
Aliyekuwa mke wa mfanyabiashara maarufu wa Zimbabwe, marehemu Wicknell Chivayo, Sonja Louise Madzikanda, amekubaliana na familia ya marehemu kuwa msimamizi mwenza wa mali alizoacha, hatua inayosubiri kuidhinishwa na Msajili Mkuu wa Mahakama Kuu.
Madzikanda atashirikiana na dada wa marehemu, Esther Chivayo, katika kusimamia mirathi hiyo yenye thamani ya mamilioni ya dola.
Kwa mujibu wa barua ya Novemba 3, 2026, iliyowasilishwa na mawakili wa Madzikanda, Mahuni Gidiri Law Chambers, makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mashauriano kati ya wahusika wote wenye maslahi katika mirathi hiyo.
Mawakili hao waliiomba ofisi ya Msajili Mkuu wa Mahakama Kuu kuweka makubaliano hayo katika jalada la mirathi ili yaweze kuzingatiwa na kuidhinishwa.

Madzikanda ana watoto wawili na marehemu Chivayo, jambo linalomweka katika nafasi muhimu katika usimamizi wa masuala yanayohusu urithi wa watoto hao.
Hatua hiyo inakuja wakati kukiwa na maswali kuhusu namna utajiri wa marehemu utakavyosimamiwa na kuhakikisha kuwa matakwa yake kuhusu mustakabali wa watoto wake yanatekelezwa.
Msemaji wa familia, Herbert Chivayo, aliwahi kuwaambia waombolezaji kuwa familia haikuwa na nia ya kutapanya mali alizozitafuta marehemu wakati wa uhai wake. Alisisitiza kuwa matakwa ya Chivayo yalikuwa kuhakikisha watoto wake wanarithi utajiri wake.

Wicknell Chivayo alifahamika nchini Zimbabwe na nje ya nchi kutokana na maisha yake ya kifahari yaliyohusisha magari ya gharama kubwa, matumizi makubwa ya fedha, zawadi za thamani na uhusiano wake na watu mashuhuri wa kisiasa.
Mfanyabiashara huyo alifariki katika ajali ya helikopta akiwa pamoja na mke wake Lucy Muteke na watu wengine watatu.
Endapo uteuzi huo utaidhinishwa, Madzikanda na Esther Chivayo watakuwa na jukumu la pamoja katika kusimamia masuala ya mirathi ya marehemu.
Hata hivyo, uamuzi wa mwisho kuhusu uteuzi wao bado unasubiriwa kutoka kwa Msajili Mkuu wa Mahakama Kuu.
