IRINGA: WAKULIMA wa miti nchini wanahimizwa kuachana na dhana ya kupanda miti na kusubiri kuvuna pekee, badala yake kuwekeza katika mbegu bora, utunzaji wa kitaalamu na uvunaji unaozingatia viwango ili kupata magogo yanayokidhi mahitaji ya viwanda na soko.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa muhimu katika kuongeza thamani ya mazao ya misitu, kuimarisha ushindani wa wakulima katika soko na kuongeza tija ya uwekezaji katika mashamba ya miti.
Wito huo umetolewa katika majadiliano ya wadau wa sekta ya misitu yaliyoandaliwa na Shirika la FORLAND katika Hoteli ya Sunset mjini Iringa, yakilenga kujadili ubora wa magogo ya miti ya mashamba pamoja na changamoto zinazokwamisha uzalishaji wa mazao yanayokidhi viwango vinavyohitajika.
Akichangia mada hiyo, mkufunzi kutoka Chuo cha Mafunzo ya Misitu na Viwanda vya Misitu Mafinga, Walter Mushi, amesema ubora wa gogo huanza kujengwa tangu hatua ya uzalishaji wa mche hadi uvunaji, hivyo wakulima wanapaswa kuzingatia utaalamu katika kila hatua.

Amesema gogo bora linapaswa kuwa na umbo zuri, kutopinda na kuwa na sifa zinazokidhi mahitaji ya soko, akibainisha kuwa elimu ya upandaji na utunzaji wa miti ni muhimu katika kuwasaidia wakulima kuzalisha mazao yenye thamani kubwa.
Kwa upande wake, Meneja wa Misitu kutoka Kampuni ya TANWAT, John Mabula, amesema wakulima wanapaswa kuzingatia vigezo vya kitaalamu kuanzia maandalizi ya shamba, uchaguzi wa mbegu, upandaji na utunzaji hadi uvunaji ili kupata magogo yenye ubora.
Amesema baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakiingia katika shughuli za upandaji miti bila kuzingatia kikamilifu vigezo muhimu vya uzalishaji, hali inayoweza kusababisha kupata mazao yasiyokidhi mahitaji ya soko.
Naye mchambuzi wa sera kutoka Shirikisho la Sekta Binafsi, Michael Kijavara, amesema upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu matumizi ya ardhi na uzalishaji wa mazao ya misitu ni muhimu katika kuwawezesha wakulima kufanya maamuzi yenye tija.
Amesema kanuni na miongozo inayotumika katika sekta ya misitu inapaswa kuzingatia mazingira ya sasa ya kilimo na mahitaji ya wadau, huku akiwataka wakulima kuwa makini na mikataba ya mauzo ya mazao yao wakiwa bado shambani.

Akizungumzia umuhimu wa ushirikiano katika kuboresha sekta hiyo, Afisa Maliasili wa Mkoa wa Iringa, Dk Bahati Golyama, amesema majadiliano hayo yameunganisha wadau katika kutafuta njia za kuboresha uzalishaji wa miti, matumizi ya teknolojia na ushiriki wa wataalamu.
Amesema Mwongozo wa Kiufundi wa mwaka 2021 unaelekeza utekelezaji wa shughuli mbalimbali za misitu, lakini bado kuna haja ya kuufikisha kwa wadau wengi zaidi ili waweze kuuelewa na kuutumia ipasavyo.
Akijibu hoja kuhusu sababu zinazowafanya baadhi ya wakulima wadogo kushindwa kuzalisha magogo bora, Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Wakulima wa Miti Tanzania (TTGAU), Castory Timbula, amesema historia ya shughuli za uvunaji wa miti imechangia changamoto zinazowakabili wadau hao.
Amesema awali wavunaji wengi walijikita katika uvunaji wa misitu ya Serikali na walipoanza kuendesha shughuli zao binafsi, hakukuwa na kanuni na taratibu zilizowalenga moja kwa moja, huku zilizokuwepo zikihusishwa zaidi na usimamizi wa misitu ya Serikali.
Timbula ameshauri wadau wote, hususan wakulima wadogo, washirikishwe katika mchakato wa kupitia na kuboresha Mwongozo wa Kiufundi wa mwaka 2021 ili uweze kuzingatia hali halisi ya uzalishaji na changamoto wanazokabiliana nazo.
Akieleza sababu za kuandaliwa kwa majadiliano hayo, Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa FORLAND kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Emma Nzunda, amesema hatua hiyo imetokana na changamoto ya upatikanaji wa magogo yenye ubora unaokidhi viwango vinavyohitajika.
Nzunda amesema Serikali imeweka viwango vya ubora wa mazao ya misitu, hivyo ni muhimu wadau kuelewa sifa zinazotakiwa ili kuboresha uzalishaji na kuhakikisha mazao yanayopatikana yanaendana na mahitaji ya soko.
Amesema maoni yaliyotolewa yataisaidia FORLAND na wadau wengine kutathmini namna ya kuboresha uelewa wa viwango vya uzalishaji na mapitio ya Mwongozo wa Kiufundi wa mwaka 2021, ili uweze kuwafikia na kueleweka na wadau wengi zaidi.
