Tulia Ackson Aaga IPU, Zungu Achaguliwa Kuongoza Mkutano wa 153 – Video

Global Publishers
October 6, 2026
36 views
0 Comments

ARUSHA: Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, ametoa hotuba yake ya mwisho kwa wajumbe wa umoja huo, akiwashukuru kwa ushirikiano waliompa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake.

Dkt. Tulia ametoa hotuba hiyo Oktoba 6, 2026, wakati wa Mkutano wa 153 wa IPU unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Tulia amesema miaka mitatu iliyopita alipewa heshima ya kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kushika nafasi ya Rais wa IPU, akieleza kuwa uongozi huo umekuwa heshima kubwa kwake binafsi na kwa Taifa la Tanzania.

Mkutano wa 153 wa IPU ulifunguliwa rasmi Oktoba 5 na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika hatua nyingine, Baraza la Uongozi la IPU limemchagua Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu, kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja huo.

Zungu amechaguliwa leo, siku ya pili ya mkutano huo unaowakutanisha viongozi na wajumbe kutoka mabunge mbalimbali duniani.

Hoja ya kumchagua Zungu kuongoza mkutano huo ilitolewa na Spika wa Bunge la Wawakilishi la Uingereza (House of Commons), Sir Lindsay Hoyle, na kuungwa mkono na baadhi ya nchi, zikiwemo Uganda na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Mkutano wa 153 wa IPU ulioanza Oktoba 5 unatarajiwa kuendelea hadi Oktoba 9, 2026, ukiwa na ajenda mbalimbali zinazohusu utawala bora, amani, ushirikishwaji na ushirikiano wa mabunge duniani.