Nyaisonga aonya dhidi ya waganga wa kienyeji – HabariLeo

KIGOMA: RAIS wa Baraza la Maaskofu Mashariki mwa Afrika (AMECEA), Askofu Gervas Nyaisonga, ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo la Mbeya, amewataka Watanzania wenye changamoto za macho kupata matibabu kutoka kwa wataalamu wenye taaluma badala ya kwenda kwa waganga wa kienyeji ambao, amesema, matibabu yao hayaaminiki.

Askofu Nyaisonga alitoa kauli hiyo wakati akizindua jengo na huduma za matibabu ya macho ya kibingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kabanga, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.

Alisema matibabu ya macho, hasa huduma za kibingwa, ni muhimu kwa maisha ya wananchi, hivyo ni lazima kuhakikisha huduma hizo zinatolewa na madaktari waliosomea taaluma hiyo na kuidhinishwa na mamlaka husika za Serikali.

“Matibabu ya macho ni huduma nyeti na muhimu kwa maisha ya Mtanzania. Ni muhimu wananchi kuhakikisha wanapata huduma kutoka kwa wataalamu wenye taaluma na wanaoaminika,” alisema.

Alisema matatizo ya macho yamekuwa changamoto kwa Watanzania wengi, hivyo wananchi wanapaswa kufanya uchunguzi wa afya ya macho mara kwa mara badala ya kusubiri hadi tatizo liwe kubwa ndipo watafute matibabu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Siro, ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Joseph Murimi, alisema uzinduzi wa jengo na uboreshaji wa huduma za macho ni hatua muhimu, lakini kinachopaswa kupewa kipaumbele ni kuhakikisha huduma hizo zinatoa matokeo kwa wananchi.

Balozi Siro alisema huduma za matibabu ya macho zimekuwa changamoto kwa wananchi wengi mkoani Kigoma, hivyo kusogezwa kwa huduma za kibingwa karibu na wananchi kutasaidia kupunguza safari za kwenda katika hospitali kubwa za kitaifa nje ya mkoa huo.

Awali, Meneja Mkazi wa Programu ya Macho kutoka Shirika la TanZanEye, Ryner Linuma, ambalo limefadhili mradi huo katika Hospitali ya Kabanga inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma, alisema uzinduzi wa jengo hilo ni hatua kubwa katika kuboresha huduma za macho mkoani humo.

Alisema mradi huo umegharimu jumla ya Sh bilioni moja, zikijumuisha ujenzi wa jengo, ununuzi wa vifaa tiba na samani.

Alisema Sh milioni 647 zitatumika kununua vifaa vitakavyowezesha kutolewa kwa huduma za kibingwa za macho, sambamba na kumwezesha daktari mmoja kupata mafunzo ya ubingwa katika upasuaji wa macho.

Kwa mujibu wa Linuma, hatua hiyo itafanya hospitali hiyo kuwa na madaktari wawili wenye uwezo wa kutoa huduma za kibingwa za macho, hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi wa Kigoma.