SIRRO ATAKA FURSA YA BIASHARA UKANDA WA MAZIWA MAKUU ITUMIKE VIZURI

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

MKUU wa mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro amewataka wafanyabiashara wa mkoa huo kutumia fursa ya mkoa huo kupakana na nchi za ukanda wa maziwa makuu kufanya biashara zao kuwa na tija kubwa wakati huu ambao serikali imeweka mazingira mazuri kwao kwenyee sekta ya biashara.

Balozi Sirro alisema hayo katika kikao kilichoandaliwa na Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC) na wafanyabiashara wa mkoa Kigoma ili kutoa taarifa ya mabadiliko ya Muundo na wajibu wa sasa wa TNCC kutoka iliyokuwa Chemba ya wafanyabiashara ,wenye viwanda na kilimo (TCCIA).

Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya Kigoma,Dk.Rashid Chuachua Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa wakati huu ambao mkoa Kigoma umeteuliwa kuwa mkoa wa biashara na uchumi kwa ajiili ya soko la nchi za ukanda wa maziwa makuu serikali imefanya mambo mengi kuchochea shughuli za biashara mkoani humo.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa katika kutekeleza hilo serikali imeweka mazingira rahisi na wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji wa biashara wenye tija hivyo wafanyabiashara wa mkoa Kigoma wanapaswa kutumia nafasi hiyo kutekeleza wajibu wao baada ya serikali kufanya majukumu yake.

Awali akitoa maelezo kuhusu mkutano huo unaojulikana kama Kigoma Bussines Break Fast,Meneja wa TNCC mkoa Kigoma,Prosper Guga  alisema kuwa baada ya mabadiliko ya muundo na majukumu ya TNCC hawajapata nafasi ya taasisi hiyo na wafanyabiashara kukaa pamoja kuelezana kuhusu mabadiliko hayo ili waweze kuuliza na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusiana na taasisi hiyo.

Guga alisema kuwa mkoa Kigoma unatekeleza mpango mkubwa wa serikali wa kuinua biashara na uwekezaji kwenda nchi za maziwa makuu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya dira ya Taifa hivyo mkutano huo umekuja na kuwapa nafasi ya kukaa na kuzungumza kwa pamoja namna ya kuliendea jambo hilo kwa pamoja bila kuachwa mtu nyuma sambamba na kuzifanya biashara kuwa na tija kwa kuondoa vikwazo mbalimbali vya kibiashara.