SHALOM ROBERT:SERIKALI YAWEKA USAWA KATIKA ELIMU MAFINGA IRINGA

MATUKIO DAIMA MEDIA

MAFINGA.Wananchi wa Mji wa Mafinga Wilayani Mufindi Mkoani Iringa wameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kujenga shule ya Serikali ya mchepuo wa kiingereza hali inayoweka usawa kwa watoto wote kupata elimu bora.

Mdau wa maendeleo ambaye pia ni Mwanahabari Ndg.Shalom Robert akiwa mgeni wa heshima katika Mahafali ya Tatu ya Shule ya Chief Mkwawa English Medium amesema  jitihada za Serikali kuweka usawa kwa watoto kwa kujenga shule hiyo kunawafanya hadi wananchi wenye uchumi wa chini kuwapeleka watoto wao kupata elimu bora.

Aidha Robert Amesema shule hiyo imefanikiwa kupokea watoto wa Mama Lishe,Machinga,Wakulima na hata Wafugaji ambao wasingeweza kuwasomesha watoto wao kwenye shule ya mchepuo wa Kiingereza.

Ofisa Elimu Msingi Halmashauri ya Mji wa Mafinga Doroth Kobelo amesema ujenzi wa shule hiyo umepunguza mzigo kwa wazazi waliotamani kuwapeleka watoto wao English medium kwani ada yake ni nafuu na kila mzazi anaweza kumudu.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Chief Mkwawa English Medium Mwalimu James Kelela amesema shule hiyo imekuwa kimbilio la wazazi wengi kwani serikali imewekeza  miundombinu bora ya kujifunzia hali inayopelekea wazazi wengi kupeleka watoto wao hapo.

Katika mahalafi hayo shalom amechangia vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni mbili ili kuwafanya watoto wapate elimu bora pamoja na Michezo.