MBEYA; Kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa takribani dakika 30 na kusababisha nyumba 21 kusombwa na maji huku kaya 43 zikikosa makazi katika Kata ya Nzovwe, jijini Mbeya, Mkuu wa Mkoa huo, Jumanne Sagini, amewaagiza wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi kuhama mara moja kwa muda ili kunusuru maisha yao.
Akizungumza baada ya kuwatembelea waathirika wa mafuriko hayo, Sagini ameonya kuwa madhara yaliyotokea ni ishara ya hatari inayoweza kujitokeza zaidi endapo mvua kubwa zinazotabiriwa zitaendelea kunyesha huku wananchi wakiendelea kukaa katika maeneo hatarishi.
“Serikali imekuwa ikizungumzia uwepo wa mvua za El Niño, lakini baadhi ya watu wamekuwa wakifanya mizaha badala ya kuchukua tahadhari na kumuomba Mungu,sasa tumeona mvua ya nusu saa tu imesababisha madhara haya,Je, kama ingenyesha kwa saa saba hali ingekuwaje?” Amehoji Sagini.

Kutokana na hali hiyo, mkuu huyo wa mkoa ameagiza kamati ya maafa kuhakikisha kaya zilizoathirika zinapata msaada wa haraka wa chakula na magodoro, akieleza kuwa baadhi ya waathirika wamelazimika kuhifadhiwa na ndugu pamoja na majirani.
Aidha amethibitisha kuwa hakuna mtu aliyepoteza maisha katika tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuchukua tahadhari dhidi ya mvua zinazoendelea kunyesha ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Amesema tayari Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)imeanza kuchukua hatua za kuboresha maeneo hatarishi, ikiwemo kushughulikia mtaro unaotajwa kuchangia mafuriko hayo baada ya maji kujaa na kufurika.
Kwa upande wake, mmoja kati ya waathirika wa tukio hilo, Innocent Mwongole, ameiomba Serikali kuhakikisha mtaro huo unafanyiwa marekebisho na vifusi vinavyotokana na shughuli za ujenzi wa barabara vinaondolewa ili kuzuia mafuriko mengine yasitokee.
