Na Hamida Ramadhan, Dodoma Matukio Daima Media Dodoma
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Judith Suminwa Tuluka, ameishukuru Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushirikiana na nchi hiyo katika masuala ya usalama na maendeleo ya kiuchumi, akisema ushirikiano huo ni muhimu katika kulinda maslahi ya mataifa hayo mawili.
Akiongea leo Novemba 4 Mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea mji wa Serikali Mtumba Dodoma, Waziri Mkuu huyo, amesema Tanzania na DRC zina uhusiano wa muda mrefu uliojengwa katika misingi ya undugu na ujirani mwema, hivyo ni muhimu kuendelea kuimarisha ushirikiano huo ili kulinda usalama na kukuza uchumi wa nchi hizo.
Ameeleza kuwa ushirikiano huo utaendelea kuimarishwa kupitia maeneo mbalimbali yenye maslahi ya pamoja, ikiwamo juhudi za kuendeleza miji na kuboresha mazingira ya maendeleo kwa wananchi wa nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi wa DRC, John Banza Lunda, amesema amevutiwa na hatua za maendeleo ya miundombinu zilizofikiwa na Tanzania, akieleza kuwa ziara yake nchini imempa fursa ya kujionea uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta hiyo.
Banza Lunda amesema safari yake kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma imemwezesha kushuhudia maendeleo ya miundombinu ya usafiri, pamoja na uwekezaji katika majengo ya umma, ikiwamo Bunge na Mji wa Serikali wa Mtumba.
Amesema Tanzania imepiga hatua katika kuimarisha miundombinu, jambo ambalo ni muhimu katika kurahisisha usafiri, kuboresha utoaji wa huduma na kukuza uchumi wa taifa.
Ameeleza kuwa serikali ya nchi yake pia inaendelea kuweka juhudi katika kujenga na kuimarisha miundombinu ndani ya DRC ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, amesema anatarajia kutumia Treni ya Reli ya Kisasa (SGR) kusafiri kurejea Dar es Salaam ili kujionea zaidi uwekezaji uliofanywa na Tanzania katika sekta ya usafiri wa reli.
Waziri huyo ameishukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ukarimu na mapokezi mazuri aliyoyatoa kwa ujumbe wa DRC wakati wa ziara yao nchini.
“Katika kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, Banza Lunda amesema DRC inaendelea na juhudi za kuendeleza bandari katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, ambayo inatarajiwa kuanza kufanya kazi Machi 2027,” Amesema.
Na Kuongea “mesema bandari hiyo itakuwa muhimu katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kukuza biashara katika maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika, hususan katika kuimarisha shughuli za kiuchumi za wananchi wa maeneo hayo, ” Amesema waziri Lunda
Naye Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amesema Tanzania imefurahi kupokea ujumbe kutoka DRC kwa ziara ya kindugu na kirafiki inayolenga kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo.
Kairuki amesema mahusiano ya Tanzania na DRC hayajaanza leo, bali yamejengwa kwa muda mrefu kutokana na historia ya undugu, ujirani na ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Amesema ziara hiyo ni fursa muhimu ya kuendeleza urafiki na kuimarisha mahusiano yaliyopo, huku akieleza kuwa Tanzania inathamini uhusiano huo na itaendelea kujenga mazingira mazuri ya ushirikiano na taifa hilo.
Ameongeza kuwa ziara za aina hiyo zina nafasi kubwa katika kuimarisha mshikamano wa mataifa hayo na kufungua fursa zaidi za kushirikiana katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na DRC.

