Ali Kamwe Atoa Kauli Nzito Baada ya Yanga Kufumwa na Simba

Afisa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ali Kamwe

Afisa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ali Kamwe, amezungumzia kipigo cha mabao 2-1 walichopata dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC, katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Jumamosi, Oktoba 10, 2026, kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kamwe amekiri kuwa Simba imevunja mwiko wa miaka mitatu bila kuifunga Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, akiwapongeza wapinzani wao kwa ushindi huo na kuwataka mashabiki kutambua kuwa matokeo ni sehemu ya mchezo wa soka.

“Imewachukua Kolo miaka mitatu na miezi mitano kupata ushindi wa kwanza kwenye ligi mbele yetu. That’s football na fair play kwao kwa dakika 90 nzuri,” aliandika Kamwe.

Amesema Yanga haiwezi kushinda kila mchezo wa dabi, akisisitiza kuwa kupoteza mchezo mmoja hakumaanishi kuwa timu hiyo imepoteza nafasi ya kuwania ubingwa wa ligi msimu huu.

“Tusingeweza kushinda kila siku, kila mechi ya derby. Haiwezekani, unless umejua mpira kupitia TikTok,” aliongeza.

Kamwe amebainisha kuwa bado kuna mechi nyingi za kuchezwa katika ligi hiyo, hivyo Yanga ina nafasi ya kurejea kileleni mwa msimamo kwa kufanya vizuri katika michezo inayofuata.

Amesema jukumu la kikosi hicho kwa sasa ni kuongeza nguvu na kuhakikisha kinarejea katika nafasi ya juu ya msimamo, akieleza kuwa mbio za ubingwa bado hazijaamuliwa.

Aidha, kiongozi huyo ameitaka timu kuelekeza nguvu zake katika mashindano ya CAF Champions League, ambako Yanga inakabiliwa na mchezo muhimu wa kuwania tiketi ya kufuzu hatua ya makundi.

Kwa mujibu wa Kamwe, mchezo huo ni muhimu sana kwa klabu hiyo, akionya kuwa kushindwa kupata matokeo yanayohitajika kunaweza kuleta maumivu makubwa zaidi kwa timu na mashabiki wake.

Ameitaka benchi la ufundi pamoja na wachezaji kutafakari makosa yaliyojitokeza katika mchezo dhidi ya Simba na kuyafanyia kazi wakati wa mazoezi ili kurekebisha mapungufu kabla ya mchezo huo muhimu.

Kamwe amehitimisha kwa kuwahimiza mashabiki wa Yanga kuendelea kuwa na imani na timu yao, akisisitiza kuwa mwisho wa msimu ndio utakaotoa picha halisi ya mafanikio ya timu katika mbio za ubingwa.

“Daima mbele wanangu. Atakayecheka mwisho wa msimu ndiye atakayecheka vizuri,” alisisitiza Kamwe.