KILIMANJARO: Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umetunukiwa Cheti cha ISO 9001:2015 cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hatua inayolenga kuimarisha ubora wa huduma kwa wanachama, waajiri na wadau.
Cheti hicho kimetolewa baada ya NSSF kukamilisha mchakato wa uhakiki na ithibati ya mfumo wake wa usimamizi wa ubora, hatua inayoweka msingi wa kuendelea kuboresha utendaji, uwajibikaji na ufanisi wa utoaji wa huduma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kitaifa wa Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu, ameipongeza NSSF kwa hatua hiyo, akisema ni ishara ya juhudi zinazofanywa na Mfuko katika kuhakikisha huduma zinaendelea kuimarika.
Babu pia amewataka waajiri wenye malimbikizo ya michango kutumia fursa ya msamaha wa tozo iliyotolewa na Serikali kurekebisha madeni yao na kuendelea kutimiza wajibu wa kulipa michango kwa wakati.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, amesema Mfuko ulikamilisha mchakato wa kupata Cheti cha ISO 9001:2015 hadi Juni 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha huduma zake zinatolewa kwa viwango bora.
“Cheti hiki kinaonesha dhamira ya Mfuko ya kuendeleza huduma bora na uwajibikaji. Hivyo, natumia nafasi hii kuwapongeza TBS kwa kazi kubwa waliyoifanya hadi kufanikisha upatikanaji wa cheti hicho, pamoja na watumishi wote wa NSSF,” amesema Mshomba.

Amesema NSSF pia imepiga hatua katika uandikishaji wa wanachama, ukusanyaji wa michango, uwekezaji, ulipaji wa mafao na matumizi ya TEHAMA.
Kwa mujibu wa Mshomba, thamani ya Mfuko imeongezeka kutoka Sh9.8 trilioni Juni 2025 hadi Sh11.42 trilioni Juni 2026, sawa na ongezeko la asilimia 16.

–
Aidha, amesema wastani wa muda wa kushughulikia na kulipa mafao umepungua kutoka siku 63 mwaka 2021 hadi siku 19 katika mwaka wa fedha 2025/26.
Amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali yameendelea kurahisisha huduma kwa wanachama na waajiri, ambao sasa wanaweza kupata huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.
