Global Publishers
October 6, 2026
6 views
0 Comments

MKURANGA: Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Kipolisi Rufiji, imemhukumu Juma Mfaume Kombo (20), mkazi wa Kijiji cha Tengere wilayani Mkuranga, kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na kulipa fidia ya Shilingi milioni 3 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi.
Hukumu hiyo imetolewa Oktoba 5, 2026 na Hakimu Sambo, baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka dhidi ya mshitakiwa.
Ilidaiwa mahakamani kuwa Kombo alitenda kosa hilo Mei 1, 2026 katika Kijiji cha Dondwe, wilayani Mkuranga, ambapo alimbaka mwanafunzi wa Kidato cha Pili ambaye jina lake limehifadhiwa kwa ajili ya kulinda utambulisho wake.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano pamoja na kielelezo kimoja kwa lengo la kuthibitisha shtaka lililokuwa likimkabili mshitakiwa.
Baada ya upande wa mashtaka kukamilisha ushahidi wake, mshitakiwa alipewa nafasi ya kujitetea, kabla ya mahakama kupitia ushahidi wa pande zote na kumtia hatiani.
Baada ya kutiwa hatiani, mwendesha mashtaka aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa, akieleza kuwa vitendo vya ubakaji vinaendelea kuongezeka katika jamii na kusababisha madhara makubwa kwa waathirika.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Sambo amesema makosa ya ubakaji yana athari kubwa kwa waathirika katika nyanja za kisaikolojia, kijamii, kiuchumi na kiafya.
Mahakama hiyo hatimaye imemhukumu Kombo kutumikia kifungo cha miaka 30 jela pamoja na kulipa fidia ya Shilingi milioni 3.
