siyo tu kukusanyika na familia na marafiki, bali pia ni fursa ya kushirikiana furaha na watu wengine, hususan watoto wanaohitaji upendo, faraja na msaada kutoka kwa jamii.
Baada ya shughuli hizo katika kituo cha Agape,na kutoa wito kwa jamii kuwakumbuka watoto Wenye uhitaji kwa mahitaji mbalimbali ya kibinadamu.
Mlezi wa Kituo cha Agape aliyejitambulisha kwa jina la Mama Tina, Raia wa Kigeni aliyelowea nchini kwa miaka mingi, amesema kituo hicho kina watoto zaidi ya 40 ambapo wengine wako shule za bweni, na wamewalea watoto ambao wengine kwasasa wameshafikia hatua ya kujitegemea na wengine wanasoma elimu ya juu.
Akatoa wito kwa watu wenye mapenzi mema kuwatembelea watoto kituoni hapo na kuwapatia msaada wa mahitaji kikiwemo chakula, Vifaa vya shule, mavazi na mahitaji mengine muhimu ya kijamii.
Kwa upande wake Judith aliendelea na sherehe ndogo nyumbani kwake maeneo ya Kihonda akiwa ndugu, jamaa na Marafiki wachache, akihimiza Umoja na mshikamano katika kufikia mafanikio yeyote kwa kila mtanzania.
Mwisho



