.
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daniel Sillo, amesema Bunge lipo tayari kushirikiana na Serikali katika kufanikisha mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), akisisitiza umuhimu wa michezo katika kujenga afya, umoja, udugu na nidhamu.
Sillo ameyasema hayo wakati wa Bonanza la Bunge lililowakutanisha wabunge, wizara na taasisi mbalimbali jijini Dodoma, ambapo aliwataka washiriki kutumia michezo kama sehemu ya kujenga afya bora na kuimarisha mahusiano baina yao.
Amesema michezo ina nafasi kubwa katika kupunguza msongo wa mawazo, jambo alilolieleza kuwa ni muhimu kwa wabunge kutokana na majukumu yao ya kutunga sheria, kuisimamia Serikali na kufanya maamuzi yanayogusa maisha ya wananchi.
“Nimefurahishwa kuona idadi kubwa ya washiriki katika michezo ya leo. Michezo hupunguza msongo wa mawazo na mwili wenye afya ni suluhisho muhimu katika kufanya maamuzi mazuri,” amesema Sillo.
Sillo amewapongeza washindi pamoja na washiriki wote wa bonanza hilo, huku akiishukuru Benki ya NMB kwa kuwezesha kufanyika kwa shughuli hiyo na kuchangia katika kuimarisha afya na ustawi wa wabunge.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Wateja Binafsi wa NMB, Filbert Mponzi, amesema benki hiyo imeendelea kuboresha huduma zake za kifedha, ikiwemo kuwezesha wananchi kupata mikopo kwa njia ya kidijitali.
Mponzi pia ametajwa katika taarifa za hivi karibuni za NMB kuhusu huduma za kifedha kwa wafanyabiashara.
Amesema kupitia huduma ya NMB Mkononi, mteja anaweza kupata mkopo wa MshikoFasta kwa kutumia simu yake bila kulazimika kufika benki au kupitia taratibu ndefu za maombi, huku tathmini ya uwezo wa kukopa ikifanyika kwa kuzingatia historia ya miamala ya mteja.
Mponzi amesema mteja wa kawaida anaweza kukopa hadi Sh milioni mbili bila kujaza fomu wala kuweka dhamana, akieleza kuwa huduma hiyo inalenga kupunguza changamoto ya wananchi kukosa mikopo kutokana na masharti magumu ya dhamana.
“Mkopo huu ni suluhisho kwa wananchi wetu, wakiwemo wabunge, mamalishe, bodaboda na wafanyabiashara wengine. Hakuna dhamana inayohitajika, tunaangalia miamala yako,” amesema.
Aidha, Mponzi amesema NMB imeboresha huduma zake kwa wajasiriamali, ambao wanaweza kupata mikopo ya hadi Sh milioni tano bila dhamana, huku tathmini ikizingatia taarifa za miamala ya biashara zao.
Amesema NMB pia imehamia kwenye mfumo mpya wa kibenki baada ya kutumia mfumo wa awali kwa takribani miaka 15, hatua ambayo amesema itaiwezesha benki hiyo kutoa huduma za kisasa na zenye ufanisi zaidi, hususan katika eneo la huduma za kidijitali.
“NMB tumeingia kwenye mfumo mpya. Tunatarajia kuona mambo mazuri zaidi katika huduma zote kutokana na kuingia kwenye mfumo huu mkubwa,” amesema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Machano Ali Machano, aliipongeza NMB kwa mchango wake kwa Bunge, akisema wabunge wanatambua na kuthamini ushirikiano unaotolewa na benki hiyo katika shughuli mbalimbali, ikiwemo michezo.
Machano amesema mashindano ya Mabunge ya Afrika Mashariki yanatarajiwa kufanyika jijini Arusha mwezi Desemba mwaka huu, yakishirikisha wabunge kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema Tanzania, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo NMB, inapaswa kutumia mashindano hayo kama fursa ya kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku akisisitiza umuhimu wa maandalizi mazuri.









