CRDB yazindua kampeni kidijitali zaidi – HabariLeo

DAR ES SALAAM: Benki ya CRDB imeboresha huduma zake za Internet Banking kwa kuweka mifumo inayowawezesha wateja kufanya miamala kwa haraka, urahisi na usalama zaidi, huku ikitoa fursa ya kujisajili wenyewe na kuanza kutumia huduma hiyo bila kulazimika kufika katika matawi ya benki hiyo.

Maboresho hayo ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kuendelea kuboresha huduma za kidijitali na kuwapa wateja urahisi wa kufanya miamala yao wakati wowote na mahali popote.

Akizungumza kuhusu maboresho hayo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Bonaventure Paul, amesema hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza kwa watumiaji wa Internet Banking na kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa huduma za kibenki.

Amesema huduma hiyo sasa inawawezesha wateja kufanya miamala saa 24 kwa siku na siku saba za wiki, hali inayowapa uhuru wa kupata huduma za kibenki muda wowote bila kutegemea saa za kazi za matawi au mawakala.

Paul amesema moja ya maboresho muhimu ni kuanzishwa kwa mfumo wa kujisajili mwenyewe (Self-registration), unaomwezesha mteja mwenye akaunti ya CRDB iliyounganishwa na kadi ya ATM kujisajili na kuanza kutumia Internet Banking bila kufika katika tawi la benki.

Amesema hatua hiyo itapunguza muda na gharama ambazo wateja wamekuwa wakitumia kufuata huduma hiyo kwenye matawi, huku ikiongeza urahisi wa kupata huduma za kidijitali.

Aidha, amesema maboresho mengine ni kuwepo kwa uwezo wa mteja kurejesha huduma yake (Unlock) pale akaunti ya Internet Banking inapozuiwa kutokana na kuingiza nywila isiyo sahihi mara kadhaa.

Amesema kupitia mfumo huo, mteja anaweza kurejesha huduma yake bila kulazimika kufika katika tawi la benki kwa ajili ya kuhakikiwa upya.

Maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza matumizi ya huduma za kibenki kupitia njia za kidijitali, kupunguza utegemezi wa huduma za ana kwa ana na kuwezesha wateja wa CRDB kupata huduma kwa urahisi zaidi.