WIZARA YA KILIMO YAFIKIA MAKUBALIANO NA WACHAKATAJI WA NGANO KUNUNUA NGANO YOTE INAYOZALISHWA NCHINI

 Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko imefikia makubaliano na Chama cha Wachakataji wa Ngano kuhakikisha ngano inayozalishwa nchini inanunuliwa kwa bei ya Shilingi 1,200 kwa kilo kama bei ya mkulima, kwa lengo la kuwahakikishia wakulima soko, kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa ngano kutoka nje ya nchi.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa ngano Dodoma, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, ameelekeza COPRA kuimarisha ufuatiliaji wa makubaliano na kuratibu ushirikiano na taasisi nyingine za Wizara ya Kilimo na Serikali,  kuwaunganisha wakulima na wanunuzi na kuhakikisha ngano inayozalishwa inakidhi viwango na ubora unaohitajika na viwanda.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachakataji wa Ngano, Bw. Hussein Suphian, amesisitiza umuhimu wa upatikanaji wa ngano ya ndani yenye ubora unaokidhi mahitaji ya viwanda. Aidha, amehakikishia Wizara utayari wao kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa mipango inayowekwa na serikali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Bi. Irene Madeje Mlola, amesema Mamlaka itaendelea kuratibu, kufuatilia na kutekeleza maelekezo ya Waziri kwa kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora, huduma za ugani, kufuatilia taarifa za uzalishaji, kuunganisha wakulima na wachakataji na kufuatilia utekelezaji wa makubaliano kwa kushirikiana na Wizara, Halmashauri na taasisi nyingine za serikali.

Ushirikiano huo unalenga kuimarisha soko la ngano ya ndani, kuongeza tija kwa wakulima, kuhakikisha viwanda vinapata malighafi na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika uagizaji wa ngano.

Mahitaji ya ngano nchini yanakadiriwa kuzidi tani milioni moja kwa mwaka, huku uzalishaji wa ndani ukifikia takribani tani 152,096 katika msimu wa 2025/2026. Serikali inalenga kuongeza uzalishaji hadi tani 200,000 katika msimu wa 2026/2027, tani 300,000 katika msimu wa 2027/2028 na tani 450,000 ifikapo mwaka 2030.