Mradi wa makazi waleta mapinduzi sekta ya nyumba Zanzibar – HabariLeo

Zanzibar. Kampuni ya Infinity Developments imeanza rasmi mauzo ya awamu ya kwanza katika mradi wa Infinity Hills Zanzibar huku nyumba 350 za makazi na maeneo 42 ya biashara zikiwekwa sokoni.

Taarifa za kimasoko zinabainishwa kuwa mwitikio wa awali ukitajwa kuwa mkubwa na miamala yenye thamani ya mabilioni ya shilingi tayari ikiwa imefanyika.

Mradi huo wa matumizi mchanganyiko unaotekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC), unalenga kutengeneza jamii jumuishi inayounganisha sekta za makazi, biashara, elimu na burudani katika eneo lililo karibu na Mji Mkongwe (Stone Town).

Infinity Hills ni miongoni mwa miradi mikubwa inayolenga kubadilisha namna watu wanavyoishi, kufanya biashara na kuwekeza Zanzibar, huku mpango wake mkuu ukijumuisha pia shule ya kimataifa ya GEMS ambayo inatarajiwa kujengwa ndani ya mradi huo.

Kwa mujibu wa Infinity Developments, maandalizi ya awali ya mradi huo yanaendelea na shughuli za ujenzi zinatarajiwa kuanza hivi karibuni, hatua itakayoutoa mradi kutoka katika hatua ya upangaji na uendelezaji kwenda kwenye utekelezaji wa miundombinu na majengo.

Mwitikio mkubwa wa wanunuzi

Mkuu wa Mauzo wa Infinity Hills, Hamida Swalehe, amesema mwitikio wa wanunuzi na wawekezaji umekuwa mkubwa tangu mradi huo ulipoanza kutangazwa, huku kampuni ikiwa tayari imerekodi miamala yenye thamani ya mabilioni ya shilingi.

“Mwitikio kuhusu Infinity Hills umekuwa wa kutia moyo sana. Tayari tumeshapokea miamala yenye thamani ya mabilioni ya shilingi za Kitanzania, jambo linaloonyesha imani ambayo wanunuzi wameweka katika mradi huu katika hatua hii ya awali,” amesema.

Amesema mwitikio huo unaonyesha imani ya wanunuzi katika eneo la mradi, mpango wake mkuu na thamani ya muda mrefu inayoweza kupatikana kutokana na kuwa sehemu ya jamii iliyopangwa kitaalamu karibu na Mji Mkongwe.

“Uzinduzi wa mauzo ya Awamu ya Kwanza unawapa wanunuzi fursa ya kuingia katika mradi katika hatua ya awali, wakati jamii hii pana ikiendelea kujengwa,” ameeleza.

Awamu hiyo inajumuisha majengo ya studio, nyumba zenye chumba kimoja na zenye vyumba viwili, pamoja na maeneo 42 ya biashara.

Kwa mujibu wa kampuni, nyumba hizo zimebuniwa kwa kuzingatia matumizi bora ya nafasi na mwanga wa asili, huku wakazi wakitarajiwa kuwa na fursa ya kupata huduma za kibiashara na huduma nyingine muhimu zilizo na karibu na mradi.

Elimu ilivyozingatiwa kwa ukubwa

Moja ya vipengele vinavyotajwa kuwa muhimu katika mpango mkuu wa Infinity Hills ni ujenzi wa shule ya kimataifa ya GEMS.

Shule hiyo inalenga kuongeza huduma za elimu ndani ya jamii hiyo na kuifanya Infinity Hills kuwa chaguo linaloweza kuvutia zaidi familia zinazotafuta makazi yanayounganisha nyumba, elimu na huduma za kila siku katika eneo moja.

Kwa Infinity Developments, uwepo wa shule hiyo ni sehemu ya dhana pana ya mradi ya kujenga jamii ambayo si mkusanyiko wa nyumba pekee, bali mazingira yenye huduma zinazokidhi mahitaji mbalimbali ya wakazi.

Infinity Hills ni mradi wa zaidi ya ujenzi wa nyumba

Infinity Hills imepangwa kuwa jamii ya matumizi mchanganyiko, ikiwa na maeneo ya makazi, biashara, ofisi, elimu, burudani na maeneo ya wazi.

Mpango mkuu unajumuisha bustani zenye mandhari nzuri, bwawa la kuogelea la jamii, migahawa, maeneo ya biashara na sehemu za watoto kuchezea.

Mradi huo pia unafaidika na ukaribu wake na maeneo ya pwani, huduma za Mji Mkongwe pamoja na vituo vya afya, mambo yanayotarajiwa kuongeza urahisi wa maisha kwa wakazi na kuvutia wawekezaji.

Awamu ya pili ya mradi inatarajiwa kuongeza idadi ya nyumba pamoja na jengo maalum la biashara. Jengo hilo limepangwa kuwa na maduka na maeneo ya chakula na vinywaji katika ghorofa za chini, huku ghorofa ya pili ikitarajiwa kuwa na ofisi za kisasa.

Utekelezaji

Meneja wa Mradi wa Infinity Hills, Michael John Makoye, amesema kampuni imejikita katika kuhakikisha kasi ya utekelezaji inaendelea huku maandalizi ya hatua inayofuata ya mradi yakiendelea.

“Kipaumbele chetu ni utekelezaji wenye nidhamu. Timu yetu inajiandaa kwa hatua inayofuata ya utekelezaji, na lengo letu litakuwa kutekeleza mradi kwa ufanisi, kudumisha ubora na kuhakikisha maendeleo yanaonekana wazi katika kipindi chote cha ujenzi,” amesema.

Ameeleza kuwa kampuni pia inakusudia kutoa taarifa za maendeleo ya mradi mara kwa mara ili kuwawezesha wanunuzi, wawekezaji na wadau wengine kufuatilia hatua mbalimbali za utekelezaji.

Hatua hiyo ni muhimu kwa mradi ambao tayari umeanza kuvutia wanunuzi kabla ya ujenzi wa majengo kuanza, kwani maendeleo yanayoonekana yatakuwa sehemu muhimu ya kujenga imani kwa wawekezaji na wanunuzi wapya.

Fursa za ajira na biashara

Mbali na ujenzi wa nyumba na miundombinu, Infinity Hills inatarajiwa kuwa na mchango mpana katika uchumi wa Zanzibar kupitia ajira, biashara na uhamishaji wa ujuzi.

Mradi huo unatarajiwa kutoa fursa kwa wafanyakazi na watoa huduma wazawa katika hatua za ujenzi na baadaye wakati wa uendeshaji wa jamii hiyo.

Afisa Mkuu wa Fedha wa Infinity Group, Rohit Kapoor, amesema miradi mikubwa ya uwekezaji ina faida lukuki za kiuchumi zinazovuka mipaka ya eneo la utekelezaji.

“Miradi mikubwa huzalisha mnyumbuliko wa faida za kiuchumi. Infinity Hills itasaidia kuleta ajira, fursa kwa biashara za wazawa, itaongeza shughuli za ziada za kiuchumi na itachangia mapato ya serikali huku mradi ukiendelea,” amesema.

Amebainisha kuwa kampuni inalenga kuhakikisha ukuaji wa Infinity Developments unaambatana na ushiriki mpana wa wazawa katika shughuli za kiuchumi zinazozalishwa na miradi yake.

“Nia yetu ni kuhakikisha kwamba ukuaji wa Infinity na uendelezaji wa miradi yetu unaleta ushiriki wenye maana wa kiuchumi na fursa ndani ya Zanzibar,” amesema.

Dhamira ya muda mrefu Zanzibar

Mkurugenzi Mtendaji wa Infinity Developments, Samuel Saba, amesema Infinity Hills ni sehemu ya dhamira ya kampuni ya muda mrefu ya kuwekeza Zanzibar kupitia miradi inayolenga kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.

“Infinity Hills inawakilisha dhamira yetu ya muda mrefu kwa Zanzibar. Lengo letu si tu kujenga nyumba za makazi, bali kutengeneza jamii iliyopangwa vizuri inayoleta pamoja makazi, biashara, elimu, burudani na maeneo ya umma, huku ikizalisha ajira na kuchangia maendeleo endelevu ya kiuchumi ya kisiwa hiki,” ameema.

Amesema kampuni inataka mradi huo uakisi uwezo wake wa kutekeleza miradi mikubwa kuanzia hatua za maandalizi hadi ujenzi na hatimaye makabidhiano kwa wanunuzi.

“Kwetu sisi, mradi huu pia unahusu utekelezaji. Tunataka kila hatua ya Infinity Hills, kuanzia maandalizi na ujenzi hadi kukamilika na makabidhiano, ionyeshe kiwango, ukubwa na uwezo wa utekelezaji ambao Infinity Developments inakusudia kuuleta Zanzibar,” alisema.

Kwa kuanza rasmi kwa mauzo ya awamu ya kwanza, Infinity Hills sasa inaingia katika hatua muhimu ya kubadili mpango wake kutoka kwenye michoro na maandalizi kwenda kwenye jamii inayotarajiwa kujengwa.

Kwa nyumba 350 na maeneo 42 ya biashara yaliyo sokoni, pamoja na mpango wa shule ya kimataifa ya GEMS na huduma nyingine zilizopangwa, mradi huo unaweka mkazo katika kuunganisha makazi, biashara, elimu na burudani katika jamii moja, huku ukilenga kuwa sehemu ya sura mpya ya maendeleo ya Zanzibar.