WANANCHI WALIA UKOSEFU WA VYOO KITUO CHA AFYA ILAGALA

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Wananachi wa kata ya Ilagala katika halmashauri ya wilaya Uvinza mkoani Kigoma wamelalamikia ukosefu ya huduma ya vyoo katika kituo cha afya Ilagala hali ambayo inawapa taabu wanapofika kupata huduma za matibabu kituoni hapo.

Wananchi hao walitoa malalamiko hayo wakati wa mkutano wa mbunge wa jimbo la Kigoma Kusini, Nuru Kashakari Maarufu kandahari ambapo walisema kuwa kutokana na ukosefu wa huduma hiyo inawalazimu kutafuta namna ya kuweza kupata huduma ya choo nje ya kituo hicho cha afya katika huduma ya kulipia.

Mmoja wa wananchi wa jimbo hilo, Magdalena Laurent kutoka kijiji cha Ilagala            alisema kuwa hasa wanawake wamekuwa wakihangaika kutokana na ukosefu wa vyoo kwenye kituo hicho cha afya na kumuomba mbunge asaidia kuondoa changamoto hiyo.

Akizungumzia changamoto hiyo Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya Uvinza, Cleement Morabu alikiri kuwepo na changamoto ya upungufu wa vyoo katika kituo hicho cha afya baada ya vyoo vya wagonjwa vilivyokuwepo awali kujaa na kwamba tayari mpango wa ujenzi wa vyoo vingine umeandaliwa na idara imeshaomba fedha kwa ajili ya kuondoa changamoto hiyo.

Kutokana na hali hiyo Mbunge wa jimbo la Kigoma Kusini, Nuru Kashakari (Kandahari) ametoa jumla ya shilingi milioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa matundu mawili ya vyooo sambamba na kusaidia ujenzi wa wodi ya wagonjwa ambayo ujenzi wake umekwama.

Kandahari ambaye yuko kwenye ziara ya jimbo la kuzungumza na wananchi na kutembelea miradi mbalimbali ameitaka Halmashauri kuweka mipango ya kushughulikia changamoto za huduma za wananchi ili kuweza utoaji huduma kwa wananchi kuwa rahisi.