KABLA YA KUSTAAFU, JENGA MAISHA YATAKAYOKULIPA BAADA YA AJIRA

 

Matukio Daima Media, Morogoro 

Miaka ya utumishi wa umma inapokaribia ukingoni, swali muhimu sio tu mtumishi atapokea kiasi gani cha mafao, bali ataishi vipi baada ya mshahara wa kila mwezi kusimama.

Serikali sasa inasisitiza maandalizi ya mapema ili kustaafu kusigeuke kuwa mwanzo wa matatizo ya kipato.

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Edith Rwiza, amewataka watumishi wanaokaribia kustaafu kuanza kutumia rasilimali walizonazo kujenga shughuli za kiuchumi zitakazowawezesha kuendelea kuzalisha kipato baada ya ajira.

Amesema kilimo, ufugaji na biashara ni miongoni mwa maeneo ambayo watumishi wanaweza kuwekeza mapema, badala ya kusubiri hadi watakapostaafu ndipo waanze kutafuta namna ya kujipatia kipato.

Kauli hiyo inaendana na hali ya maandalizi ya kustaafu nchini, ambapo FinScope Tanzania 2023 imebaini kuwa asilimia 28 ya Watanzania wenye umri wa miaka 55 au chini hawakuwa na mpango wa kustaafu.

Aidha asilimia 23 wametaja kilimo na ufugaji, huku asilimia 15 wakitaja biashara zao wenyewe kama sehemu ya mipango yao ya maisha ya baada ya ajira.

Kwa watumishi walio chini ya PSSSF, kustaafu kwa lazima ni miaka 60, huku kustaafu kwa hiari kukianza miaka 55. Hii ina maana kuwa mtumishi anaweza kuwa na miaka kadhaa ya kuandaa maisha yake kabla ya kufikia ukomo wa ajira.

Mkurugenzi wa Sehemu ya Usajili wa Shule, kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Patrick Leyana, amesema watumishi wanapaswa kutumia kipindi cha ajira kujenga vitega uchumi, ili baada ya kustaafu wasitegemee chanzo kimoja cha fedha.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo, Oliva Magambo, amesisitiza umuhimu wa kuanza kujifunza mapema namna ya kuendesha biashara na kusimamia uwekezaji, akieleza kuwa maandalizi ya kustaafu yanapaswa kuwa zaidi ya kutenga fedha.

Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania tayari kina programu zinazolenga kuwaandaa watumishi kwa maisha baada ya ajira, zikiwemo mafunzo ya upangaji wa maisha ya kustaafu, uendeshaji wa biashara, uwekezaji na usimamizi wa mafao.

Kwa mtumishi, hivyo, kustaafu kunaweza kuwa mwisho wa ajira lakini sio lazima kuwe mwisho wa uzalishaji; maandalizi anayoyafanya akiwa bado kazini ndiyo yanaweza kuamua aina ya maisha atakayoishi baada ya mshahara.

Mwisho