Tanzania na Msumbiji Zasaini Makubaliano ya Ulinzi na Usalama

Global Publishers
October 8, 2026
0 views
0 Comments

Mawaziri wa Ulinzi wa Tanzania na Msumbiji wamesaini mikataba ya makubaliano yenye lengo la kuimarisha usalama na ushirikiano wa kiulinzi kati ya nchi hizo mbili.

Makubaliano hayo yamesainiwa wakati wa kufungwa kwa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ulinzi na Usalama kati ya Tanzania na Msumbiji, uliofanyika katika Ukumbi wa The Aga Khan Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Luteni Kanali Kelvin Baraka Byabato, amesema moja ya madhumuni makuu ya kikao hicho ni kuendeleza maono ya waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Hayati Samora Machel wa Msumbiji.

Amesema mkutano huo unalenga kuendelea kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Msumbiji katika masuala ya ulinzi na usalama, pamoja na kujenga mazingira ya amani na utulivu kati ya mataifa hayo jirani.