WANACHAMA WA CHAMA CHA WAKALA WA FORODHA TANZANIA (TAFFA), WAUGOMEA MKUTANO WA OKTOBA 28

NA.MATUKIO DAIMA MEDIA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya usafirishaji mizigo ya Beam Tanzania Limited, Julius Ng’anga, ametoa angalizo kwa uongozi wa TAFFA pamoja na wanachama wake kuhusu utaratibu uliotumika katika kupitisha na kusaini mkataba unaolalamikiwa, akieleza kuwa kuna maswali mengi ambayo bado hayajapatiwa majibu ya kuridhisha kwa wanachama.

Julius amesema moja ya mambo yanayotia mashaka ni uhalali wa mkutano uliofanyika Oktoba 28, wakati suala la mkataba huo tayari lilikuwa mahakamani.

Amesema wanachama walitarajia kupewa nakala za mkataba ili waupitie, kuusoma na kutoa maoni yao kabla ya kusainiwa, badala yake mkataba huo ulisomwa kama taarifa bila kuwapa nafasi ya kuuchambua kwa kina.

Amehoji pia kama mkataba uliosomwa katika mkutano huo ndio uliosainiwa, akisema wanachama walipaswa kushirikishwa katika mchakato mzima wa majadiliano na kupata nafasi ya kuelewa vipengele vyake kabla ya uamuzi wa mwisho kufanyika.

“Kulikuwa na maswali kuhusu uwepo wa wageni walioalikwa kwenye mkutano huo, ambao waliondoka kabla ya mkutano kuanza kujadili hoja za msingi,wanachama walihitaji kupata ufafanuzi kuhusu mamlaka iliyowatuma wageni hao na sababu za kuondoka kwao kabla ya mkutano kukamilika”alisema

Katika hoja nyingine, Julius amesema kuna mashaka kuhusu kuanza kwa matumizi ya mfumo unaohusishwa na mkataba unaolalamikiwa, wakati suala la uhalali wa mkataba huo bado linajadiliwa mahakamani. 

Ameongeza kuwa hata utaratibu wa upigaji kura haukuwa wazi kwa kuwa hakukuwa na uhakika wa namna wakurugenzi wa kampuni mbalimbali walivyotambuliwa na kura zao kuhesabiwa.

Ameitaka pia TAFFA kutoa maelezo kuhusu madai ya kuwepo kwa watu waliotajwa kuwa mamluki wakati wa mkutano, akisisitiza kuwa wanachama wanahitaji kujua utaratibu uliotumika kuwatambua na kuhakikisha maamuzi yaliyofanyika yanaakisi maoni halisi ya wanachama.

Julius ameendelea kuhoji sababu za mkataba huo kuhusisha kampuni au watu kutoka nje ya nchi katika shughuli ambazo, kwa mtazamo wake, zinaweza kusimamiwa na taasisi za ndani.

 Amesema Tanzania tayari ina taasisi zenye mamlaka ya kutoa leseni na kusimamia shughuli husika, hivyo ni muhimu kueleza sababu za kutafuta huduma hizo kutoka nje badala ya kuimarisha mifumo ya ndani.

Amesema pia muda wa miaka 15 uliotajwa katika mkataba huo unahitaji ufafanuzi, hasa iwapo kutakuwa na mabadiliko au kusitishwa kwa mkataba kabla ya muda wake kuisha, kutokana na gharama zinazoweza kuwa tayari zimetumika katika utekelezaji wake.

Aidha ameitaka TAFFA kuweka wazi mkataba huo, kutoa majibu kwa maswali ya wanachama na kuhakikisha maamuzi yote yanayohusu maslahi ya wanachama yanafanyika kwa uwazi, uwajibikaji na kwa kuzingatia ridhaa ya wanachama.

MWISHO.