Matukio Daima Media, Morogoro
ASKARI saba wa Jeshi la Polisi waliojeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea eneo la Magole, wilayani Kilosa,Mkoani Morogoro wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi, huku hali zao zikiripotiwa kuendelea vizuri.
Taarifa hiyo imetolewa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji, wakati wa shughuli ya kuuaga miili ya askari watatu waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea Oktoba 8, 2026.
Askari waliofariki ni G9771 Sajenti Abdallah Ramadhani (37), aliyekuwa dereva wa gari la Polisi lenye namba za usajili PT 5361 GMW, PC Rehoboan Marko (32) na PC Michael Lucian (23).
Akizungumza katika shughuli hiyo leo, Oktoba 10, 2026, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura, amekiagiza Kikosi cha Usalama Barabarani kusimamia kwa ukamilifu utekelezaji wa sheria za barabarani, akisema uzembe wa kutokuzingatia sheria hizo unachangia ajali nyingi.
Wambura amewataka madereva kufuata sheria na kuchukua tahadhari ili kuepusha vifo na majeruhi, akieleza kuwa jeshi limepata pigo kwa kuwapoteza askari waliokuwa tegemeo katika majukumu yao.
“Jeshi limepata pigo kwa kuondokewa na askari wengi katika kipindi kifupi, ni askari tuliokuwa tunawategemea,” amesema.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amesema jeshi limepoteza askari makini, baadhi yao wakiwa wakufunzi wa mafunzo ya kijeshi.
Wakati huo huo, utambuzi wa mabaki ya miili ya watu waliofariki katika ajali ya basi la Green Line na lori eneo la Mkambarani, wilayani Morogoro, unaendelea. Mkemia Mkuu wa Serikali anachukua sampuli za vinasaba vya mabaki ya miili pamoja na baadhi ya ndugu waliojitokeza kusaidia utambuzi wa marehemu.



