Dar es Salaam. Serikali inapaswa kuanzisha mfumo maalumu wa kitaifa wa kusimamia miradi ya afya, utakaohakikisha fedha zinatolewa kwa wakati, uwezo wa wakandarasi unathibitishwa kabla ya kupewa kazi na mikataba inasimamiwa kwa karibu hadi mradi unapokamilika na kuanza kutoa huduma.
Hayo ni miongoni mwa mapendekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya, viongozi wa kisiasa, wananchi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wakisisitiza kuwa suluhisho la ucheleweshaji wa miradi ya afya linahitaji mabadiliko katika mfumo mzima wa utekelezaji, badala ya kutegemea hatua za dharura baada ya mradi kusuasua.
Mfumo huo unapendekezwa uwe na uwezo wa kuonesha kwa wakati maendeleo ya kila mradi, fedha zilizotengwa na zilizotolewa, kiwango cha utekelezaji, changamoto zinazoukabili na hatua zinazopaswa kuchukuliwa pale ratiba inapokiukwa.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Alex Msoka, anasema Serikali inapaswa kuanza kwa kufanya tathmini ya haraka ya miradi yote ya hospitali iliyochelewa nchini ili kubaini hali halisi kabla ya kuamua hatua za kuchukua.
“Jambo la kwanza ni kufanyika kwa tathmini ya haraka ya miradi yote ya hospitali iliyochelewa, ikiwamo kubaini asilimia ya utekelezaji, sababu za uchelewaji, fedha zilizotumika na fedha zinazohitajika kukamilisha mradi,” anasema.
Baada ya tathmini hiyo, anapendekeza miradi yenye umuhimu mkubwa kwa wananchi ipewe kipaumbele, iwe na muda maalumu wa kukamilika na mpango wa utekelezaji unaoweza kupimwa na kufuatiliwa.
Kwa Dk Msoka, mfumo huo haupaswi kuishia katika kujua mradi umefikia wapi, bali unatakiwa kuweka wazi nani anawajibika kwa kila hatua na nini kinapaswa kufanyika pale mkandarasi au taasisi inayohusika inaposhindwa kutekeleza wajibu wake.
Anasema pale mkandarasi anaposhindwa kutekeleza majukumu yake, hatua za kimkataba zinapaswa kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria bila kusubiri ucheleweshaji uongezeke na kuathiri gharama na muda wa mradi.
Pendekezo lingine ni kubadili mfumo wa upangaji na utoaji wa fedha za miradi ya afya.
Wadau wanataka Serikali ijiridhishe kabla ya kuanza mradi kwamba ina mpango wa fedha unaoweza kuufikisha hadi kukamilika, badala ya kuanza ujenzi bila uhakika wa mtiririko wa fedha.
Kwa mujibu wa hoja zinazotolewa, utoaji wa fedha unapaswa kuendana na ratiba ya ujenzi na hatua zilizofikiwa, huku malipo yakifanyika kwa kazi iliyotekelezwa na kuthibitishwa.
Mbunge wa Singida Mjini, Yagi Kiaratu, anasema Serikali inapaswa kutoa kipaumbele kwa kukamilisha miradi iliyoanza kabla ya kuanzisha mingine.
“Ushauri wangu kwa Serikali ni ichukue jitihada za kuhakikisha kwanza miradi ya zamani inakamilika kuliko kuanzisha mingine. Tukimaliza iliyopo ndipo tuanze mingine kulingana na mahitaji,” anasema.
Kiaratu anasema utoaji wa fedha kwa awamu ndogo ndogo unaweza kuchangia miradi kusuasua na kuongeza gharama, hivyo utekelezaji wa bajeti unapaswa kwenda sambamba na upatikanaji wa fedha kwa wakati.
Kuhusu mikataba, mapendekezo ya CAG yanaweka mkazo katika hatua ambayo mara nyingi huamua hatima ya mradi kabla hata ujenzi haujaanza, katika uchaguzi wa mkandarasi.
CAG, Charles Kichere, anasisitiza umuhimu wa kuzingatia taratibu za ununuzi na kufanya tathmini ya kutosha ya uwezo wa mkandarasi kabla ya kumpa mkataba.
Kwa mantiki hiyo, bei ya chini pekee haipaswi kuwa msingi wa uteuzi. Uwezo wa kifedha, kitaalamu na kiutendaji wa mkandarasi kutekeleza mradi kwa muda uliokubaliwa unapaswa kuthibitishwa.
CAG pia anapendekeza usimamizi na ufuatiliaji wa mikataba uimarishwe ili kuhakikisha kazi zinatekelezwa kwa mujibu wa masharti, gharama na muda uliokubaliwa.
Pale mkandarasi anaposhindwa kutekeleza wajibu wake, hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa mkataba na sheria za ununuzi.
Teknolojia itumike katika ufuatiliaji
Mbunge Kiaratu anapendekeza Serikali kutumia mifumo ya kidijitali kufuatilia maendeleo ya miradi kwa wakati halisi.
Kwa mfumo huo, taarifa za utekelezaji, matumizi ya fedha na hatua iliyofikiwa zinaweza kupatikana kutoka ngazi ya eneo la mradi hadi Serikali Kuu.
“Mfumo huo ni mzuri kwa sababu unaleta uwazi. Rai yangu ni uboreshwe vizuri na usomane kuanzia chini mpaka juu. Tukienda hapo, kila kitu kitakuwa wazi na usimamizi utakuwa rahisi,” anasema.
Mfumo wa aina hiyo unaweza pia kusaidia kubaini mapema mradi unaoanza kutoka kwenye ratiba, badala ya kusubiri ucheleweshaji uwe mkubwa ndipo uongozi uchukue hatua.
Wadau pia wanataka taarifa za miradi ziwe wazi kwa wananchi wanaotarajia kunufaika na huduma hizo.
Rehema Jonas, mkazi wa Singida, anasema wananchi wanapaswa kujua mradi umefikia hatua gani, muda uliopangwa wa kukamilika na namna fedha za umma zinavyotumika.
“Serikali inapaswa kuhakikisha mikataba inasimamiwa ipasavyo na hatua zinachukuliwa kwa wale wanaochelewesha utekelezaji bila sababu za msingi. Wananchi tunahitaji kuona miradi inayotumia fedha za umma inakamilika na kuanza kutoa huduma,” anasema.
Kwa mtazamo wake, uwazi wa taarifa unaweza kuongeza shinikizo la uwajibikaji na kupunguza sintofahamu kuhusu matumizi ya fedha za umma.
Singida iwe kipimo cha utekelezaji
Mapendekezo hayo yanapata uzito katika Mkoa wa Singida, ambako ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa umekuwa sehemu ya mjadala kuhusu ucheleweshaji wa miradi ya afya.
Badala ya kuangalia mradi huo kama changamoto ya Singida pekee, wadau wanaona unapaswa kuwa sehemu ya tathmini pana ya namna miradi ya afya inavyopangwa, kufadhiliwa na kusimamiwa nchini.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Jessica Lebba, anasema uongozi wa mkoa na hospitali umeweka mkakati wa kuhakikisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa unakamilika ndani ya muda wa mkataba na kwamba ukaguzi wa mara kwa mara unafanyika kufuatilia kasi na ubora wa kazi.
Kwa mujibu wa Dk Lebba, kukamilika kwa hospitali hiyo kutasaidia kupunguza gharama za rufaa na safari za wagonjwa, huku wananchi wakipata huduma za kibingwa karibu na maeneo yao.
Katika ngazi ya jamii, Kamati za Afya za Vituo vya Huduma za Afya (HFGC) zinaweza kuwa sehemu ya mfumo huo wa ufuatiliaji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe, anasema kamati hizo zinapaswa kupata mafunzo ya awali kuhusu usimamizi wa ujenzi, upokeaji wa miradi na ufuatiliaji wa ubora wa kazi.
Anasema pia zinapaswa kushirikishwa katika hatua muhimu za miradi, ikiwamo uchaguzi wa wakandarasi na makabidhiano.
Hii inaweza kuongeza ufuatiliaji kutoka ngazi ya jamii na kuwezesha changamoto kubainika mapema kabla hazijageuka kuwa ucheleweshaji mkubwa.
Kwa wananchi, kipimo cha mwisho cha mafanikio ya mradi wa afya si kukamilika kwa jengo pekee, bali uwezo wake wa kuanza kutoa huduma zilizokusudiwa.
Rama Rashid, mkazi wa Singida Mjini, anasema Serikali inapaswa kuwa na mkakati maalumu kwa miradi ya afya kwa sababu inahusisha moja kwa moja maisha ya wananchi.
“Miradi kama hospitali haipaswi kusubiri muda mrefu kukamilika kwa sababu kila siku wananchi wanahitaji huduma,” anasema.
Rais wa MAT, Dk Msoka, anaongeza kuwa uboreshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida unapaswa kwenda sambamba na kuwepo kwa muunganiko mzuri wa huduma za afya na usafiri ili wagonjwa waweze kufika hospitalini kwa wakati.
Kwa hiyo, mfumo unaopendekezwa unapaswa kuanzia kabla ya ujenzi kwenye upangaji na bajeti na kuendelea hadi hospitali inapokabidhiwa, kuwekewa vifaa, wataalamu na kuanza kutoa huduma.
Hapo ndipo suluhisho la ucheleweshaji wa miradi ya afya linapoweza kutoka kwenye kufuatilia tatizo baada ya kutokea na kwenda kwenye kuzuia tatizo kabla halijatokea.
Badala ya Serikali kusubiri mradi uchelewe, mfumo huo utawezesha kubaini mapema upungufu wa fedha, udhaifu wa mkandarasi, kuchelewa kwa malipo au changamoto nyingine na kuchukua hatua kabla gharama haijawa kubwa zaidi.
Kwa Dk Msoka, huo ndio msingi wa mfumo wa kitaifa wa usimamizi wa miradi ya afya unaopaswa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi, bajeti ya mradi hadi kukamilika na kuanza kutoa huduma, pamoja na uwajibikaji wa wazi kwa kila taasisi na kiongozi mwenye dhamana.


