Na Fadhili Abdallah,Kigoma
HUDUMA za matibabu ya kibingwa ya macho zimeanzishwa mkoani Kigoma mpango ambao unaelezwa utapunguza changamoto ya wananchi wa mkoa huo wanaohitaji matibabu ya kibingwa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo kwenye hospitali kubwa za kitaifa nje ya mkoa Kigoma.
Hali hiyo inakuja kufuatia hospitali ya rufaa ya Kabanga iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma kuzindua jengo la matibabu ya macho lenye huduma zote za vifaa vya upimaji, wataalam akiwemo Daktari bingwa wa macho ambaye anaweza kufanya upasuaji na kusimamia matibabu ambayo hayakuwahi kufanyika mkoani humo.
Meneja Mkazi wa program ya macho kutoka Shirika la TanZanEye, Ryner Linuma ambalo limefadhili mradi huo kwa hospitali hiyo ya Kabanga inayomilikiwa na Kanisa katoliki jimbo la Kigoma alisema kuwa kuzinduliwa kwa jengo hilo kunaleta mapinduzi makubwa ya utoaji wa huduma za macho mkoani Kigoma kufikia matibabu ya Kibingwa.
Meneja huyo alisema kuwa kiasi jumla ya shilingi Bilioni moja ambazo zinajumuisha ujenzi wa jengo, vifaa tiba na samani za jengo hilo jipya huku kiasi cha shilingi milioni 647 kikitarajia kutumika kununua vifaa ambavyo vitawezesha huduma za kibingwa kufanyika sambamba na kusomesha daktari bingwa wa upasuaji wa macho ambapo itafanya huduma hizo kuwa na madaktari wawili wanaoweza kutoa huduma za kibingwa za macho.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo Rais wa Mabalaza ya Maaskofu Mashariki ya Afrika (AMECEA), Askofu Gervas Nyaisonga ambaye ni Askofu Mkuu wa jimbo la Mbeya alisema kuwa magonjwa ya macho yamekuwa changamoto kubwa kwa Watanzania wakiwemo wananchi wa mkoa Kigoma hivyo kuwepo kwa huduma hiyo hasa huduma za kibingwa zinapaswa ziwe endelevu ili kuondoa changamoto ya watu kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.
Katika uzinduzi huo Askofu Nyaisonga aliwataka wananchi wa mkoa Kigoma kuanza kufanya uchunguzi wa matatizo ya macho mapema badala ya kusubiri ugonjwa ukomae akihimiza pia kutumia huduma za madaktari wenye taaluma badala ya kwenda kwa waganga wa kienyeji kwani matibabu hayo hayana uhalisia.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa Kigoma,Balozi Simon Siro ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa wilaya Kasulu , Kanali Joseph Murimi alisema kuwa kufunguliwa kwa jengo hilo na uboreshaji wa huduma ni jambo moja lakini muhimu kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaleta matokeo kwa wananchi.







