Binti wa Ruto na Mtanzania Isaya Kufunga Ndoa Kesho, Wateka Insta!

Global Publishers
November 5, 2026
30 views
0 Comments

Mtoto wa Rais wa Kenya, William Ruto, Charlene Ruto, amezua gumzo mitandaoni baada ya kushiriki picha kadhaa akiwa katika vazi la harusi pamoja na mchumba wake, mfanyabiashara Mtanzania Isaya Yunge.

Charlene amechapisha picha hizo kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, akionyesha muonekano wake katika vazi jeupe la harusi huku Isaya akionekana akiwa amevalia suti nyeusi.

Picha hizo zimekuja wakati taarifa zikieleza kuwa wawili hao wanatarajiwa kufunga ndoa ya kanisani kesho, Novemba 6, 2026, jijini Mwanza, Tanzania.

Tukio hilo linatarajiwa kuwakutanisha ndugu, jamaa na wageni mbalimbali kutoka Tanzania na Kenya, kutokana na nafasi ya familia ya Charlene katika uongozi wa Kenya.

Harusi hiyo inafuatia sherehe ya jadi ya Kalenjin inayojulikana kama Koito iliyofanyika Agosti 8, 2026, katika eneo la Kilgoris, Kaunti ya Narok nchini Kenya, ambapo familia za wawili hao zilikutana kurasimisha hatua ya ndoa yao.

Isaya Yunge ni mfanyabiashara wa teknolojia kutoka Tanzania na mwanzilishi mwenza wa SomaApp, jukwaa linalowaunganisha wanafunzi wa Afrika na fursa za masomo na ufadhili.

Uhusiano wa wawili hao umeendelea kuvutia hisia za watu nchini Kenya na Tanzania, huku maandalizi ya harusi yao yakizua gumzo katika mitandao ya kijamii.