WAFANYABIASHARA wa mazao katika eneo la Tunduma mkoani Songwe wameiomba Serikali kupitia upya gharama za vibali, vyeti vya afya ya mimea (Phytosanitary) na tozo mbalimbali zinazotozwa katika biashara ya mazao, wakieleza kuwa gharama hizo zinaongeza mzigo wa uendeshaji na kuathiri mnyororo wa thamani wa mazao.
Akizungumzia changamoto hizo, mfanyabiashara wa mazao, Lusekelo Mwansasu, amesema gharama za kupata nyaraka zinazohitajika katika usafirishaji wa mazao zimekuwa mzigo kwa wafanyabiashara, ambao hulazimika kutumia fedha nyingi kabla hata ya kuuza bidhaa zao.
Mwansasu amesema moja ya changamoto hizo ni gharama ya cheti cha afya ya mimea (Phytosanitary), ambayo kwa mujibu wa maelezo yake imeongezeka kutoka Sh 400,000 hadi Sh 800,000, hali inayoongeza gharama za kusafirisha mazao.
Kutokana na hali hiyo, ameiomba Wizara ya Kilimo na taasisi zinazohusika na usimamizi wa mazao kuangalia uwezekano wa kurejesha ada hiyo katika kiwango cha awali cha Sh 400,000 ili kupunguza mzigo wa gharama kwa wafanyabiashara.
Aidha, amesema kuna tozo ya Sh 165,000 inayohusishwa na biashara ya kopra ambayo ameiomba Serikali kuiondoa ili kurahisisha shughuli za biashara na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao.
Amesema gharama hizo haziishii kwenye vyeti na tozo pekee, bali pia kuna malipo mengine yanayohusiana na kodi, vibali na taratibu za usafirishaji kutoka katika taasisi mbalimbali, hali inayofanya gharama za kupeleka mazao sokoni kuwa kubwa.
Mwansasu amesema changamoto nyingine inayowakabili wafanyabiashara wa mazao ni kupata wanunuzi, huku wakilazimika pia kugharamia wafanyakazi wanaoshiriki katika shughuli za ununuzi na usafirishaji wa mazao.
Ameeleza kuwa hali hiyo inaathiri uendeshaji wa biashara na uwezo wa wafanyabiashara kuendelea kutoa ajira kwa watu wanaotegemea shughuli hizo.
“Tayari wamewasilisha maoni na malalamiko yao katika vikao mbalimbali, ikiwemo mabaraza ya biashara ya wilaya na mkoa, wakitarajia kuwa changamoto hizo zitafanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi, ” Amesema.
Mwansasu amesisitiza umuhimu wa Serikali kushirikiana na wadau wa biashara ya mazao kupitia upya tozo na gharama zinazotozwa ili kuweka mazingira rafiki ya biashara, kuongeza thamani ya mazao na kuchochea maendeleo ya uchumi.
