SUA YATOA TUZO 242, YAJIANDAA KUTUNUKU SHAHADA KWA WANAFUNZI 3,309

Matukio Daima Media

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kuenzi utamaduni wa ubora na mafanikio kwa kutoa tuzo 242 kwa washindi 205, wakati kikijiandaa na Sherehe za 48 za Mahafali zinazotarajiwa kufanyika Alhamisi, Oktoba 8, 2026.

Akizungumza katika Sherehe za 43 za Utoaji wa Zawadi za SUA, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Raphael Chibunda, alisema tuzo hizo zimetolewa kwa kutambua na kuhamasisha ubora katika taaluma, uongozi na utafiti.

Alisema tuzo hizo zimefanikishwa na mchango wa wafadhili 56 na zinajumuisha zawadi za kitaaluma 214, tuzo za uongozi 23 pamoja na zawadi tano za utafiti.

“Tunayo furaha kutoa tuzo 242 kwa washindi 205 ambazo zimefanikishwa kupitia mchango wa ukarimu wa wafadhili 56,” alisema Prof. Chibunda.

Kwa mujibu wa Prof. Chibunda, wanafunzi 45 miongoni mwa waliotambuliwa wamefanikiwa kupata zaidi ya tuzo moja, huku tuzo 18 zikitolewa kwa washindi zaidi ya mmoja.

Tukio hilo limekuja wakati SUA ikielekea katika Sherehe zake za 48 za Mahafali, ambapo jumla ya wanafunzi 3,309 wanatarajiwa kutunukiwa shahada katika programu 69.

Prof. Chibunda aliwapongeza washindi wote wa tuzo hizo na kuwataka kuendeleza kiwango cha juu cha utendaji walichokionesha ili kiwe msingi wa mafanikio yao katika maisha ya kitaaluma na kikazi.

“Tunawapongeza kwa dhati washindi wetu wote wa tuzo kwa ufanyaji vizuri wao na kuwahimiza kuendeleza moyo huu wa ubora wanaposonga mbele katika maisha yao ya kitaaluma na kikazi,” alisema.

Utafiti na uongozi watambuliwa

Mbali na mafanikio ya kitaaluma, SUA pia imetambua mchango wa watafiti na viongozi bora wa wanafunzi kupitia tuzo hizo.

Prof. Chibunda alisema utafiti na ubunifu ni miongoni mwa misingi muhimu ya majukumu ya SUA, hivyo watafiti watano wametambuliwa kwa kazi zao zilizoonyesha ubora wa kipekee na kuchangia katika kuongeza maarifa na maendeleo.

Aidha, viongozi bora wa wanafunzi wametambuliwa baada ya kuchaguliwa kupitia mchakato wa wazi na wa kidemokrasia, uliowapa wanafunzi nafasi ya kuwachagua wenzao walioonyesha uwezo wa uongozi.

Chuo pia kimeendelea kutoa Tuzo ya Jumuiya ya Wahitimu (Convocation) kwa Mwanafunzi Bora wa Shahada ya Umahiri (Masters), tuzo iliyoanzishwa mwaka 1989.

Tuzo hiyo hutolewa kwa kuzingatia vigezo maalumu, ikiwemo mhitimu kuwa na GPA ya 4.0 au zaidi, kukamilisha masomo yote katika SUA na kuwasilisha tasnifu ndani ya kipindi cha miaka miwili.

Prof. Chibunda alitoa shukrani kwa wafadhili 56 walioshiriki kufanikisha utoaji wa tuzo hizo, akisema mchango wao ni muhimu katika kujenga utamaduni wa ubora na kuwahamasisha wanafunzi na wafanyakazi kufanya vizuri.

Aliipongeza pia mitaa ya Ndaki, Shule, Kurugenzi na Idara za SUA kwa juhudi zao za kuhamasisha na kuratibu michango kwa ajili ya tuzo hizo.

Alisema SUA inaendelea kuboresha mazingira ya kitaaluma ili kutoa fursa kwa wanafunzi na wafanyakazi kufikia uwezo wao kamili, sambamba na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chuo unaolenga kuongeza ushindani wa taasisi hiyo na kukabiliana na mahitaji yanayobadilika ya jamii na soko la ajira.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Fabian Magawa Madele,akizungumza katika sherehe hiyo, aliitaka sekta ya mifugo kuongeza mchango wake katika pato la taifa, akisema kwa sasa sekta hiyo inachangia takribani asilimia sita pekee ya pato la taifa licha ya Tanzania kuwa na utajiri mkubwa wa mifugo.

Dkt. Madele alisema hayo Jumatano, Oktoba 7, 2026, wakati akizungumza katika Sherehe za 43 za Utoaji wa Zawadi za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), zilizofanyika chuoni hapo Morogoro.

Alisema Tanzania ina zaidi ya ng’ombe milioni 40 na zaidi ya mbuzi milioni 20, sambamba na mifugo mingine, hali inayotoa fursa kubwa ya kuifanya sekta hiyo kuwa injini muhimu zaidi ya uchumi wa taifa.

Kwa mujibu wa Dkt. Madele, ukubwa wa rasilimali hiyo ya mifugo unapaswa kuendana na mchango mkubwa zaidi katika uchumi, kupitia kuongeza tija, ubunifu, utafiti, uzalishaji wa bidhaa za mifugo na matumizi bora ya teknolojia.

Alisema uwepo wa idadi kubwa ya mifugo nchini unaonyesha fursa iliyopo, hivyo wataalamu na wadau wa sekta hiyo wanapaswa kuhakikisha rasilimali hiyo inatumika kwa tija na kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa uzalishaji.

Dkt. Madele, ambaye pia ni mhitimu wa SUA, alisema Chuo hicho kina nafasi muhimu katika kuzalisha wataalamu, maarifa na tafiti zitakazosaidia kuendeleza sekta ya mifugo na kilimo kwa ujumla.

Akizungumza na wanafunzi waliopata tuzo katika sherehe hizo, Dkt. Madele alisema utoaji wa zawadi ni zaidi ya kutambua mafanikio, bali ni ishara ya bidii, nidhamu, ustahimilivu na kiu ya kutafuta maarifa.

Aliwataka wanafunzi hao kutokuchukulia tuzo walizopata kama mwisho wa safari yao, bali wazitumie kama mwanzo wa majukumu na fursa kubwa zaidi katika maisha yao ya kitaaluma na kikazi.

“Leo, mnatambuliwa kwa mafanikio yenu. Yasherehekeeni, lakini msiyachukulie kama mwisho wa safari. Yachukulieni kama mwanzo wa majukumu makubwa zaidi na fursa kubwa zaidi,”alisema.

Alisema mafanikio ya kitaaluma hayaji kwa njia nyoofu, bali yanahitaji ukakamavu, huku akiwataka washindi kukumbuka changamoto walizopitia pamoja na watu waliowaunga mkono hadi kufikia hatua hiyo.

Dkt. Madele aliwataka wanafunzi hao kuwa tayari kukabiliana na vikwazo vitakavyoweza kujitokeza katika safari yao ya maisha, akieleza kuwa mafanikio yanahitaji uvumilivu na dhamira.

Aidha, aliwapongeza wahadhiri, watafiti, wataalamu wa maabara na wafanyakazi wa utawala wa SUA kwa mchango wao katika kuwajenga wanafunzi kitaaluma na kuwaandaa kuwa wataalamu na viongozi wa taifa.

Alisema mafanikio ya wanafunzi hao hayawezi kutenganishwa na mchango wa familia zao, wakiwemo wazazi, walezi, wenza, ndugu na marafiki, ambao wamekuwa msaada katika safari yao ya masomo.

Dkt. Madele alisema msaada wa kifedha, kihisia na kiushauri kutoka kwa familia na wadau wengine umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yaliyosherehekewa katika hafla hiyo.

Aliwataka kutumia maarifa kujenga taifa

Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Madele amewataka wanafunzi na wapokea zawadi kutumia mafanikio yao kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Aliwataka kuwa wabunifu, wenye nidhamu na uadilifu, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia maarifa waliyoyapata chuoni kutatua changamoto zinazolikabili taifa.

“Zaidi ya yote, tumieni maarifa yenu kutumikia binadamu na kujenga taifa letu,” alisema.

Alisema SUA itaendelea kuwa na nafasi muhimu katika kuzalisha maarifa, kuendeleza rasilimali watu, kuchochea mabadiliko katika kilimo na kuchangia maendeleo ya Tanzania.

Sherehe hizo za 43 za Utoaji wa Zawadi za SUA zimefanyika siku moja kabla ya Sherehe za 48 za Mahafali ya Chuo hicho, ambapo jumla ya wahitimu 3,309 wanatarajiwa kutunukiwa shahada katika programu 69.

…..