NA Matukio Daima Media, Morogoro
Miili 29 imepatikana na majeruhi 30 wameokolewa katika ajali mbaya iliyohusisha basi la abiria la Dream Line na lori lililokuwa limebeba miti aina ya mirunda katika eneo la Mkambarani, Kikombe cha Chai, barabara kuu ya Morogoro -Dar es salaam mkoani Morogoro, huku mamlaka zikitarajiwa kufanya uchunguzi zaidi ili kubaini idadi kamili ya watu waliofariki.
Ajali hiyo imetokea usiku wa Oktoba 8, mwaka huu, baada ya lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 902 ENG kugongana uso kwa uso na basi lenye namba T 672 ELT lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Mbeya.
Basi hilo liliteketea kwa moto, hali iliyofanya zoezi la uokoaji kuwa gumu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori kujaribu kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari katika eneo lisiloruhusiwa.
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Joseph Mwasabeja, amesema kikosi chake kiliongeza magari ya uokoaji baada ya kubaini ukubwa wa ajali na moto uliokuwa umesambaa.
Mwasabeja amesema hatua ya kwanza ilikuwa kuokoa maisha ya watu, huku akieleza kuwa kikosi chake kilifanikiwa kutoa miili 29 na kuwasaidia majeruhi 30 kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro. Ameongeza kuwa idadi rasmi ya vifo na majeruhi inapaswa kuthibitishwa na wataalamu wa afya.
Miongoni mwa manusura ni Obtato Mwanyigu, ambaye amesema alishuhudia lori likihama upande wake wa barabara na kuelekea upande wa basi walimokuwa wakisafiria.
Abiria wengine wamesema ajali hiyo ilikuwa mbaya sana na kutoa wito kwa madereva kuchukua tahadhari wanapotumia barabara.
Ajali nyingine iliyothibitishwa na Polisi imetokea eneo la Miti Bora, kati ya Dakawa na Dumila wilayani Mvomero, ikihusisha gari la Polisi lililokuwa na askari waliokuwa kazini na lori aina ya Scania mali ya kampuni ya ATT. Kantimbo amesema watu wanne walifariki katika ajali hiyo na majeruhi kupelekwa hospitalini.
Wakati uchunguzi ukiendelea, mamlaka husika zinatarajiwa kutoa taarifa itakayobainisha idadi kamili ya watu waliofariki katika ajali ya Mkambarani, pamoja na utambulisho wa waathirika.FOMU ZA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA 2027 MEDALA HIGH SCHOOL IDODI IRINGA










