ARUSHA; Wataalamu wa kada mbalimbali wametakiwa kujifunza na kutumia teknolojia ya akili unde (AI) katika kuboresha utendaji wa majukumu yao.
Aidha walimu na wahadhiri wamehimizwa kuiboresha mifumo ya ufundishaji na tathmini ili kuhakikisha wanafunzi wanaitumia teknolojia hiyo kama nyenzo ya kujifunzia, badala ya kutegemea kufanya kazi zinazopaswa kutekelezwa na wao wenyewe.
Mwito huo umetolewa na Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Eliamani Sedoyeka katika kongamano la kitaaluma lililoandaliwa na chuo hicho na kuwakutanisha wanafunzi wa shahada ya uzamili, wanataaluma na wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili changamoto zinazoikabili jamii na kuangalia namna ya kuzitatua kupitia tafiti na maarifa yao jijini Dar es Salaam leo.
“Mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani hayawezi kuzuiliwa, hivyo ni muhimu kwa walimu, wahadhiri na wataalamu wa kada mbalimbali kujifunza namna ya kuitumia AI katika kuboresha utendaji wao wa kitaaluma,” alisema.

Alisema wataalamu wanapaswa kuhakikisha wanapata mafunzo ya teknolojia hiyo ili kuelewa namna inavyoweza kutumika katika fani zao na kuongeza ufanisi katika majukumu wanayotekeleza.
Akizungumzia matumizi ya AI katika elimu, Profesa Sedoyeka alisema teknolojia hiyo inaweza kusaidia katika tafiti kwa kubaini maeneo ambayo tayari yamefanyiwa utafiti na yale ambayo bado yana mapengo ya maarifa yanayohitaji kuchunguzwa huku akisisitiza kuwa matumizi hayo yanaweza kuwawezesha wanafunzi na watafiti kutambua maeneo mapya ya kufanyia tafiti na kurahisisha mchakato wa kupata taarifa za kitaaluma.
Alisisitiza kuwa changamoto kubwa ni baadhi ya wanafunzi kutumia AI kufanya kazi zao na kuwasilisha matokeo kana kwamba wamezifanyia wao wenyewe, jambo linaloweza kudhoofisha malengo ya elimu ya kuwajengea maarifa, ujuzi, weledi na kubadili tabia.
Alisema walimu wanapaswa kubuni namna mpya za kutoa kazi na mitihani zitakazohakikisha wanafunzi wanapata ujuzi unaokusudiwa hata wanapotumia teknolojia hiyo.
Kwa upande wake Mhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Uongozi na Utawala Bora kutoka IAA, Sharfani Zuberi amewataka wanafunzi hasa wa vyuo vikuu kuepuka matumizi mabaya ya AI katika kufanya tafiti na kuandika kazi za kitaaluma, bali watumie maarifa na uwezo wao binafsi ili kulinda ubora na uadilifu wa taaluma.
“Naomba wanafunzi waache kutumia AI kwa namna hasi, kwa sababu taaluma haina udanganyifu. Tujaribu kutumia akili zetu darasani, tunapoandika makala na tunapochapisha tafiti zetu,” alisema.
Katika utafiti aliouwasilisha, Zuberi alisema alijikita kuchunguza nafasi ya mawasiliano kati ya menejimenti na wafanyakazi, akieleza kuwa mawasiliano ni nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo ya taasisi.
