Global Publishers
October 5, 2026
0 views
0 Comments
LOS ANGELES, Marekani — Staa wa televisheni na mfanyabiashara, Kim Kardashian, amefunguka kuhusu kipindi alichokaa bila kuwa katika uhusiano wa kimapenzi baada ya kuvunjika kwa ndoa yake na mwanamuziki Kanye West.
Kim alisema kipindi hicho kilikuwa muhimu kwake kwani kilimpa nafasi ya kujikita zaidi katika kulea watoto wake, kazi pamoja na miradi yake ya biashara.
Kwa mujibu wa Kim, licha ya kuwa aliwahi kuwa katika uhusiano na mchekeshaji Pete Davidson baada ya kutengana na Kanye, kwa ujumla alitumia takriban miaka mitano akiwa bila uhusiano wa kimapenzi wa kudumu.
Kim alisema hakuhisi shinikizo la kukimbilia uhusiano mwingine, akieleza kuwa alihitaji muda wa kujiponya na kujifanyia kazi.

“Nilihisi vizuri kuwa single. Niliweza kuzingatia watoto wangu na miradi ambayo nilitaka kuhusika nayo,” alisema Kim katika mahojiano ya hivi karibuni.
Alisema pia hakujihisi mpweke wala kuwa na haraka ya kumpata mtu mwingine, akiamini kuwa alihitaji kwanza muda wa kujitengeneza upya kabla ya kufungua moyo wake tena.
Kim na Kanye West walifunga ndoa mwaka 2014 na walijaliwa watoto wanne. Kim aliwasilisha ombi la talaka mwaka 2021, huku ndoa yao ikikamilishwa kisheria mwaka 2022.
Baada ya kutengana, Kim alianza uhusiano na Pete Davidson ambao uliendelea kwa takriban miezi tisa kabla ya wawili hao kuachana mwaka 2022.
Kwa sasa, Kim amesema anathamini zaidi maisha yake, watoto wake na kazi zake, huku akionekana kuwa katika hatua tofauti ya maisha yake ya kimapenzi.

