Muuza magari ageuka mwana wa mfalme

Dar es Salaam. “Unaweza ukalala maskini na kuamka tajiri,” Kauli hiyo inaweza kuelezea kwa ufupi mabadiliko ya maisha ya Clément Vandenkerckhove, raia wa Ubelgiji aliyewahi kufanya kazi kitengo cha mauzo katika kampuni ya magari, kabla ya kutambuliwa rasmi kuwa mtoto wa Prince Laurent wa Ubelgiji.

Vandenkerckhove, mwenye umri wa miaka 26, sasa ametambuliwa kisheria kama mwanamfalme wa Ubelgiji baada ya Prince Laurent, mdogo wake na Mfalme Philippe, kukiri na kuthibitisha  kuwa ndiye baba yake mzazi.

Hatua hiyo imehitimisha miaka kadhaa ya sintofahamu kuhusu uhusiano wa Vandenkerckhove na familia ya kifalme ya Ubelgiji.

Kwa mujibu wa jarida la Soir Mag, Prince Laurent alikamilisha mchakato wa kisheria wa kumtambua Vandenkerckhove mbele ya msajili wa kiraia Februari mwaka huu. Vandenkerckhove pia alihudhuria na kusaini nyaraka hizo.

Ikulu ya Ubelgiji imethibitisha kuwa Prince Laurent amemtambua kisheria Vandenkerckhove kuwa mwanawe, lakini imeeleza kuwa suala hilo ni la kifamilia na haikutaka kutoa maelezo zaidi.

Kutokana na kutambuliwa huko, Vandenkerckhove amepewa hadhi ya mwanamfalme, ingawa hatarajiwi kuwa na majukumu rasmi ya kifalme.

Vandenkerckhove ni mtoto wa Prince Laurent na Iris Vandenkerckhove, anayefahamika zaidi kwa jina la Wendy Van Wanten, mwanamitindo, mwimbaji na mwigizaji maarufu nchini Ubelgiji.

Prince Laurent ni mdogo wa Mfalme Philippe na ana watoto wengine watatu aliowapata na mkewe, Princess Claire wa Ubelgiji, ambaye alimuoa mwaka 2003.

Licha ya kupata hadhi ya mwanamfalme, Vandenkerckhove hataingia kwenye mstari wa kurithi kiti cha ufalme wala kuwa na majukumu rasmi ya kifalme.

Kwa mujibu wa New York Times, Profesa Christian Behrendt, mtaalamu wa sheria za katiba kutoka Chuo Kikuu cha Liège nchini Ubelgiji, amesema hadhi hiyo imetokana na amri ya kifalme ya mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Profesa Behrendt, mtu anaweza kuingia kwenye mstari wa urithi wa kiti cha ufalme endapo amezaliwa katika ndoa iliyopitishwa na serikali kupitia amri maalumu.

Hivyo, ingawa Vandenkerckhove sasa anatambuliwa kama mwanamfalme, hana nafasi ya kumrithi Mfalme Philippe, ambaye ni baba yake mkubwa.

Prince Laurent alitangaza Septemba mwaka jana kwamba Vandenkerckhove ni mwanawe wa damu, akisema uamuzi huo ulifanyika kwa kuzingatia uelewano na heshima kwa wote waliohusika.

Uhusiano wao umeendelea kuonekana hadharani. Juni mwaka huu, Vandenkerckhove alichapisha picha akiwa na Prince Laurent pamoja na picha nyingine akiwa na Frans Vancoppenolle, ambaye amekuwa mwenza wa muda mrefu wa mama yake, katika ujumbe wa kuadhimisha Siku ya Baba.

Vandenkerckhove alizaliwa Agosti 2000 kutokana na uhusiano wa zamani kati ya Prince Laurent na Iris Vandenkerckhove.

Wawili hao walikuwa na uhusiano katika miaka ya 1990, kabla ya Prince Laurent kumuoa Princess Claire mwaka 2003.

Kwa muda mrefu, utambulisho wa baba wa Vandenkerckhove ulizungumziwa katika vyombo vya habari nchini Ubelgiji, lakini familia hiyo haikuthibitisha rasmi madai hayo hadi Prince Laurent alipotoa tamko mwaka jana.

Kabla ya kutambuliwa rasmi, Vandenkerckhove aliishi maisha ya kawaida na hata kufanya kazi hiyo.

“Nataka uhusiano na baba yangu.”

Kwa Vandenkerckhove, kupata cheo cha kifalme si jambo pekee lenye umuhimu. Zaidi ya hadhi hiyo, ameeleza umuhimu wa kujenga uhusiano wa karibu na baba yake baada ya miaka mingi ya kutokuwa na uhakika kuhusu nafasi yake katika familia ya kifalme.

Taarifa zinaeleza kuwa Prince Laurent amekuwa akitenga muda kwa ajili ya mwanawe huyo na wawili hao wameendelea kujenga uhusiano wao kupitia mazungumzo na muda wanaotumia pamoja.

Vandenkerckhove pia hajaonyesha haraka ya kubadili jina lake la ukoo kuwa la kifalme, huku akiendelea kujitambulisha kwa jina la familia ya mama yake.

Imeandikwa na Anitha Bosco kwa msaada wa mtandao.