
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza mpango wa kusitisha matumizi ya kadi za kukwangua za muda wa maongezi ya simu kuanzia Januari 1, 2027, na kuhamia kwenye mfumo wa kidijitali wa kuongeza muda wa maongezi.
Kwa mujibu wa taarifa ya umma iliyotolewa na TCRA Oktoba 8, 2026, hatua hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha na mawasiliano za kidijitali, kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi usiotumia fedha taslimu.
TCRA imeeleza kuwa mpango huo unalenga kuongeza urahisi wa upatikanaji wa muda wa maongezi, kupunguza matumizi ya kadi halisi za kukwangua na kuimarisha matumizi ya njia za kidijitali katika huduma za mawasiliano.
Kwa mujibu wa TCRA, zoezi la majaribio la kusitisha matumizi ya kadi za kukwangua za muda wa maongezi litafanyika kuanzia Oktoba 1, 2026, katika mikoa na wilaya zilizotajwa na mamlaka hiyo.
Maeneo hayo ni Mkoa wa Dar es Salaam, Wilaya ya Dodoma, Chamwino, Kondoa Mjini na Kongwa katika Mkoa wa Dodoma; Wilaya ya Arusha, Arusha Jiji na Karatu katika Mkoa wa Arusha; Nyamagana, Ilemela na Misungwi katika Mkoa wa Mwanza; pamoja na Jiji la Mbeya, Wilaya ya Mbeya na Mbarali katika Mkoa wa Mbeya.
TCRA imesema zoezi hilo litahusisha uhamasishaji wa watumiaji wa huduma za mawasiliano kuhusu matumizi ya njia za kidijitali za kuongeza muda wa maongezi badala ya kutegemea kadi za kukwangua.
TCRA imeeleza kuwa watumiaji wataendelea kupata huduma za kuongeza muda wa maongezi kupitia njia mbalimbali za kidijitali zinazotolewa na watoa huduma za mitandao ya simu na washirika wao walioidhinishwa.
Njia hizo ni pamoja na kununua muda wa maongezi moja kwa moja kupitia akaunti za fedha za simu kwa kutumia huduma za USSD au programu za simu; mashine za kujihudumia za benki (ATM) na mawakala wa benki; pamoja na mifumo mingine ya kidijitali inayotolewa na watoa huduma za mitandao ya simu na washirika wao.
Aidha, watumiaji wanahimizwa kujielimisha kuhusu njia hizo ili kuendelea kupata huduma bila usumbufu wakati wa utekelezaji wa mpango huo.
KADI ZILIZO MIKONONI MWA WATUMIAJI
Kuhusu watumiaji ambao bado wana kadi za kukwangua za muda wa maongezi, TCRA imesema katika maeneo ya majaribio, kadi ambazo zitakuwa hazijatumika baada ya Januari 1, 2027, hazitatumika tena, na watumiaji watahitajika kuwasiliana na watoa huduma wao kupitia vituo vilivyoidhinishwa ili kupata msaada wa kuzitumia.
Hata hivyo, watumiaji katika maeneo hayo ambao watakuwa na salio la kadi za kukwangua watashauriwa kutumia njia za kidijitali za kuongeza muda wa maongezi kadiri mpango utakavyoendelea kutekelezwa.

