Rais Samia: Tanzania Injivunia kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa IPU – Video

Global Publishers
October 6, 2026
12 views
0 Comments

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali inajivunia kupewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 7, 2026.

Rais Samia ameyasema hayo Oktoba 5, 2026, katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huo, akieleza kuwa Tanzania imelichukulia jukumu la kuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa umuhimu mkubwa.

Amesema nafasi ya Bunge ni muhimu katika kuimarisha utendaji wa Serikali pamoja na kuongeza uwajibikaji kwa wananchi.

“Serikali yangu inalitazama jukumu hilo kwa umuhimu mkubwa, ikitambua kwamba nafasi ya Bunge inaongeza nguvu katika kazi ya Serikali na katika uwajibikaji tunaodaiwa kwa Wananchi wa Tanzania,” amesema Rais Samia.

Kwa mujibu wa Rais Samia, kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni fursa kwa Tanzania kuendelea kushirikiana na mabunge kutoka mataifa mbalimbali katika kujadili masuala yanayohusu maendeleo, uwajibikaji na uimarishaji wa demokrasia.

Mkutano wa 153 wa IPU unawakutanisha wabunge na viongozi wa mabunge kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mustakabali wa mabunge na ushirikiano wa kimataifa.

Mkutano huo unaendelea Arusha hadi Oktoba 7, 2026.