Magari mapya kuboresha huduma wananchi wa kasulu – HabariLeo

KASULU: Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Luteni Kanali Joseph Murimi, amezindua magari mawili mapya ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

Magari hayo ni basi la watumishi aina ya TATA lililonunuliwa kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri pamoja na Suzuki Jimny lililotolewa na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya shughuli za ugani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jana Oktoba 6, 2026, Luteni Kanali Murimi amesema basi hilo litasaidia kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya watumishi kwa kuwawezesha kufika kazini kwa wakati na kushiriki katika ziara na shughuli mbalimbali za kikazi.

Amesema upatikanaji wa usafiri kwa Divisheni ya Kilimo ni hatua muhimu katika kuweka mazingira bora kwa wataalamu kuwafikia wananchi, hususan wakulima ambao ni sehemu kubwa ya wakazi wa Halmashauri hiyo.

“Gari hili litarahisisha wataalamu kuwafikia wakulima na kutoa elimu ya kilimo itakayosaidia kuongeza uzalishaji wenye tija,” amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Samwel Kadogo, amewataka watumishi kulitunza basi hilo na kulitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, akisema upatikanaji wake utasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, CPA Francis Kafuku, amelishukuru Baraza la Madiwani kwa kuridhia ununuzi wa basi hilo, akisema litawawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao katika mazingira bora na kuwa na usafiri wa uhakika.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi, Magdalena Joseph amesema Halmashauri imekuwa ikitekeleza shughuli mbalimbali za kuwahudumia wananchi na kushiriki katika matukio ya kitaifa, huku changamoto ya usafiri ikiwa miongoni mwa vikwazo vilivyokuwepo.

Amesema uwepo wa basi hilo utarahisisha ushiriki wa watumishi katika shughuli hizo na kuongeza uwezo wao wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi.

Naye Hashim Kizigo amesema upatikanaji wa basi hilo utaongeza ushiriki wa watumishi katika shughuli za kijamii, ikiwemo misiba, ambazo hapo awali baadhi yao walishindwa kushiriki kwa wingi kutokana na changamoto ya usafiri.