TAMASHA LA BUHA KUTANGAZA FURSA ZA UWEKEZAJI KIGOMA

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

TAMASHA la utamaduni wa kabila la Waha mkoa Kigoma linaelezwa litatumika kutangaza fursa na vivutio mbalimbali vya uwekezaji mkoani Kigoma ikiwemo kwenye masuala ya utalii na malikale.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Stewart Zindutse alisema hayo katika mkutano na waandishi wa habari akitangaza kufanyika kwa tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Desemmba 17 hadi 19 mwaka huu wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

 

Zindutse alisema wakati huu ambapo mkoa Kigoma umeteuliwa kuwa mkoa wa kimkakati kwa uchumi na biashara lakini pia ongezeko kubwa la uwekezaji mkoani humo linaongeza chachu katika uwekezaji kwenye fursa za kutangaza mila na tamaduni za mkoa huo kama sehemu ya uwekezaji kwenye masuala ya utalii na historia hivyo tamasha hilo linabeba kwa nguvu ajenda hiyo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa tamasha hilo limeungwa mkono na wananchi wenye asili ya mkoa Kigoma wanaoishi nchi mbalimbali duniani ambapo wamekubali kushiriki tamasha hilo na kubeba ajenda ya kutangaza utamaduni wa kabila la Waha Kimataifa.

 

Naye Mwenyekiti wa kamati ya habari na mawasiliano , Prosper Kwigize alisema kuwa pamoja na kuonyesha mavazi, vyakula na mambo mbalimbali yenye aasili ya kabila la Waha lakini pia watatumia nafasi hiyo kuibua ajenda ya kuhifadhi utamduni wa Kabila la Waha katika teknolojia ya sasa ya Computer kupitia akili mnemba (AI).

 

Kwigize alisema kuwa awali kabla ya wakoloni Kigoma ilikuwa inajulikana kama Buha Empire kutokana na Kabila la Waha lakini baada ya mabadiliko ya tawala mbalimbali hilo lilibadilika na mkoa huo kuitwa Kigoma hivyo asili ya Buha inapotea hivyo tamasha hilo litaeleza historia hiyo kwa jamii kubwa ya Watanzania ndani na nje ya nchi.