ASKOFU MLAWI: RAIS SAMIA ANA MAADUI, TUMUOMBEE HEKIMA

NA HAMIDA RAMADHAN, MATUKIO DAIMA MEDIA DODOMA

ASKOFU wa Makanisa ya Kipentekosti na Rais wa TPA, Dkt. Mussa Mlawi, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anakabiliwa na maadui wengi, akiwataka Watanzania kumuombea ili Mungu ampe hekima na busara katika kuiongoza nchi.

Dkt. Mlawi amesema kupewa dhamana ya kuongoza nchi si jambo dogo, hivyo Rais anahitaji hekima, busara na msaada wa Mungu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika uongozi.

Akizungumza kwenye kanisa la Spiritual Pentecoste Church of Tanzania (SPCT)Oktoba4,2026 lililopo Chamwino Ikulu Jijini Dodoma kwenye Ibada maalumu ya Usimiko na pongezi kwa Makamu wa Rais wa Tanzania Deogratius Ndejembi amesema aliwahi kupeleka barua ya maono 14 aliyooteshwa kuhusiana na uongozi wa Rais Samia na kugoma kuyaweka bayana na hivyo anaomba nafasi ya kukutana nae tena amwelezee na aweze kuyafanyia kazi ili uongozi wake utamatike kwa ufasaha.

Amesema anaomba kukutana na Rais kwa kuwa anaamini huenda baadhi ya mambo hayo hayajamfikia moja kwa moja, hivyo angependa kupata nafasi ya kuyawasilisha mwenyewe kwa Mkuu wa Nchi.

“Naomba kuonana tena na Rais Samia ili nimfikishie mambo 14 ambayo hayajatekelezwa. Ninaona huenda ujumbe huu haujamfikia moja kwa moja,” amesema.

Dkt. Mlawi amesema dhamira yake ni kumsaidia Rais kupata taarifa na maoni ambayo anaamini yanaweza kuwa muhimu katika kuendelea kuimarisha uongozi na maendeleo ya Taifa, akisisitiza kuwa maombi yake hayalengi kumshambulia Mkuu wa Nchi.

Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kumheshimu Mungu na Rais Samia, akisema nafasi aliyonayo ni dhamana kubwa ambayo inahitaji kuungwa mkono kwa maombi na ushauri unaolenga maslahi ya Taifa.

Amesema Rais Samia anapaswa kuendelea kuongoza bila ubaguzi wa dini wala kabila, ili kila Mtanzania ajione kuwa sehemu ya Taifa na kupata fursa ya kushiriki katika maendeleo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mlawi amempongeza Makamu wa Rais,Deogratius Ndejembi, kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini, akimtaka kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu na kwa kuzingatia maslahi ya Watanzania.

Amesema viongozi waliopo katika nafasi za juu wanapaswa kuwa karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuhakikisha hoja zinazowasilishwa zinapatiwa majibu na hatua stahiki.

Dkt. Mlawi pia ameiomba Serikali kuikumbuka Chamwino katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akitaja ujenzi wa barabara za lami na uwekaji wa taa za barabarani kuwa miongoni mwa mahitaji muhimu kwa wananchi wa eneo hilo.

Amesema uwepo wa barabara bora na taa za barabarani utasaidia kuimarisha usalama, kurahisisha usafiri na kuongeza fursa za shughuli za kiuchumi kwa wananchi.

Akizungumzia uhusiano wake na uongozi wa Taifa, Dkt. Mlawi amesema tangu mwaka 2023 alipodai kupata maono kuhusu safari ya Rais Samia, ameendelea kufuatilia masuala ya uongozi na maendeleo ya nchi.

Amesema viongozi wa dini wana wajibu wa kuwaombea viongozi wa Serikali, kutoa ushauri na kuhimiza amani na umoja wa Watanzania, huku akisisitiza kuwa dhamira yake ni kuona Taifa likiendelea kuwa na amani, mshikamano na maendeleo.

Lakini pia katika ibada hiyo waliombea taifa na wakulima mvua kubwa zinazozaniwa kunjesha msimu huu zisilete madhara. 

Naye Rev. Elesiana Buguzi kutoka Ufalme wa Mbinguni Ministry amesema wanaamini kuwa kupitia maombi hayo, mvua za El Niño hazitasababisha madhara, bali zitakuwa na tija kwa taifa na wananchi kwa ujumla.

“Tunayo imani kwamba kupitia maombi haya, mvua za El Niño hazitaleta madhara, bali zitakuwa na tija kwa taifa na wananchi kwa ujumla,” amesema Rev. Elesiana.

Mwisho