Chivayo na Mkewe Kuzikwa Bila Vichwa, Familia Yafichua Kilichopatikana

HARARE, Zimbabwe — Mfanyabiashara wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, na mkewe, Lucy Muteke, wanatarajiwa kuzikwa Alhamisi katika makaburi ya Glen Forest, Harare, huku familia ikisema sehemu za vichwa vyao bado hazijapatikana baada ya ajali mbaya ya helikopta.

Chivayo na Lucy walifariki Jumatano iliyopita baada ya helikopta aina ya Bell 430 waliyokuwa wakisafiria kuanguka katika eneo la Kudenga Farm, Marondera.

Wanandoa hao walikuwa wakisafiri kutoka nyumbani kwao Gandami, Chikomba East, wakati ajali hiyo ilipotokea. Watu wengine watatu waliokuwa ndani ya helikopta hiyo pia walifariki.

Kwa mujibu wa msemaji wa familia, Hebert Chivayo, nguvu ya ajali hiyo ilisababisha miili kusambaratika, huku baadhi ya mabaki yakiteketea kwa moto. Hadi sasa, vichwa vya marehemu hao havijapatikana.

Akizungumza na waandishi wa habari, Hebert alikanusha taarifa zilizosambaa mitandaoni kwamba mafuvu manne yalikuwa yamepatikana.

“Hatukupata kichwa chochote. Kulikuwa na baadhi ya vipande vya mifupa vilivyodhaniwa kuwa mafuvu, lakini haikuwa hivyo,” alisema.

Alisema vitu vya mwisho vilivyotambuliwa vilikuwa saa ya mkononi ya Chivayo na saa ya Lucy.

Familia pia imesema hakutakuwa na kuonyeshwa miili kwa mara ya mwisho kabla ya mazishi kutokana na hali ya mabaki yaliyopatikana.

Chivayo na Lucy watazikwa makaburi mawili tofauti lakini ya karibu, licha ya taarifa zilizodai kuwa wangezikwa katika kaburi moja.

Hebert pia alikanusha madai kwamba mazishi hayo yatakuwa ya watu wachache au ya familia pekee, akisema mtu yeyote anayetaka kushiriki katika maombolezo anakaribishwa.

“Wicknell alikuwa mtu wa watu wote, maskini na matajiri. Hakuwa mchaguzi,” alisema.

Mazishi hayo yanatarajiwa kufanyika katika makaburi ya Glen Forest mjini Harare, huku waombolezaji wengine wakitarajiwa kukusanyika katika makazi ya marehemu yaliyopo Gletwin Park.

Chivayo ametangazwa kuwa shujaa wa mkoa (provincial hero) na serikali ya Zimbabwe.