Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro amekabidhi misaada kwa waathirika wa mvua za El Nino zinazoendelea kunyesha mkoani Kigomana kuleta madhara kwa watu mbalimbali huku akionya wale wote wanaokaidi kuhama kwenye maeneo hatarishi ambayo yameainishwa na serikali.
Mkuu huyo wa mkoa Kigoma amesema hayo akikabidhi misaada kwa wananchi wa kata ya Gungu manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo alisema tahadhari imetolewa wananchi kuhama kwenye maeneo hatarishi ambayo yameainishwa lakini wananchi badala ya kufuata maelekezo hayo wengine wanabeza na kusema kuwa ni propaganda kwa ajili ya matumizi ya fedha kwa watendaji kujiilipa posho jambo ambalo serikali imesema haikubaliani nalo na hatua za kisheria kwa watu hao zitachukuliwa.
Pamoja na hilo Balozi Sirro alisema kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua na kuwasaidia wananchi watakaoathirika na mvua hiyo kwa sababu mkoa Kigoma umeelezwa kuwa moja ya mikoa ambayo itapata mvua nyingi na kuanzia mwezi Oktoba wilaya za Kigoma, Buhigwem Kakonko, kasulu na Kibondo zimekumbwa na mvua kubwa za upepo ambazo tayari zimeleta madhara kwa wananchi.
Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa mkoa kuhusu athari zilizojitokeza Kaimu Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Hashim Mvogogo alisema kuwa tangu mwezi Oktoba mwaka huu Mvua za El Nino zilipoanza mkoani Kigoma kaya Zaidi ya 100 zimeathirika ambapo nyumba 121 na makanisa manne zimeezuliwa paa na nyingine kuanguka.
Mvogogo alisema kuwa kata zilizoathirika na mvua hiyo ni pamoja na Gungu ambapo nyumba 70 zimeathirika, Kibirizi nyumba 47, Mwanga Kusini Nyumba mbili na kata ya Katubuka nyumba mbili.
Akieleza msaada uliotolewa kwa wahanga wa mvua hiyo alisema kuwa wamewasilisha tani 2.6 za Mchele, unga wa mahindi tani 1.9, maharage tani moja, sukari, mafuta ya kupikia na sabuni za kufulia huku wakiendelea kushughulikia mahitaji ya magodoro, shuka, Blanketi na maturubaki huku waathirika wahifadhiwa katika maeneo mbalimbali.
Baadhi ya waathirika wa mvua hizo Akiwemo Kobwa Kamana wameishukuru serikali kwa misaada hiyo ya vyakula ingawa alisema kuwa wanaomba serikali ifikirie Zaidi mahitaji ya namna ya kurudi kwenye makazi yao kwa kuwapatia misaada ya bati za kuezekea nyumba zao.
Mwisho.




